Lowassa aeleza tena alichozungumza na rais Magufuli

Jamii Africa

Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa atoboa siri ya kufanya mazungumzo na rais John Magufuli kwamba ilikuwa ni kumshawishi kurejea kwenye Chama Cha Mapinduzi.

Kauli ya Lowossa inakuja siku chache baada ya kukutana na rais Magufuli ambapo waliongea mambo mbalimbali ikiwemo utendaji wa serikali ya awamu ya tano katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo Lowassa alionekana kusifu juhudi za serikali kuboresha maisha ya watu.

Mazungumzo hayo yalizua mjadala katika jamii ikizingatiwa kuwa Lowassa alikuwa mwanachama mtiifu wa CCM lakini mwaka 2015 alihamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  na kupata nafasi ya kugombea urais ambapo alichuana vikali na rais Magufuli.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari, Lowassa amenukuliwa akisema alipewa mwaliko na rais wa kwenda ikulu na pamoja na mambo mengine alishawishiwa kurudi CCM lakini alikataa kwasababu uamuzi wa kukihama chama hicho haukuwa wa kubahatisha.

“Ujumbe wa Dokta Magufuli  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwangu ulikuwa ni kunishawishi kutaka nirejee CCM, suala ambalo sikukubaliana nalo na nilimueleza Rais kwamba uamuzi wangu wa kukihama chama hicho haukuwa wa kubahatisha”, imeeleza taarifa hiyo.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA amesema atendelea kubaki kati chama hicho na kuwataka wanachama wa chama hicho kudumisha umoja  ili kuwaletea watanzania mabadiliko ya kweli.

“Nawajulisha watanzania wapenda mabadiliko ya kweli kwamba niko imara na madhubuti kuliko wakati mwingine wowote ule, sijayumba wala sitayumbishwa. Ninaendelea na dhamira yangu ya kuamini katika CHADEMA na kusimamia mabadiliko kupitia UKAWA”, imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *