Mawaziri wa Magufuli wafunguka ripoti ya CAG

Jamii Africa

Hatimaye mawaziri wa wizara zilitajwa kwenye ripoti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) waanza kujitetea juu ya matumizi mabaya ya fedha yaliyotokea kwenye taasisi wanazosimamia.

Wakiongozwa na Waziri Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe wameitisha mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma ili kuyatolea ufanuzi baadhi ya mambo ikiwa ni hatua ya kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti ya CAG.

Mawaziri hao ni wa wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleman Jafo; Waziri wa Sera na Utaratibu wa Bunge, Jenista Mhagama; Waziri wa Ardhi, William Lukuvi.

Wengine ni Waziri wa Mifugo, Luhaga Mpina na Maji na Umwagiliaji, Isaaka Kamwele. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako; Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Mwanjelwa na  Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira, Kangi Lugola.

Katika utetezi wao mbele ya wanahabari, mawaziri wawili wamekubaliana na ripoti ya CAG na kuahidi kurekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza na kutengeneza mfumo imara wa serikali utakaozuia upotevu wa mapato.

Wa kwanza kujitetea alikuwa Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jafo ambapo alisema wizara yake imepokea ripoti ya CAG na wameanza kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa hasa kwa kuchukua hatua za kisheria kwa baadhi ya watumishi waliohusika na matumizi mabaya ya fedha za umma.

             Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akiongea na wanahabari

Amesema watumishi 434 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu ambapo 9 wamefukuzwa kazi, 210 walipewa onyo, 13 wametakiwa kulipa fidia kwa fedha zilizopotea.

“Wengine walishushwa vyeo, kupewa barua za onyo na wengine kufikishwa mahakamani , baadhi kama 13 hivi wanatakiwa kulipa fidia kwa fedha zilizopotea”, alisema Waziri Jafo.

Ameongeza kuwa wamewaagiza wakuu wa mikoa yote kuhudhuria vikao vyakujadili ripoti ya CAG kwenye halmashauri  zao na kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa watu waliohusika na matumizi mabaya ya fedha.

Akielezea juu ya  pesa za maendeleo kutofika kwenye halmashauri licha ya kuwepo kwenye vitabu vya bajeti, Waziri Jafo alisema  serikali itajitahidi kuimarisha mfumo wa kuzifikisha fedha hizo ili zitimize malengo yaliyokusudiwa ya miradi ya maendeleo.

Amebainisha kuwa katika mwaka 2015/16 fedha za maendeleo zilizopelekwa kwenye halmashauri ni asilimia 39 lakini ziliongezeka katika mwaka uliofuata wa 2016/2017 hadi asilimia 59.

Akitolewa ufafanuzi wa hoja ya CAG kuhusu fedha ya zaidi ya bilioni 3.53 zilizokusanywa na wakala wa serikali kutowasilishwa kwenye halmashauri alisema hali hiyo ilitokea kwasababu ya matumizi ya vitabu vya risiti ambavyo wakati mwingine vinapotea.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo amesema, wameimarisha mfumo ukusanyi mapato wa kielektroniki na wameandaa utaratibu mzuri wa kuwapata wazabuni wenye uwezo wa kukusanya mapato.

“Hoja hizi zilikuwa hazifanyiwi kazi ipasavyo lakini katika mwaka 2015/2016 Waziri Mkuu aliitisha kikao maalum na watendaji wa serikali ili kujadili mikakati ya utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ambapo wakuu wa mikoa wanatakiwa kushiriki vikao vyote vya Halmashauri vinavyojadili ripoti ya CAG na kuchukua hatua stahiki kwa watendaji wabadhirifu”, alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameendelea kusisitiza kuwa Tanzania iko katika nafsi nzuri ya kuendelea kukopa kwasababu deni la taifa ni himilivu na halijavuka kiwango cha kimataifa cha asilimia 56.

Katika hoja aliyotoa CAG kwenye ripoti alisema serikali inapaswa kuwa makini kuhusu ongezeko la deni la taifa ambalo linatishia kukosekana kwa huduma za afya ikiwemo wagonjwa wanaotibiwa  nje ya nchi.

Akifafanua zaidi, Waziri Mpango alisema, “Nizungumzie deni la taifa, tulifanya tathmini ya uhimilivu wa deni la taifa na tunaangalia vigezo mbalimbali. Kwa kuangalia vigezo hivyo vya kimataifa, taifa linaweza kuendelea kukopa”.

Alisema thamani ya deni la taifa na uhimilivu wake ni asilimia 34.4 ambapo ukomo wake ni asilimia 56. Pia umezungumzia mkanganyiko wa kiwango halisi cha deni la taifa ambacho kimekuwa kikitofautiana kulingana na mabadiliko ya ubadilishaji fedha.

Ameongeza kuwa deni halisi la taifa hadi kufikia Novemba 2017 lilikuwa trilioni 47 na taarifa iliyolewa na Waziri Mkuu kuwa deni limefikia trilioni 56 ni kwasababu deni hilo lilijumuishwa na deni la serikali na lile la nje.

 

Mapato na utekelezaji wa bajeti

Waziri mipango alisema kwa wastani serikali inakusanya trilioni 1.3 kwa mwezi ambapo  fedha hizo zinagawanywa kwenye mafungu mbalimbali. “Makusanyo yameongezeka hivi sasa kwa wastani TRA inakusanya trilioni 1.3 kwa mwezi lakini jambo la muhimu ni kuangalia kinachotoka kinaenda kufanya nini”.

Amebainisha kuwa fedha hizo huelekezwa kulipa mishahara ya watumishi wa umma (bilioni 550), kulipa deni la taifa ambapo huwa kati ya bilioni 600 hadi 900 kutegemea na kuiva kwa deni husika. Kiasi kinachobaki hutumika kulipa marupurupu, posho, huduma kwa askari, viongozi na zinazobaki hupelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

“Hizo jingine zinapelekwa wapi? Cha msingi tunazitumia vizuri, tunazipeleka kwenye miradi ya maendeleo, kuhudumia wananchi kutoa elimu bure, huduma za afya”, aalisema Dkt. Mpango.

Hata hivyo, leo walizungumza mawaziri wachache na kwa mujibu wa  Waziri Mwakyembe, mawaziri waliobaki wataendelea kutoa majibu wakati mwingine.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *