Lions Club, Halmashauri ya Morogoro yawatelekeza wanafunzi iliyowaahidi kuwasomesha

Jamii Africa

 Mkuu wa Chuo akataa kuwapokea mpaka walipe ada

– Lions Club Morogoro yasema ilikuwa hisani tu kwa wanafunzi hao 

Wanafunzi 24 wa Chuo Cha Uuguzi Cha Berega kilichopo Kilosa mkoani Morogoro wametelekezwa na mfadhili wao Chama Cha Lions Clubs Morogoro ambalo liliahidi kuwasomesha na kuwatafutia ajira baada ya kumaliza masomo.

Wanafunzi hao waliingia kwenye makubaliano na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Lions Club Morogoro kwa niaba ya Shirika la International Lions Club Association kutoka Sweden ambao walianza masomo katika chuo hicho mwaka jana kwa makubaliano ya Halamashauri ya Wilaya ya Morogoro na wafadhili hao kuwalipia ada za masomo kwa kipindi chote watakachokuwepo chuoni.  

Wanafunzi hao walidahiliwa katika chuo hicho katika kozi ya uuguzi ngazi ya cheti miaka 2 na Diploma kwa miaka 3 ambapo hulipa ada ya shilingi milioni 2 na laki tano (milioni 2.5) kila mwaka.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya wanafunzi  hao kutoka likizo na  kulipoti chuoni hapo ili kuanza masomo ya mwaka wa pili, ambapo uongozi wa chuo ulikataa kuwapokea kwa sababu shirika la Lions Club limekataa kuendelea kugharimia masomo ya wanafunzi hao.

Mwanafunzi mmoja (jina lake tunalihifadhi) anasema walilipoti chuoni hapo tarehe 30 Septemba 2017 lakini walipata taarifa kutoka kwa mkuu wa Chuo hicho cha Berega Nursing School, Wilbard Mrase kuwa hawatakiwi kuonekana katika mazingira ya chuo mpaka walipe ada na madeni ya nyuma wanayodaiwa.

“Hivyo sisi ilipofika tarehe ya kufungua chuo tukarejea chuoni  kwani ndiyo tarehe ya kufungua, tulipofika kuripoti ofisini, Mkuu wa Chuo akadai twende kwa Mhasibu wa Chuo  anajua utaratibu. Baada ya kutusikiliza na kujadili naye Mhasibu yeye akasema swala letu haliwezi hivyo akaenda kuongea na mkuu wa chuo” anaeleza mwanafunzi huyo na kuongeza kuwa,

“Baada ya muda si mrefu mkuu wa chuo akaja kwa madai ya kuzungumza na sisi lakini cha kushangaza hajatusikiliza wala kuturuhusu kuzungumza chochote, akaongea yeye mwenyewe mwanzo mwisho akiwa na jazba na kutoa maamuzi kuwa sisi tuondoke”.

Fikra Pevu imefahamishwa kuwa Mkuu huyo wa Chuo, Wilbard Mrase hakuwasikiliza wanafunzi lakini aliwaamuru waondoke chuoni kwa sababu amewasiliana na Lions Club ambao ni wafadhili  akidai kuwa wamekataa kuendelea kugharimia masomo ya wanafunzi hao.

“Alisema chuo hakitupokei mpaka tuje na pesa ya mwaka huu na madeni ya nyuma akidai amewasiliana na wafadhili na kumueleza kuwa hawataweza kulipa tena” anaeleza mwanafunzi huyo kwa uchungu.

Mwanafunzi mwingine ambaye ni miongoni mwa wanafunzi hao 24 (jina tumelihifadhi), anasema walimtaka Mkuu huyo wa Chuo kuwapa barua ya maandishi inayoonyesha wafadhili hao kusitisha ufadhili wao lakini hawakupewa barua hiyo na kuamriwa kuondoka chuoni.

“Pamoja na hayo wamesema hawataendelea kulipa pesa lakini hakuna  maandishi yanaonyesha  Lions Club wamekataa kulipa hizo pesa  na sisi kutokana na familia zetu kuwa duni hatuna uwezo kuwalipa hizo pesa”,  Anaongea mwanafunzi huyo wa mwaka wa pili katika Chuo Cha Berega ambapo anaonyesha hali ya kutoa machozi kutokana na uchungu alionao,  “Hatujapokelewa tunalala chini, hatupewi chakula maisha ni magumu” 

Wanafunzi hao hawakukata tamaa, kwa sababu walifahamu haki yao ipo na wataipata kwa njia yoyote. Walifunga safari mpaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kufanikiwa kumuona Mkuu wa Mkoa huo, Steven Kebwe. Walimueleza changamoto wanayokabiliana nayo.

“Tulijitahidi sana kuomba tupewe barua lakini hatukupewa na ilipofika jumatatu usiku tuliondoka, Jumanne tarehe 03/10/2017 tukaamua kurudi ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro” anasema mwanafunzi huyo.

Katika kuwasaidia wanafunzi hao, Mkuu wa Mkoa aliwasiliana na mwakilishi wa Lions Club ambapo alipewa majibu kama yaliyotolewa na Mkuu wa Chuo cha Berega kwamba Lions Club hawana nia ya kuendelea kuwasomesha wanafunzi hao.

Licha ya kupata majibu hayo, walizidi kuhoji sababu za Lions Club kusitisha ufadhili wao lakini hawajapata majibu zaidi ya kupokea vitisho kutoka kwa watendaji wa serikali katika Wilaya ya Morogoro.

“Mkuu wa Mkoa alipofanya mawasiliano na muwakilishi wa Lions Club kupitia simu akajibiwa kuwa wafadhili wamejitoa japo sisi hajatueleza sababu na hatima yetu hasa ni nini zaidi ya kutushauri turudi halmashauri, ambako halmashauri huko sisi walishindwa kutusaidia tangu awali”, anafafanua mwanafunzi huyo.

                                                     Sehemu iliyosainiwa ya makubaliano ya kuwasomesha wanafunzi

Makabaliano ya Awali

Mgogoro huo wa wanafunzi na uongozi wa Chuo haujaanza leo, kinachotokea leo ni matokeo ya makubaliano ya awali kuvunjwa.

Fikra Pevu imeelezwa kuwa mwaka 2016 Halmashauri ya wilaya ya Morogoro kupitia Mganga Mkuu Wilaya (DMO) walitangaza nafasi za kuomba ufadhili kutoka Lions Club ili kuwasomesha wanafunzi katika fani ya uuguzi ngazi ya cheti na diploma  katika vyuo vya Uuguzi vya Berega, Lugala na  PHN ambavyo viko mkoani Morogoro. 

Lengo la ufadhili huo lilikuwa ni kuongeza idadi ya wafanyakazi wa afya katika wilaya hiyo ambapo wanafunzi hao waliahidiwa kupata kazi baada ya kumaliza masomo katika Wilaya ya Morogoro. Makubaliano ilikuwa ni kufanya kazi katika vituo vya afya vya Wilaya hiyo kwa muda wa miaka minne na baadaye kutafuta sehemu nyingine. 

Mwanafunzi wa Chuo cha Berega (jina tumelihifadhi) anasema “ Vijana wengi tuliona kama ndio nafasi ya ukombozi kutokana na uhalisia wa familia zetu kutokuwa na uwezo wa kutusomesha hivyo tulifuatilia hilo jambo kupitia mawasiliano yaliyowekwa kwenye tangazo”.

Vijana  24 kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro walichaguliwa kujiunga na Chuo Cha Berega. Ili kukamilishwa makubaliano ya mkataba huo, walifika katika Ofisi za  Mkurugenzi wa Wilaya ya Morogoro ili kukutana na pande zote akiwemo mfadhili ambaye ni Lions Club.

Mkataba huo ilihusisha watu 3 ambao ni wanafunzi (ambao ni wafanyakazi wa baadaye wa Wilaya ya Morogoro), Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro (muajiri wa baadaye) na Lions Club Morogoro kwa niaba ya shirika la International Lions Club Association Sweden ambaye ni mfadhili. Mkataba ulisainiwa kwa makubaliano ya Lions Club kuwalipia wanafunzi hao ada kwa kipindi chote watachokuwepo chuoni na baada ya kumaliza masomo kuajiriwa katika wilaya hiyo.

                                                                             Sehemu ya Mkataba huo

Lions Club waliahidi kumlipia kila mwanafunzi milioni 2 na laki tano (2.5) ambayo ni ada ya mwaka na fedha hiyo ingekuwa inapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya chuo.

Kwa upande wao wanafunzi hao walitakiwa kugharimia sare za chuo, fedha ya kitambulisho cha mwanafunzi, karatasi za mazoezi (A4-Rim Paper) na mchango wa serikali ya wanafunzi.

Muda wa masomo ulipowadia, 24 Septemba 2016 walilipoti katika chuo cha Berega Nursing School kilichopo Kilosa Morogoro siku ambayo waliwakuta wanafunzi wengine 11 wa mwaka wa pili ambao nao walipata ufadhili kutoka Lions Club.  

Wanafunzi hao waliendelea na masomo kama kawaida lakini wakati wanakaribia kufanya mitihani ya muhula wa kwanza, walipata taarifa kutoka kwa uongozi wa chuo kuwa Lions Club hawajalipa fedha kama walivyokubaliana.

Uongozi wa chuo ulipata mshtuko kutokana na wafadhili hao kuwa na tabia ya kulipa pesa yote tena kwa wakati. Na walifanya hivyo kwa wanafunzi 11 ambao walianza katika mwaka wa masomo wa 2015/2016.

 

Mambo yabadilika, wanafunzi watakiwa kulipa ada wenyewe

Chuo kiliwasiliana na Lions Club ili kujua kuna tatizo gani limetokea. Ikumbukwe kuwa wanafunzi hao 24 walikuwa hawawasiliani moja kwa moja na wawakilishi wa Lions Club kutokana na makubaliano ya awali kuwa wangepata mrejesho wa kila kinachoendelea kupitia uongozi wa chuo.

Siku chache baadaye wawakilishi wa Lions Club walifika katika chuo hicho na taarifa iliyotolewa ni kuwa fedha ambazo zilikuwa za wanafunzi zimepotea na wanafanya utaratibu mwingine wa kuwasaidia wanafunzi hao.

Inasemekana baada ya kumaliza mitihani ya muhula wa kwanza chuo kilitoa taarifa kwa wanafunzi hao kutakiwa kulipa wenyewe ada ya chuo ambayo ni milioni 2.5 kwa mwaka. Kwa mujibu wa wanafunzi hao walikataa kwa sababu masharti hayo mapya yalikuwa yanavunja mkataba wa awali.

Baada ya kumaliza mitihani ya muhula wa kwanza tulipewa taarifa kwenda kwa wazazi kuhusu wao kutakiwa kulipia ada ya chuo million 2.5. Sisi hatukukubaliana na swala hilo la kupeleka mzigo huo kwa wazazi maana si wao waliotupeleka pale, chuo kikatupinga”, anafafanua mmoja wa wanafunzi hao.

 

Siku chache baadaye

Mgogoro huo baina ya wanafunzi na chuo uliendelea kutokota na ikawalazimu wanafunzi hao kuandika barua ya malalamiko tarehe 6 Februari, 2017 kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Sudi Mpili kupitia kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Dkt. Alen Mlekwa. Barua hiyo ilipomfikia Mkurugenzi huyo haikufanyiwa kazi na ndipo wanafunzi hao wakaonana moja kwa moja na Mkurugenzi huyo lakini hawakupata majibu ya kuridhisha.

Wanafunzi hao hawakukata tamaa walisonga kudai haki yao, siku ya 19 Aprili 2017 walifunga safari tena kumuona Mkuu wa Wilaya ya Morogoro. Naye pia hakuonyesha nia ya kuwasaidia na hawakupata majibu ya kuridhisha.

“Tulichukua jukumu la kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Morogoro, tulipeleka barua pamoja na kuonana naye ana kwa ana. Kwa jinsi alivyotupokea na kulisikiliza jambo letu hakika siku hiyo tulitoka tumeghafilika sana pale ofisini”, anaongea mwanafunzi mwingine amabye jina lake pia tumerihifadhi na kuongeza kuwa,

“Wengi wetu walikata tamaa lakini tukajipa moyo, tuliwasilisha majibu ya Mkuu wa wilaya kwa njia ya simu kwa Mkuu wa chuo, tukajibiwa chuo hakiwezi pokea mtu pasipo pesa hata kidogo, Baadhi yetu tulijitahidi kupata hata hiyo pesa kidogo hatimaye tukarejea chuoni, wenzetu tisa (9) walishindwa kupata pesa hata kidogo walau warudi chuoni hivyo huo ndio ukawa mwisho wa wao kuwepo chuoni”.

Chuo kiliendelea na msimamo wake wa kutowahitaji wanafunzi hao mpaka walipe ada. Wanafunzi kwa ujasiri walisonga mbele mpaka ngazi ya juu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuonana na Mkuu wa Mkoa ambaye aliwasikiliza na kuagiza uongozi wa chuo hicho kuwapokea wanafunzi hao wakati wanasubiri ufumbuzi wa mgogoro huo.

“Alitusaidia kufanya mawasiliano na mkuu wa chuo na kumtaka aruhusu wanafunzi warudi chuoni, ingawa mkuu wa chuo hakutekeleza kiuhalisia, alidai mpaka aletewe barua rasmi toka kwa mkuu wa mkoa, hivyo kila mtu alirejea chuoni kwa utaratibu anaoujua mwenyewe ikiwemo hata kutoa ahadi kuwa atalipa japo kiuhalisia uwezo wa kulipa hatukuwa nao wengi wetu” anaongea mwanafunzi huyo.

Wanafunzi hao walifanikiwa kurudi Chuoni na kuendelea na masomo katika muhula wa pili ambapo Lions Club kwa mara nyingine walifika chuoni hapo kuleta fedha za wanafunzi 5 ambao wote walikuwa miongoni mwa wanafunzi 11 wa mwaka wa pili ambao kwa sasa wamemaliza masomo yao.

Wanafunzi hao wanadai kuwa chuo hakina utaratibu wa kuwashirikisha mambo yote yanayoendelea kati yao na wafadhili, jambo ambalo linawaweka katika wakati mgumu kwa sababu hawana mawasiliano ya moja kwa moja na Lions Club.

“Taarifa za sisi kulipa pesa tulipata kupitia uongozi wa chuo kwa sababu sisi hatuna mawasiliano ya moja kwa moja na lions club. Mkuu wa chuo alituita na kutuambia kuna pesa za watu 5 zimeiingizwa. Kwa kuwa lions Club wameonyesha nia ya kulipa ninyi endeleeni kusoma na sisi tumekubali huu utaratibu wa wao, huwezi kujua kesho wanaweza kulipa fedha ya watu wengine”.

Baada ya kumaliza masomo yao mwaka wa kwanza walienda likizo na kurejea chuoni hapo tarehe 30 Septemba 2017 kuanza masomo ya mwaka pili lakini chuo bado kimeshikilia msimamo wake wa kutowatambua wanafunzi hao mpaka walipe ada.

 

Malalamiko ya wanafunzi

Wanafunzi hao ambao wako katika hatari ya kukosa sifa ya kuendelea na masomo kwa sababu mpaka sasa wako nje ya chuo kwa wiki 2 tangu wafungue chuo. Wamejaribu njia mbalimbali kupata ufumbuzi wa tatizo lao lakini hakuna anayewasikiliza ambapo mmoja wao ameimbia Fikra Pevu kuwa,

“Tumerudi chuoni tukijua lions club wanalipa pesa kidogodogo, mambo yamebadilika hatujapokelewa chuoni kwa kuwa uongozi wa chuo unahitaji sisi tuendelee kujilipia zile pesa  wakidai  Lions Club wamesema hawawezi tena kuendelea kulipa pesa”.

‘Familia zetu ni duni tunaishi katika mazingira magumu, tunagawana chakula na wenzetu, tunaenda mtaani kuomba omba. Mkuu wa chuo amekataa kutusikiliza na  kutuandikia barua kwa Lions Club”.

Naye mwanafunzi mwingine anasema “niwaombe serikali watusaidie maana viongozi wa wilaya wameshindwa kutusaidia na wanatupa vitisho. Sisi pekee yetu hatuwezi hatusikilizwi kwa wakati”.

Hata hivyo, wameiomba serikali iwasaidie kwa sababu hawajapata barua rasmi kutoka Lions Club inayoonyesha kuwa shirika hilo limesitisha ufadhili huo.

 

Kauli ya Lions Club

Mwakilishi wa Chama cha Lions Club kutoka Morogoro ambaye alitambulika kwa jina la Dkt. Peter Nkulila amesema shirika hilo liliamua kutoa msaada wa kuwalipia ada wanafunzi hao na sasa hawana fedha. 

“Ilikuwa ni hisani tu sio ufadhili,kama mwenye hisani hajaleta hela? Wahisani walisema watawasaidia sasa hawana hela, wana wazazi na ndugu kama nyinyi wanaweza kuwasaidia”

Hata alipoulizwa kuhusiana na makubaliano ya awali waliyoingia na wanafunzi hao, mwakilishi huyo amesema shirika hilo halikuingia makubaliano na wanafunzi wa Chuo Cha Berega bali Halmashauri ya Morogoro ndio wana dhamana na wanafunzi hao.

“Hawakuingia mkataba na Lions Club, kazungumze na Mwenyekiti wa Halmashauri (Wilaya ya Morogoro) wao ndio wenye mradi wa serikali”.

 

Mkuu wa Chuo Cha Berega akataa kuzungumza

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Berega School of Nursing, Wilbard Mrase, alipotafutwa kwa njia ya simu alikataa kulizungumzia suala hilo na alimtaka mwandishi wa Fikra Pevu kufika ofisini kwake ili ampatie taarifa kwa kina.

“Hatuwezi kuongea haya mambo kwenye simu ukitaka kupata taarifa kwa usahihi funga safari uje ofisini” amesema Mkuu wa Chuo hicho na kukata simu.

Hata alipotafutwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili hakupatikana kwa sababu simu yake ilikuwa haipatikanani.

 

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *