LHRC kuungana na MCT kutafuta tafsiri ya ‘Uchochezi’ mahakamani

Jamii Africa

Siku moja baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuvipiga faini vituo vya runinga vya Star TV, Azam, Channel  Ten, EATV na ITV kwa kukiuka maadili ya uandishi na  kutangaza habari zinazodhaniwa kuwa  za kichochezi,  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetofautiana na  hatua hiyo na kinakusudia kwenda mahakamani kupata tafsiri sahihi ya neno ‘Uchochezi’.

Adhabu hiyo ilitolewa jana na TCRA ambapo vituo hivyo vya runinga vilitozwa faini jumla ya shilingi milioni 60 baada ya kutangaza habari ya LHRC juu ya  tamko la tathmini ya uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani uliofanyika katika kata 43 kwenye mikoa 19 ya Tanzania  Novemba 24 mwaka jana ambapo kilibaini mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tathmini hiyo iliibua mambo mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kujeruhiwa  kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi  na vilevile kuwatia hofu wapiga kura.

Inaelezwa kuwa  habari hiyo ilitangazwa Novemba 30, 2017 na vituo vya runinga (vilivyotajwa hapo juu) ililenga kuhatarisha amani ya nchi na taifa kinyume na kanuni za utangazaji za mwaka 2015.

Lakini hata hivyo adhabu hiyo inaonekana  ni hatua ya kudidimiza uhuru wa vyombo vya habari nchini ikizingatiwa kuwa uchaguzi  huo uligubikwa na matukio mengi ya uvunjaji wa haki za binadamu ambapo  wanahabari walitimiza wajibu wao wa kuhabarisha umma.

Akizungumza leo  jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dr. Hellen Kijo Bisimba amesema  maazimio hayo ya TCRA ni ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na serikali inapaswa kuwa tayari kupokea maoni tofauti ili kujenga jamii inayoheshimu misingi ya demokrasia.

“Kuna kuendelea kukiukwa kwa ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 juu ya haki ya uhuru wa kujieleza hususani haki ya kupata na kutoa taarifa juu ya maswala muhimu yanayohusu jamii”, amesema Dr. Hellen Kijo Bisimba.

Amesema mamlaka hiyo ingetumia njia za kikatiba kubaini upotoshaji uliofanywa na kujibu hoja za msingi zilizotolewa na tathmini ya LHRC iliyotangazwa kwenye runinga na siyo kuviadhibu vyombo hivyo vilivyotimiza majukumu yanayotambulika kisheria.

“Upande wowote ambao ulihisi kuwepo kwa upotoshaji walitakiwa  kutumia haki yao kikatiba kutoa hoja zao na si kutumia mamlaka kuviadhibu vyombo vya habari. Kanuni ya 8 ya kanuni ya maudhui ya vyombo vya habari ya mwaka 2005 inavitaka vyombo vya habari kuwa na mizania kwa taarifa za kiuchunguzi. Taarifa iliyoripotiwa toka LHRC haikuwa ya kiuchunguzi hivyo haikuhitaji mizania”, amesema Dr. Hellen Kijo Bisimba

Amebainisha kuwa wataendesha harambee ya kuvisaidia vyombo vilivyokumbwa na adhabu hiyo ili viendelee kutekeleza shughuli za kila siku na wakati huohuo wanakusudia kwenda mahakamani kupata tafsiri sahihi ya neno ‘uchochezi’ ambalo limekuwa likitumiwa na baadhi ya mamlaka za serikali kuwatia hatiani watu wanaotoa maoni juu ya mustakabali wa taifa.

“Tunaungana na wadau ambao wapo tayari kwenda Mahakamani kuomba tafsiri ya neno Uchochezi na pia tafsiri ya kifungu cha kanuni ya maudhui hususani kifungu cha 8 katika mazingira ya utawala wa serikali dhidi ya raia”, amefafanua Dr. Hellen Kijo Bisimba.

Kwa upande wake, Baraza la Habari Tanzania (MCT), limetangaza siku ya jana kutafuta ufafanuzi wa kisheria mahakamani wa tafsiri ya makosa ya kiuchochezi.Hatua hiyo inakuja kufuatia ongezeko la adhabu kwa vyombo vya habari nchini ikiwemo faini, kufungiwa na kukemewa.

Kwa mujibu wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, vituo hivyo vya runinga vimetiwa hatiani kwa makosa matatu chini ya kifungu cha 5 na 6 cha Kanuni ya Maudhui ya mwaka 2005 na kupigwa faini kwa viwango tofauti pamoja na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 6.

 

Uhuru wa Vyombo Vya Habari nchini

Mwaka 2017, serikali iliyafungia magazeti kadhaa yakiwemo Raia Mwema, Tanzania Daima, MwanaHalisi kwa makosa mbalimbali ya uchochezi lakini kasi hiyo inawatisha wadau wa masuala ya habari duniani ikizingatiwa kuwa uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi ambayo inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote ili kujenga jamii iliyostaarabika.

Kulingana na Utafiti wa Twaweza (2016) unaeleza kuwa  “Uhuru wa kujieleza umekuwa ukikabiliwa na vitisho vikali ambapo polisi wamekamata watu 358 kwa mwaka 2015 na watu 911 mwaka 2016 kwa kosa la kutumia lugha mbaya”.

Hata hivyo, ili kusimamia maudhui na ukuaji wa tasnia ya habari nchini, sheria mbalimbali zimepitishwa ikiwemo; Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Habari (2016) na Sheria ya Takwimu (2015). Lakini changamoto inajitokeza ni jinsi sheria hizo zinavyotekelezwa ambapo zinatajwa kuminya uhuru wa kujieleza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *