Maambukizi  ya Ukimwi yanavyoshamirisha yatima shule za msingi Iringa, Mbeya

Jamii Africa

Mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe imetajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi yatima wanaondikishwa katika shule za mingi, jambo linaloweza kuongeza gharama za matunzo kwa watoto hao.

Kulingana na uchambuzi wa takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) za mwaka 2016 zinaeleza kuwa mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na wanafunzi  29,062 yatima sawa na asilimia 14.4% ya wanafunzi wote wa shule za msingi kwa mwaka huo.

Iringa ilikuwa na wanafunzi  wa shule za msingi wapatao 202,113 lakini kati ya hao mwanafunzi 1 kati ya 10 alikuwa ni yatima.

Kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, mtoto anahesabika kuwa ni yatima endapo atafiwa na mzazi mmoja au wote wawili. Kimsingi anakosa matunzo au upendo wa mzazi mmoja au wote wawili ambapo inaweza kuwa ni changamoto kwa ukuaji wake hasa katika upatikanaji wa elimu.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa siyo Iringa pekee ndiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi yatima lakini mikoa yote inayounda kanda ya Nyanda za Juu Kusini iko kwenye nafasi ya juu kabisa miongoni mwa mikoa 5  ya Tanzania bara yenye yatima wengi.

Nafasi ya pili inashikwa na mkoa wa Njombe ambao ulikuwa na wanafunzi  yatima 19,794 sawa na asilimia 12.7, ikifuatiwa na Mbeya (41,956) sawa na 11.3%. Mkoa wa nne ni Pwani (26,545) sawa na 10.4% na nafasi ya tano ni Kagera (45431) sawa na asilimia 9.8.

Mikoa hiyo mitano inaunda jumla ya asilimia 44.2  ya wanafunzi wote  731,536 yatima waliokuwepo katika shule za msingi kwa mwaka wa 2016. Hiyo ni sawa na kusema kuwa watoto 4 wa mikoa hiyo mitano kati ya 10 ya Tanzania bara ni yatima.

Lakini iko mikoa ambayo imefanikiwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi  yatima ikiwemo Manyara ambayo ilikuwa na wanafunzi 15,854 sawa na 6.2% ikifuatiwa na Kigoma (6.5%),  Singida na Mtwara ambazo zote kwa pamoja zilikuwa na 6.7 %. Na mkoa wa tano toka chini ni Lindi (6.8%).

Nini kiini cha kuwepo utofauti mkubwa wa kimkoa wa uwepo wa wanafunzi yatima katika shule za msingi za serikali na binafsi nchini?

ASILIMIA ZA WANAFUNZI YATIMA KATIKA SHULE ZA MSINGI KIMKOA- 2016

 

Wadau waelezea dhana hiyo

Wadau wa afya na masuala ya elimu ya jamii wanaeleza kuwa kuna uhusiano mkubwa wa ugonjwa wa UKIMWI na uwepo wa wanafunzi wengi au wachache yatima katika maeneo mbalimbali nchini.

 Kulingana na takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) za mwaka 2017 zinaeleza kuwa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa ambayo ina wanafunzi wengi yatima ndiyo vinara wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini.

Kwa muktadha huo idadi ya wazazi wanaofariki kwa maradhi hayo nayo ni kubwa; uwezekano wa watoto wengi kubaki au kuondokewa na wazazi wote wawili ni mkubwa. VVU husambazwa zaidi kwa njia ya ngono (Uasherati na uzinzi), Matumizi ya pombe na dawa za kulevya, kutakasa wajane na baadhi ya mila na desturi. Ugonjwa huo hauna dawa wala kinga.

TACAIDS inaeleza kuwa  mkoa wa kwanza ni Njombe wenye  asilimia 14.8 ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu kwa asilimia 9. Lakini imebainika kuwa mikoa yenye wanafunzi yatima wachache katika shule ina viwango vidogo vya maambukizi ya UKIMWI. Mafano  Manyara (1.5%) na Lindi (2.9%).

Msemaji wa Tacaids, Glory Mziray, wakati akiongea na wanahabari alisema maeneo watanzania walioonesha kuwa na ufahamu sahihi wa elimu kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi wanafikia asilimia 60 jambo linalosababisha kuwepo mwamko mdogo wa kubadili tabia katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya maradhi hayo.

Alibainisha kuwa njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi ni tohara kwa wanaume. Njia hiyo napunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60 na kusisitiza kuwa ipo haja ya kutoa elimu zaidi juu ya uelewa wa ugonjwa huo ili watoto wapate matunzo ya wazazi wote wawili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Vijana ya YOPOCODE, Alfred Mwahalende amesema mila, ushirikina na kugombania mali ni sababu nyingine inayoongeza watoto yatima shuleni.

“Sababu zingine ni masuala ya kishirikina ambayo hayazungumzwi sana. Katika maeneo ambayo tumekutana na wanavijiji wanaseama baba alirogwa kutokana na mali ili ndugu zake warithi. Wengine wanatafuta utajiri kwa kutoa ndugu zao kafara.” Ameeleza Mwahalende.

Amebainisha kuwa elimu itolewe kwa jamii juu ya kuwatunza watoto yatima na jinsi ya kujikinga na maradhi yote yanayosababisha vifo kwa wazazi ambao wanawajibika kuwalea na kuwasomesha watoto.

“Ninachoweza kusema ni elimu  itolewe lakini pia Asasi zinazoshughulika na masuala ya watoto yatima zione njia ya kuweka sawa kuimarisha na kuwapokea watoto wengi kwenye vituo vyao.” Amesema Mwahalende.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *