Meli yazama Ziwa Victoria,yaua mmoja, 15 waokolewa

Jamii Africa

MELI ndogo ya mizigo ya Pasific, imezama katika Ziwa Victoria, ambapo mtu mmoja ameripotiwa kufariki dunia, huku wengine 15 wakiokolewa na wavuvi ndani ya Ziwa hilo; FikraPevu imethibitishiwa.

Meli hiyo inayodaiwa kumilikiwa na mtoto wa mmiliki wa kampuni ya Meli za Nyehunge Jijini Mwanza, imezama leo Alhamisi Februari 23, 2010, saa 3 asubuhi, ikiwa inatoka katika Kisiwa cha Ghana Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, na kwamba ilizama eneo la Bwiro wilayani Ukerewe.

Taarifa zilizoifikia FikraPevu dakika chache zilizopita, zinaeleza kwamba, meli hiyo ilikuwa imesheheni mizigo ya dagaa, pamoja na makreti ya soda na bia, na kwamba chanzo cha kuzama ni dhoruba kali iliyokumbana nayo katikati ya Ziwa Victoria, ambapo ilishindwa kumudu mawimbi hayo makubwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ambazo pia zimethibitishwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (Sumatra), Kanda ya Ziwa, zimeeleza kwamba, meli hiyo ya Pasific ilizidiwa mawimbi makali ndani ya Ziwa hilo, hivyo kuzama maji kabisa.

“Meli ndogo ya mizigo ya mtoto wa Nyehunge imezama kwenye Ziwa Victoria leo. Meli hii ilikuwa na wafanyakazi 16, lakini mmoja amefariki baada ya kuchoka na kuachia maboya.

“Meli hii ni ile ya Pasific. Imezama leo saa 3 asubuhi eneo la Bwiro ikiwa inatokea Kisiwa cha Ghana Ukerewe. Ila mtu mmoja amefariki anaitwa Maulidi. Na aliingia kazini siku ya jana kama kibarua kushika nafasi ya mfanyakazi mmoja ambaye alikuwa na udhuru”, alisema John Nyanguge ambaye ni mtu wa karibu na mmiliki wa meli hiyo iliyozama maji.

Hili ni tukio la pili ambapo Jumapili wiki iliyopita, boti moja ya abiria ilizama katika Ziwa Victoria, wakati ikitoka Maisome kwenda Kahunda Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, ambapo watu 35 walihofiwa kufa maji, ingawa baadaye Jeshi la polisi lilidai hakuna mtu hata mmoja aliyefariki dunia baada ya abiria wote hao kuokolewa.

Mbali na hayo, hivi karibuni watu kadhaa walinusurika kufa maji baada ya boti mbili walizokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso ndani ya Ziwa Victoria katika eneo la Musoma Vijijini Mkoani Mara.

Akithibitisha kuzama kwa meli hiyo ya Pasific mchana huu wa leo, Ofisa Mkaguzi wa Sumatra Kanda ya Ziwa, Alfred Wariana alisema, ni kweli meli hiyo imezama ndani ya Ziwa hilo ikiwa na shehena ya mizigo.

“Ni kweli meli hiyo imezama kabisa leo asubuhi. Kwa sasa tupo kwenye hekaheka za kufuatilia tukio hili, maana nimeambiwa ilikuwa na watu ndani na kati yao mmoja amefariki dunia.

“Chanzo cha ajali hii tulielezwa kwamba kulikuwa na mawimbi makali sana ndani ya Ziwa. Na wakati ikiendelea kukata mawimbi hayo, ilizidiwa na hatimaye kuzama kabisa. Ila tunafuatilia kumjua miliki wake na watu hasa waliokuwemo na waliookolewa”, alisema Ofisa huyo wa Sumatra Kanda ya Ziwa, Wariana.

Awali duru za habari zilieleza kwamba, baada ya meli hiyo kuzama, watu waliokuwemo walijitupa na kuanza kuogelea majini kwa kutumia maboya, na walienda kuokolewa na wavuvi eneo la Kunene wilayani Ukerewe, na kwamba mtu anayedaiwa kuwa ni kibarua (Maulidi), alichoka kushikilia boya ambapo inadaiwa aliachia kisha kuzama majini na kufariki dunia.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), alipopigiwa simu yake ya kiganjani mchana huu wa leo kwa lengo la kutaka kutoa ufafanuzi juu ya ajali hiyo, alipokea simu kisha akampa mmoja wa maofisa wa jeshi hilo kuongea na mwandishi wa habari hizi, ambapo ofisa huyo alithibitisha kuzama kwa meli hiyo ya Pasific.

“Unaulizia hiyo meli iliyokuwa na watu 16?. Ni kweli meli hiyo imezama ndani ya Ziwa Victoria…lakini mimi siwezi kukueleza zaidi labda msubiri Kamanda mwenyewe akitoka kikaoni atakupa maelezo kamili”, alisema ofisa huyo wa jeshi la polisi mkoani Mwanza.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *