Mafao ya mwalimu aliyefariki yakwamishwa hadi marehemu ajaze fomu

Jamii Africa

MJANE Specioza Kamala ameendelea kusotea mafao ya mume wake aliyefariki miaka 13 iliyopita, huku mwaka huu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikimwandikia marehemu barua ya kumtaka ajaze fomu ya kulipwa mapunjo ya mshahara baada ya kupanda daraja.

Marehemu Richard Mutakulemberwa aliyekuwa mwalimu katika shule ya sekondari Kahororo iliyopo Manispaa ya Bukoba, alikutwa na mauti August,19 mwaka 1998 wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na T.Kagumisa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambayo Fikra Pevu ina nakala yake, pamoja na mambo mengine inamtaka marehemu kujaza fomu kutokana na utaratibu mpya wa malipo ya malimbikizo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa

Pia barua hiyo ya Januari 4, 2012 iliyotumwa kupitia shule aliyokuwa akifundisha marehemu ya Kahororo inamtaka kufuata maelekezo kwa mujibu wa barua hiyo ili madai yake yaweze kushughulikiwa.

“Tafadhali mara upatapo barua hii jaza na utume kwa Katibu Mkuu fomu halisi na nakala moja (photocopy), pia ambatanisha barua yenye maelezo sahihi ya madai,nakala ya barua ya kupandishwa na kukubali cheo na ‘salary slip’ ya karibuni,” inaeleza sehemu ya barua hiyo kwenda kwa marehemu.

Pia mbali na barua hiyo kumtakia marehemu ushirikiano mwema katika kukamilisha zoezi hilo, inamkumbusha kuwa nyaraka zote lazima zipite kwa mkuu wake wa kituo na kutumwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Naye mjane wa Marehemu, Specioza Kamala mbali na kusikitishwa na hali hiyo, alisema tangu kufariki kwa mume wake mwaka 1998 ameendelea kufuatilia madai ya mume wake bila mafanikio na hata kufika Wizarani huku akipewa kauli za ahadi.

Alisema kuwa mbali na kuwa alishapata barua hiyo aliyoandikiwa marehemu mume wake, anachokumbuka ni kuwa mme wake alifariki kabla hajalipwa mapunjo ya mshahara baada ya kupandishwa daraja ambayo ameendelea kuyafuatilia bila mafanikio na kuwa mirathi ya marehemu ilishatolewa.

“Alipanda daraja mwaka 1996 na kufariki kabla ya kulipwa mapunjo yake ya mshahara,suala hili nilishawaeleza hata watu wa Utumishi wa Umma kutoka Dar es salaam na kunielekeza niende Wizarani na baada ya kwenda walisema faili lake halipo,” alisema mama huyo ambaye pia ni mwalimu katika moja ya shule za msingi Mkoani Kagera.

Alipoulizwa kama suala hilo liliwahi kufika katika Ofisi za Chama cha Walimu Mkoani hapa, Katibu wake wa Mkoa Aaron Masalu alisema halijafika katika ofisi hiyo huku akilihusisha na mfumo mbovu wa utunzaji wa takwimu za watumishi.

Pia alidai vyombo vinavyomshughulikia mwalimu havina utaratibu mzuri wa mawasiliano na kusema kuwa sasa wakati umefika wa mwalimu kushughulikiwa na chombo kimoja tofauti na ilivyo sasa.

Alisema mbali na kuwa utaratibu uliopo unaweza kuchelewesha malipo ya mhusika au kuyakosa kabisa alidai suluhisho ni kuwa namwajiri mmoja ambapo hivi sasa walimu wanashughulikiwa na Tamisemi,Utumishi wa Umma na Wizara yenyewe.

Imeandikwa na Phinias Bashaya-Kagera

4 Comments
  • Hawa watu niwaajabu sana! Yani mwl Muta tangu afariki tuko f2 leo watu wanafanya phd bado familia haijapata mafao yake? Wanategemea watoto wake walisomaje! Kaazi kwelikweli.

  • Inaonyesha wizara imetumia busara za Bulicheka, siku moja aliombwa mchuzi wa kubanika ili aoe nae akasema hakuna shida ila apatiwe mkaa wa migomba kwa shughuli nzima!! Na hapo vivyohivyo huyo mke kuna walakini huenda marehemu si mume wake! nawasilisha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *