Makachero wa TAKUKURU wawabana watuhumiwa ufisadi Misungwi

Jamii Africa

HATIMAYE Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (PCCB), Mkoani Mwanza, imeanza kuwahoji vigogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani hapa, wanaotuhumiwa kwa ufisadi wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo wilayani humo.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hosea

Imeelezwa kwamba, makachero wa Takukuru wameanza kuwahoji rasmi vigogo hao kuanzia Jumatano wiki hii, ikiwa ni moja ya kutekeleza maagizo ya Serikali yanayotaka watuhumiwa wa ufisadi kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Taarifa za ndani zisizo na shaka zilizotufikia jana na leo, zinadai kwamba tayari vigogo wanne wameshahojiwa kuhusiana na tuhuma hizo mbaya za ubadhilifu wa fedha za miradi mbali mbali ya maendeleo wilayani Misungwi, na kwamba jana mmoja wa kigogo aliitwa kuhojiwa na Takukuru juu ya shutuma hizo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, waliohojiwa ni miongoni mwa watumishi waliotajwa katika ripoti mbali mbali za wakaguzi, ikiwemo ya TAMISEMI na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambazo zimebainisha kuwepo kwa ubadhilifu huo wa mali za umma katika halmashauri ya wilaya hiyo ya Misungwi, na wahusika kutajwa moja kwa moja kwa majina yao.

“Tayari Takukuru imeanza kuwahoji baadhi ya vigogo wa Halmashauri ya Misungwi. Watumishi hao ni wale wanaotuhumiwa kula fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

“Kazi ya kuwahoji vigogo hao ilianza Jumatano ya Januari 29 mwaka huu. Vigogo hao wanaitwa mmoja mmoja bila wao kujijua!. Walikuwa wakiwabeza waandishi wa habari waliokuwa wakiandika habari hizo za kuwepo kwa ufisadi…lakini kwa sasa vigogo hao wapo matumbo joto”, kilisema chanzo chetu cha habari cha FikraPevu (jina tunalihifadhi).

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, miongoni mwa watumishi walioanza kuhojiwa ni wale wanaotoka kwenye idara ya Fedha, Afya na Manunuzi (Ugavi), na kwamba mara baada ya taratibu zote kukamilika vigogo hao watapandishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili dhidi yao.

Hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari pamoja na Fikra Pevu viliripoti kuwepo kwa tuhuma hizo nzito za ubadhirifu wa fedha za miradi mbali mbali ya maendeleo wilayani humo, ambapo baadaye uongozi wa halmashauri hiyo uliwaita baadhi ya waandishi wa habari, kwa ajili ya kwenda kutembelea miradi na ‘kukanusha’ habari za awali.

Hata hivyo, tuhuma hizo za ufisadi katika halmashauri hiyo, ziliibuliwa upya Januari 25 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo, baada ya kiongozi huyo kufanya ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo, ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na watumishi wa halmashauri hiyo kisha kueleza kuzungumzia tuhuma hizo nzito.

Katika kikao hicho, RC Ndikilo ambaye alikuwa akitumia ripoti mbali mbali za wakaguzi kwa kutaja baadhi ya majina ya watumishi waliotajwa kwenye ripoti hizo kwa ufisadi, alitumia muda wa dakika 57 kukemea hali hiyo, na alisema atamshauri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aivunje halmashauri hiyo, ili ianze upya.

Vyanzo vya habari vinadai kwamba, Takukuru imejipanga vema kuhakikisha vigogo wote wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha za maendeleo wilayani Misungwi watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria, ili kujibu mashtaka.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Christopher Mariba alipoulizwa jana kuhusiana na taarifa za vigogo hao wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi kuanza kuhojiwa na taasisi yake hiyo nyeti, hakukanusha bali alisema wao wanafanya kazi bila kumuonea mtu yeyote, hivyo aliomba waachwe watekeleze majukumu yao ya kila siku.

“Sisi Takukuru tunafanya kazi zetu bila kumuonea mtu. Kwa maana hiyo kila siku tunafanyakazi zetu na hata muda huu tunaendelea kutekeleza majukumu yetu. Viacheni vyombo vya dola vifanye kazi yake”, alisema Kamanda huyo wa Takukuru Mkoani Mwanza, Mariba.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma, FikraPevu – Mwanza

3 Comments
  • Mimi nadhani hakuna kitakachofuata maana kulindana ndo asili yetu
    Hapakuwa na haja ya kusema kama wanawafuatilia maana kinachotakiwa ni watuhumiwa kuwajibishwa na si kujitangaza wanawafuatilia kwani mangapi wamesema na mpaka sasa hakuna majibu yoyote yaliyoonekana
    Mfano chaguzi ndogo na hata uchaguzi mkuu mbona watoa rushwa wanaendelea kudunda mtaani
    Ushauri TAKUKURU ingevunjwa maana haisaidii chochote haiwezi kushika waliowateua/waliowaajiri na tumechoka kusikia imeshika mahakimu wa mahakama za mwanzo/wilaya wakati mikataba ya nchi inaangamiza taifa na inaonekana wazi kuwa inaingiwa kwa ushawishi wa fedha lakini tasisi hii huko hawaoni
    Mikataba hovyo kabisa ya barabara inaingiwa pia hawaoni maanispaa/halmashauri zinatengeneza majengo na wakandarasi feki pia hawoni
    Je wakioneshwa na CAG wataona? na je wakiona je CAG akiondoka wanauwezo wa kuendelea kuona hicho walichooneshwa? Mi naona ni usanii na matambo ya viongozi tulio nao wa nchi hii hata ikiwa wajibu wao watataka wasifiwe tu! Kama ndo hivyo waliajiriwa kufanya nini?

  • Nchini kwangu nadhani hakuna kitakachofuata maana kulindana ndo asili yetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *