Dawa ya kuongeza nguvu za kiume yachochea wizi wa punda ukanda wa Afrika Mashariki   

Jamii Africa

Licha ya Tanzania kupiga marufuku uchinjaji wa nyama ya punda, inaelezwa kuwa biashara ya uuzaji wa punda inaendelea kwa njia zisizo halali kutokana na uhitaji mkubwa wa mnyama huyo katika soko la kimataifa la China.

Tanzania iliungana na nchi nyingine za Afrika kama vile Uganda, Botswana, Niger, Burkina Faso, Mali, na Senegal kupiga marufuku biashara ya kuuza punda kwasababu unatishia kutoweka kwa wanyama hao ambao watumiwa na wakazi wengi wa bara hilo katika shughuli za kiuchumi ikiwemo kusafirisha mizigo na kulima.

Punda hao husafirishwa hadi nchi ya jirani ya Kenya ambayo ina kiwanda cha kusindika ngozi ya punda kijulikanacho kama Goldox Kenya Limited ambacho husafirisha bidhaa hiyo mpaka China ili kukidhi mahitaji ya soko.

Kutokana na uchache wa wanyama hao, bei yake imeongeza mara dufu ambapo vijana hutumia fursa hiyo huingia katika vijiji na kuiba punda hao na kuwasafirisha hadi Kenya ili kujipatia fedha nyingi ambazo hutolewa na kampuni hiyo.

 Kulingana na ripoti ya Msajili wa Dawa za Asili China (2017) inaeleza kuwa mahitaji ya ngozi ya punda yameongezeka kuliko punda waliopo. Inakadiriwa kuwa ngozi milioni 1.8 zinauzwa kila mwaka, huku mahitaji ya dunia ni kati ya milioni 4 hadi milioni 10. Kwa mfano bei ya punda nchini Burkina Faso imeongezeka kutoka Euro 60 mwaka 2014 hadi Euro 108 mwaka 2016.

                         Kiwanda kusindika nyama na ngozi ya punda kcha Goldox Kenya Limited kilichopo nchini Kenya

 

Mahitaji ya punda yameongezeka marudufu katika soko la China ikizingatiwa kuwa nyama yake hutumiwa kama kitoweo na ngozi yake  hutumika kutengeneza dawa ya asili ijulikanao kama ‘ejiao’ ambayo hutibu magonjwa mbalimbali.

Dawa ya Ejiao ambayo hapo awali ilikuwa inatumika kuzuia kuvuja kwa damu lakini wakati huu matumizi yake yameongezeka ambapo hupunguza uzee, kuongeza nguvu za kiume, kuzuia ugumba, kuharibika kwa mimba na kusawazisha hedhi kwa wanawake.

Licha ya dawa hiyo kuwepo kwa miaka mingi, lakini imejipatia umaarufu mkubwa kuanzia mwaka 2010 baada ya kampuni ya Dong-E-E-Jiao ya nchini China inayotengeza ejiao kuendesha kampeni ya kuitangaza dawa hiyo ambayo imewavutia watu ambao wanakabiliwa na matatizo ya uzazi. Miaka 15 iliyopita ejiao ilikuwa inauzwa kwa Dola 9 lakini sasa imepanda hadi Dola 400.

China ambayo ilikuwa inaongoza kuwa na idadi kubwa ya punda duniani, idadi hiyo inapungua kila mwaka ambapo punda waliopo katika nchi hiyo ni milioni 6 kutoka milioni 11 na kwa makadirio ya chini inaweza kufikia milioni 3. Tofauti na wanyama wengine kama nguruwe na ng’ombe, punda hawazaliani sana ambapo jike huzaa mara moja kwa mwaka na wana hatari ya mimba kuharibika kutokana mazingira na kazi ngumu wanazofanya.

Kampuni za China zilianza kununua ngozi ya punda kutoka nchi za Afrika baada ya nchi zilizoendelea kuzuia biashara hiyo kwenye nchi zao. Inaelezwa kuwa kuna punda milioni 44 duniani kote, lakini kila mwaka punda milioni 1.8 huchinjwa kwa ajili ya kutengeneza ejiao, hii ni kulingana na ripoti ya taasisi ya Donkey Sanctuary iliyopo Uingereza.

Mwaka 2017, watafiti wa Chuo Kikuu cha Misitu cha China walionya kuwa mahitaji ya ejiao yanaweza kusababisha punda kutoweka kabisa kama alivyo mnyama pangolin.

“China imeamua kuagiza punda kwa gharama kubwa kutoka maeneo mbali duniani, jambo linaloweza kuitumbukiza dunia kwenye mgogoro mkubwa wa punda”, imeeleza  ripoti iliyowekwa kwenye jarida la Equine Veterinary.

Ngozi ya punda inafika China kupitia nchi mbalimbali ikiwemo Kyrgyzstan, Brazil na Mexico. Lakini Afrika ndio kitovu cha biashara hiyo ikiongoza kwa punda wanaochinjwa na madhara yanayopatikana.

Biashara hiyo imeathiri shughuli za kiuchumi hasa katika mikoa ya kaskazini ya Arusha na Manyara ambayo iko karibu na Kenya.  Inaelezwa kuwa mwaka jana punda zaidi ya 475 waliibwa ili kusafirisha nchi jirani lakini waliookolewa ni 175 pekee. Hali hiyo imewalazimu wakazi kutembea umbali mrefu kufuata maji na kutumia jembe la mkono kulima kutokana na kuadimika kwa punda katika maeneo yao.

                                          Ngozi ya punda ikiwa imeanikwa tayari kwa ajili ya kusindikwa

 

Hatua zilizochukuliwa

Nchi 14 za Afrika zikiungana na Pakistan zimezuia biashara ya kimataifa ya punda, ambapo Tanzania iliungana na nchi hizo mwezi June mwaka jana kutokana na tishio la kutoweka kwa wanyama hao.

Hata hivyo,  serikali iliamua kuruhusu usindikaji wa bidhaa za punda nchini ili kuepusha usafirishaji wa punda kuelekea Kenya ambako kuna kiwanda kikubwa cha usindikaji. Kiwanda hicho ambachi kinamilikiwa na wawekezaji toka china kiko mkoa wa Dodoma na inakadiriwa kuwa punda 200 huchinjwa kila siku na kusindikwa kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Akizungumza bungeni katika kikao cha tisa, Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa wakati huo, Dr. Titas Kamani alisema serikali iliruhusu ujenzi wa kiwanda cha kusindika punda ili kuongeza kipato na kudhibiti biashara haramu ya punda inayofanywa na baadhi ya watu kinyume na sheria.

“Hapa kati kati kulikuwa na wimbi kubwa la wanyama kazi hawa kusafirishwa kwenda Kenya huko kuna viwanda hivi, sasa tuliona tuwachinje na kuwasindika wenyewe kisha tuuze nyama tupate fedha”, alisema Dr. Kamani.

Maamuzi hayo ya Tanzania hayajaathiri biashara ya ngozi ya punda kwasababu hakuna dalili za biashara hiyo kupungua nchini Kenya. Mwaka 2016 bei ya ngozi ilikuwa mara hamsini zaidi kuliko mwaka 2014, huku bei ya punda wazima imeongeza mara tatu zaidi kutoka Dola 60 hadi Dola 165. Nyama na ngozi ya punda kutoka Kenya huingia China kupitia Vietnam na Hong Kong.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *