MGOGORO WA MAJI: Jiji la Dar es Salaam kufuata nyayo za Cape Town

Jamii Africa

Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini litazima mitambo inayopeleka maji kwa watumiaji ifikapo Aprili 29, 2018 na kuweka historia ya jiji hilo kukosa huduma hiyo muhimu, ambapo kuzimwa kwa mitambo hiyo ni baada ya maeneo mengi ya nchi hiyo kukabiliwa na ukame kwa miaka mitatu mfululizo.

Inaelezwa kuwa jiji hilo likifunga mitambo hiyo litakuwa jiji la kwanza duniani kukosa huduma ya maji. Meya wa jiji hilo Patricia De Lille amewashauri wakazi wa jiji hilo ambao wanafikia milioni 4 kupunguza matumizi ya maji ili kuendana na hali hiyo ya kupungua kwa maji.  

Kama wanavyoiita siku hiyo ya kukosa maji ‘Day Zero’,  ni kweli kwasababu wanaangalia takwimu kila wiki juu ya akiba ya maji iliyopo na matumizi ya kila siku. Januari 8 mwaka huu, Meya De Lille alikumbusha kuwa siku hiyo ya kukosa maji kabisa itakuwa Aprili 29 kulingana matumizi ya kila siku ya jiji hilo.

Kimsingi jiji hilo halitakosa maji kabisa kwenye maeneo ya kuhifadhia, kwasababu matope na uchafu mwingine kwenye mabwawa huchukua asilimia 10 ya maji yote yasiyotumika. Mamlaka za maji za jiji zinachukua tahadhari na  ikiwa mabwawa yatafika asilimia 13.5 ya uzalishaji maji, usambazaji maji kwa wakazi utazuiwa isipokuwa kwenye maeneo muhimu kama hospitali.

Baadhi ya wakazi wa Cape Town wakisubiri kupata maji mgao baada ya jiji hilo kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji

 

Nini kitatokea kama mabomba yatokosa maji?

Wakazi wa jiji hilo watalazimika kwenda kuchota maji kwenye vituo 200 vya maji ambavyo vimetengwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ambapo kila mtu atapata lita 25 (6.6 gallons) kwa siku. Vikosi vya usalama vitasimamia zoezi hilo ili kuhakikisha vurugu hazitokei na watu hawachoti maji kuzidi kiwango walichopangiwa.

Lakini baadhi ya wafanyabiashara wameanza mchakato wa kununua maji katika miji mingine na kuyahifadhi kwenye matanki ili kuuza kwa bei ya juu hasa kwa matajiri wa jiji hilo ambao wana uwezo wa kumudu bei hiyo.

 

Hatua wanazochukua wakazi wa jiji hilo

 Jiji hilo limepunguza matumizi ya maji katika ngazi ya kaya hadi kufikia lita 87 (23 gallons) kwa mtu mmoja kila siku. Nyumba nyingi zimepunguza matumzi ya maji kwa kiasi kikubwa ikiwemo maji ya kuoga, hakuna tena kumwagilia bustani, kuosha magari, kuosha vyombo na mashine za kufulia nguo. Vyoo vingi vya umma havitumiki tena na matanki ya kuhifadhia maji yamebaki matupu.

 Kulingana na takwimu za jiji hilo, ni asilimia 54 ya wakazi ndio wanapata maji kwa sasa kwa kiwango kilichowekwa na ndio maana ‘Day Zero’ imesogezwa mbele kwa wiki kadhaa. Jiji linachukua hatua kwa watu ambao wanakiuka utaratibu uliowekwa ili kuhakikisha watu wote wanapata maji kidogo kukidhi mahitaji ya msingi.

Mamlaka za mipango miji zimesema kwa muda sasa uzalishaji maji katika jiji la Cape Town umeshindwa kuendana na ongezeko la watu ambalo limeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Ukijumuisha na miaka 3 ya kushuhudiwa kwa kiwango kikubwa cha ukame nchini Afrika Kusini, kunalifanya tishio hilo la kupotea kwa maji kama tukio la Milenia, amesema Mtaalamu mmoja wa hali ya hewa nchini humo.

 Ili kukabiliana na janga hilo la ukosefu wa maji, jiji limeanza mchakato wa kufunga mitambo ya kushafisha maji ya bahari ya Hindi ili kuyaweka katika matumizi ya kawaida na kuchimba visima virefu ili kukabiliana na hali hiyo haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo, juhudi hizo zinaweza zisifanikiwe mpaka siku ya kufungwa kwa mitambo itakapofika au hata kabla ya kuanza kwa mvua za msimu mwezi Mei mwaka huu kama zitanyesha. Watafiti wa mabadiliko ya hali ya hewa wanatabiri kuwa vipindi vya ukame vitaendelea kwa miaka mingi ijayo na kushuhudiwa kwa vipindi vichache vya mvua. Kwa hali hiyo, wakazi wa Cape Town wanajiandaa kwa jambo ambalo siku zijazo litakuwa la kawaida.

Bwawa la Berg linalotumika kuzalisha maji katika jiji la Cape Town

 

  Jiji la Dar es Salaam liko salama?

Mamlaka za Maji jijini Dar es Salaam zina mengi ya kujifunza kwa hali inayoendelea Cape Town kwasababu mazingira hayatofautiani sana na hatua muhimu zichukuliwe ili kutatua tatizo la maji kabla halijakomaa na kuwa janga.

Taarifa ya Mkoa ya Dar es Salaam inaonyesha kuna kasi kubwa ya ongezeko la watu katika jiji hilo ukilinganisha na mikoa mingine. Mpaka sasa jiji hilo lina wakazi zaidi ya milioni 4 juu kidogo ya Cape Town.

Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli za uchumi nchini ikiwemo shughuli za viwanda na biashara. Lakini linakabiliwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambazo zinaweza kuathiri uzalishaji wa maji siku zijazo ikiwa hatua muhimu hazitachukuliwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa hadha ya maji.

FikraPevu inafahamu kwamba, idadi ya watu jijini Dar es Salaam inaongezeka kwa asilimia 6 kwa mwaka huku DAWASCO  (Kampuni ya kusambaza maji) ikiwa na wakati mgumu kuhudumia kikamilifu idadi ya watu wasiofika hata robo ambao wameunganishwa na mtandao wa maji ya bomba wa kampuni hiyo ya umma.

Licha ya jitihada kadhaa zinazofanyika, lakini Mamlaka ya Maji ya mkoani humo (DAWASA) imeendelea kuwa na uwekezaji usioendana na kasi kubwa ya ongezeko hilo la watu, ambapo wengi wao wanalazimika kutumia maji ya siyo salama.

 Uchunguzi wa FikraPevu umeonyesha kwamba, asilimia 70 ya maji ambayo wanatumia wakazi wa jijini Dar es Salaam yanatokana na visima kutokana na wakazi wengi kutounganishiwa na mifumo ya maji.

Kwa bahati mbaya zaidi ya asilimia 60 ya visima vilivyojengwa jijini humo maji yake si salama na mamlaka ya maji imeshindwa kabisa kutanua wigo wa kuwaunganishia maji wakazi wengi wa jiji hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkoa wa Dar es Salaam, kuna mahitaji kwa wastani wa zaidi lita milioni 400 huku asilimia 40 ya maeneo ya jijini hayakupitiwa na mtandao wa maji achilia mbali idadi ndogo sana ya wateja wanaotumia maji yanayosambazwa na DAWASCO.

Ongezeko la asilimia 6 la watu kwa mwaka linafanya ongezeko la mahitaji ya maji kuwa lita milioni 27. Baadhi ya miradi kama ule wa Kidunda mkoani Morogoro ambao ulitarajiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji maji jijini Dar es Salaam lakini kwa wadadisi wa mambo wanasema haitaondoa tatizo la maji isipokuwa njia mbadara zikitumika. 

 

Nini kifanyike

Mamlaka za Maji zinapaswa kujifunza kwa hali inayoendelea Cape Town ambayo imeingia kwenye janga kubwa la ukosefu wa maji. Serikali iongeze bajeti ya maji ili kuruhusu ujenzi wa miundombinu na kubuniwa kwa vyanzo vingine vya maji ikiwemo usafishaji wa maji ya bahari (desalination plants ) ili kuongezaa uzalishaji wa maji unaofanywa na mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ambayo inategemea mito na mvua.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *