Kwanini Polisi katika majiji makubwa bado wanatumia farasi?

Jamii Africa

Kila nchi inafanya juhudi mbalimbali kuwapa Askari wake vifaa vya kisasa kuimarisha utendaji wao. Hapo zamani, Polisi walikuwa wanatumia bastola au bunduki tu lakini Askari wa sasa au tunaweza kuwaita wa kisasa katika nchi mbalimbali wamewezeshwa kwa vifaa ikiwemo matumizi camera, vinasa sauti, radio n.k.

Ni halali wakati mwingine kusema ni kama idara za Polisi ziko kwenye mashindano ya teknolojia ya kijeshi.

Bado nchi nyingi, haijalishi kwa kiasi gani zimepiga hatua ya maendeleo, zinatumia sheria na njia ya zamani za kipolisi kwa Askari kupanda Farasi na kuzunguka katikati ya jiji. Kama unaangalia runinga utakuwa umeshuhudia Maafisa Polisi wamepanda Farasi hasa katika majiji makubwa ya New York (Marekani), London, Berlin (Ujerumani) na hata Dar es Salaam.

Umewahi kujiuliza au kushangaa kwanini majiji hayo yaliyoendelea duniani bado yanatumia Farasi katika shughuli zao za kipolisi na kuzunguka kwenye mitaa? Kuna sababu kwa nchi zilizoendelea na hata zile zinazoendelea kuwa na kikosi maalumu cha Farasi:

 Kudhibiti umati

Hii ndio sababu kubwa inayokubalika kwanini Polisi wanatumia farasi kwenye majiji makubwa. Farasi zinaweza kupenya kwa urahisi katikati ya umati wa watu na ni rahisi kwa polisi kuwaona watu vizuri kwasababu farasi ana kimo kirefu. Ukiwa juu ya farasi unaona vizuri na ni rahisi kwa mpandaji kuwa tayari kwa lolote wakati akitekeleza majukumu yake.

Polisi wanaotumia farasi wana uwezo mkubwa wa kuvunja na kutawanya mkusanyiko wenye fujo, hasa kwenye mechi za mpira wa miguu. Fujo za mashabiki wa timu mbili pinzani zinaweza kudhibitiwa na askari mmoja aliyepanda farasi.

Sababu ya askari wanaoutumia farasi kuwa na ufanisi mkubwa hasa kudhibiti na kutawanya umati wa watu ni kwamba farasi ni mnyama mkubwa. Ukisimama mbele yao na wakakusukuma unaweza kukimbia mbali nao. Pia kuna hofu ya ndani ambayo binadamu anayo kuhusu wanyama wakubwa ambayo inahusishwa na watu kuogopa wanyama hao ambao wanaweza kudhuru.

Kwa kuongezea ni kwamba watu hawatafikiri mara mbili kabla ya kuharibu au kuchoma gari la Polisi wakati wa fujo, lakini ni tofauti kabisa kwa mnyama mkubwa ambaye unafikiri unagombana naye- mnyama huyo anaweza kupambana na wewe na kukudhuru.

Ukweli ni kwamba kuna mifano hai nchini Uingereza ambako askari 3 hadi 4 waliopanda farasi walisababisha umati wa watu wenye hasira kutawanyika kwa muda mfupi, jambo lililoshindwa kufanywa na Askari wengi wa kikosi cha kutuliza ghasia.

 

Ni rahisi kupenya

Farasi zinaweza kukimbia na kupenya kwenye maeneo yaliyobanana kama mitaa yenye maduka, pembezoni mwa barabara. Japokuwa magari yanaweza, kitaalamu kupita katika maeneo hayo haishauriwi kwasabau ya kelele au yanaweza kutumika tu kwenye maeneo fulani na kusababisha msongamano kwenye mitaa.

Farasi wanaweza kupenya kwenye mitaa iliyobanana lakini pia wanaweza kwa haraka kutawanya watu (kwa ujumla watu wakiona farasi anakuja, hukimbia)

Kwa kuongezea farasi zinaweza kutumika katika maeneo ambayo magari hayawezi kupita, kama maeneo madogo ya kuingilia sehemu za starehe, klabu au polini.

 

Kutafuta na kuokoa

Askari wanaopanda farasi wanafundishwa pia kusimamia shughuli za utafutaji na uokoaji. Wanabeba vifaa vingi na kuendelea kutafuta kwa muda mrefu hasa katika maeneo ambayo magari ya polisi hayawezi kwenda.

 

Uoni

Kazi ya kwanza ya askari polisi yoyote yule ni kuzingatia sheria na utaratibu wa mitaa. Wazo la kutumia kikosi cha farasi ni kuchukua tahadhari mapema na kuzuia ugomvi au mtafaruku kwenye mitaa kabla haujawa mkubwa ambao unaweza kuhatarisha maisha ya watu waliopo eneo husika.

Polisi aliye juu ya farasi ana faida kubwa ya urefu/kimo ukilinganisha na aliyepo kwenye gari kwasababu ni rahisi kuona, kwahiyo farasi ni njia nzuri ya kufanya dolia kwenye mitaa yenye shughuli nyingi.

Sio tu askari aliyepanda farasi anaona vizuri maeneo ya dolia lakini inasaidia watu wengine waliopo kwenye mitaa kumuona kwa urahisi na kumsogelea ikiwa atahitajika kutoa msaada.

 

Historia na Utamaduni

Farasi anahusishwa kwenye historia, tamaduni na desturi za nchi nyingi duniani. Katika maeneo kama Sweden na Scotland, askari anayepanda farasi sio tu anatumikia Jeshi la Polisi, lakini anawakilisha utambulisho wa jinsi farasi anavyotimiza majukumu yake kikamilifu ambayo hayawezi kufanywa na mtu mwingine (ni heshima na fahari).

 

Urafiki na kuvutia

Watu wengi wanafikiri askari wanaopanda farasi kwa kiasi fulani wanaonekana kama ni marafiki, wanafikika na kuvutia kuliko polisi ambao wako kwenye magari yaliyo na vioo vikubwa. Watu wengi wanaweza kumsogelea askari aliyepanda farasi kuliko yule aliyepo kwenye gari.

Katika maeneo mengi, watu huwapungia mkono askari waliopanda farasi na kuwaambia ‘Hello’ jambo linalotengeneza urafiki kati ya askari hao na wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *