Magufuli: Eneo lolote tutakalogundua lina madini tutazungusha ukuta

Jamii Africa

Rais John Magufuli ameagiza watendaji wa Serikali kujenga kuta kuzunguka maeneo yote yenye rasilimali muhimu ikiwemo madini ili kudhibiti upotevu wa mapato na kuwanufaisha watanzania.

Akizungumza leo katika hafla ya uzinduzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, amesema kwa miaka mingi nchi imekuwa ikiibiwa kutokana na kutokuwepo kwa mfumo thabiti wa kusimamia sekta ya madini.

Ameeleza kuwa mikakati ya Serikali yake ni kuona maeneo yote yaliyo na rasilimali muhimu kama madini yanalindwa na kuhifadhiwa kwa kuzungushiwa kuta ili kuwadhibiti baadhi ya watu ambao wanatumia rasilimali za nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa na taasisi za Serikali.

“Tumegundua eneo jingine na lenyewe lina Tanzanite. Nawahakikishia kuwa eneo lolote tutakalogundua lina madini au rasilimali tutazungusha ukuta. Hata kama ni mlima Kilimanjaro mkiona kuna umuhimu, zungushia,” amesema.

Ameongeza kuwa kabla ya kujengwa kwa ukuta huo, Serikali ilipata upinzani kutoka kwa baadhi ya watu ambao walisema jambo hilo haliwezekani kufanikiwa kwasababu ya mazingira ya eneo lenyewe la Mirerani ambalo shughuli za uchimbaji wa madini zinaratibiwa na wachimbaji wadogo wadogo.

“Wapo wengine walisema huu ukuta hautawezekana kujengwa, Jeshi la Wananchi limewaambia kinachowezekana Ulaya na Tanzania kinawezekana”, amesema Rais na kuongeza kuwa nchi itafaidika na mapato yatakayopatikana kwenye mgodi huo.  “Faida za ukuta huu ni nyingi, kuimarisha usalama lakini value for money (thamani ya fedha) itaonekana miongoni mwa wananchi”.

Hata hivyo, Rais amemuagiza Mkuu wa Majeshi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo kuandaa mpango mzuri utakaosimamia ulinzi wa ukuta huo ambao una urefu wa kilomita 24.5 na umeligharimu Taifa bilioni 5.

Ujenzi wa ukuta katika mgodi wa Mirerani ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Septemba, 2017  wakati akizindua barabara ya Kia-Mirerani. Katika uchimbaji wa madini ya Tanzanite Serikali ilikuwa inapata faida ya asilimia 5 tu na nyingine iliyobaki ilienda mikononi mwa wawekezaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi amesema wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mgodi huo unalindwa na taratibu za kuingia katika eneo hilo zinafuatwa. Pia emesema Jeshi la Taifa liko imara na litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi.

Naye Waziri wa Madini, Angelah Kairuki amesema wizara yake imeandaa kanuni zitakazotoa mwongozo wa namna shughuli za ulinzi, uchimbaji na kijamii zitakavyoratibiwa ndani ya ukuta huo.

“Wizara ya madini kwa sasa inaandaa kanuni za Mirerani za mwaka 2018 ambazo tunakusudia kuzihainisha wiki ijayo na kipekee kanuni hizo zitatoa mwongozo wa namna shughuli za ulinzi, uchimbaji, biashara ya madini na shughuli za kijamii zitakazoendeshwa ndani ya ukuta huu uliojengwa kuzungukwa mgodi wa Tanzanite”, amesema Waziri Kairuki.

Ameongeza kuwa utaratibu wa kuingia katika mgodi huo utakuwa ni kwa watu ambao wana vitambulisho vya taifa na mchakato wa kutoa vitambulisho hivyo umeanza kwa watu 6,500 ambao wameandikisha taarifa zao za awali.

“Vilevile tumechukua hatua nyingine za udhibiti ikiwemo kutolewa vitambulisho maalumu vya kuingia katika eneo la mgodi ambapo hadi sasa jumla ya watu 6,500 wameshaweza kusajiliwa na zoezi linaendelea kwa wale ambao bado hawajapata vitambulisho hivyo”, amesema Waziri Kairuki.

 

Mgunduzi wa Tanzanite akumbukwa

Serikali kupitia Rais John Magufuli imempa Milioni 100 Mzee Jumanne Ngoma aliyegundua madini ya Tanzanite ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa maendendeleo ya Taifa.

“Watu hawa hawatambuliwi, tazama mzee huyu ndiye aliyegundua madini haya leo tusingekuwepo hapa kama isingekuwepo huyu mzee, tazama sasa amepooza mguu wake”, amesema Rais na kuongeza kuwa tangu madini ya Tanzanite yagunduliwe na mzee Ngoma mwaka 1967, licha ya kutambuliwa na Serikali kwa barua ya Mwalimu Julius Nyerere, mzee huyo hajafaidika na chochote na Serikali imeamua kumpa milioni 100 ya matibabu na kujikimu.

Mzee Ngoma ambaye alikuwepo katika hafla ya uzinduzi wa ukuta wa Mirerani amesema anamshukuru Rais kwa kumtambua na kumpa heshima ya kipekee kwa ugunduzi wake wa madini ya Tanzanite.

“Ninashukuru sana Mheshimiwa Rais kwa heshima hii kwa kunitambua mimi kama mgunduzi wa madini, ni heshima kubwa kwangu na niseme kuwa wewe umechaguliwa na Mungu”, amesema Mzee Ngoma.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *