Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar: Dk. Shein ahimiza uwazi, uwajibikaji serikalini

Jamii Africa
Zanzibar President Dr Shein addresses the rally yesterday during 52th years of Zanzibar Revolution Celebrations at Aman Stadium in Zanzibar yesterday . PHOTO|PMO

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuanzia Aprili mwaka huu serikali yake itaanza kuwalipa wafanyakazi wa umma kima cha chini cha mshahara cha shilingi 300,000 kutoka 150,000 za awali ikiwa ni mkakati wa kuboresha maisha ya wananchi wa visiwa vya Zanzibar.

Rais Dk. Shein ametoa ahadi hiyo wakati akihutubia wananchi katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Aman mjini Zanzibar ambapo amesema mkakati huo wa serikali utaanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo.

“Katika kipindi hiki mipango yote imekamilika ya kuwalipa wafanyakazi wa serikali kima cha chini cha mshahara kutoka 150,000 cha sasa hadi sh. 300,000. Kiwango hichi kimeongezeka kwa asilimia 100, mshahara utaanza kulipwa mwezi Aprili hivi karibuni”, amesema Dk. Shein.

Amesema nia ya serikali ni kuongeza hali kwa watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, kuongeza uzalishaji na utolewaji wa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi.

Amebainisha kuwa serikali yake haitasita kuwachukulia hatua baadhi ya wafanyakazi ambao wameshindwa kuwajibika kwenye nafasi zao licha ya serikali kuboresha utolewaji wa mishahara na posho mahali pa kazi ambapo amewataka kuheshimu sheria na miiko ya dhamana walizopewa.

“Serikali katika mwaka 2016 imelishughulikia suala la nidhamu kwa wafanyakazi kwa mujibu wa sheria namba 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011 ya kanuni za kazi”, amesema Dk. Shein na kuongeza kuwa,

“Wapo wafanyakazi wameondoshwa kwenye dhamana za uteuzi kwa kukiuka maadili ya kazi, vilevile wapo waliosimamishwa kazi kutokana na ubadhirifu wa mali ya umma na wanaendelea kuchunguzwa na kushughulikiwa na taasisi zinazohusika”.

Ameongeza kuwa serikali yake itahakikisha wananchi wote bila kujali nafasi zao wananufaika na rasilimali za nchi ikiwemo kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana na wanawake ambao hawako katika sekta rasmi ili kuwawezesha kiuchumi.

Wakati huo huo, Dk. Shein amezungumzia suala kupambana na ufisadi na kuwa ataendelea kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli za kupambana na vitendo vya rushwa huku akiwataka wananchi na viongozi wa serikali kutambua juhudi hizo ili kujenga muungano wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Pia katika hotuba yake hakuacha kuwasifu na kuwaenzi waasisi wa Tanzania akiwemo rais Julius Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume kwa kufanikisha uhuru wa Tanganyika na Zanzibar. Kudumisha na kuimarisha muungano ambao umeifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani na utulivu kwa wananchi wote.

        Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na viongozi wa majeshi ya Tanzania

 

 Mafanikio yaliyopatikana

Rais Dk. Shein hakuacha kutaja mafanikio yaliyopayika kwenye utawala wake ikiwa ni sehemu ya kuenzi mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Katika sekta ya nishati serikali imefanikiwa kupunguza tatizo la umeme katika kisiwa cha Pemba ambapo nyaya zenye urefu wa  mita 800 zimetandazwa chini ya bahari ya Hindi kutoka mkoa wa Tanga hadi kwenye kisiwa cha Pemba.

Amefanikiwa kuboresha sekta ya afya kwa kusomesha Madaktari Bingwa wazawa katika nchi za China na Cuba.  kujenga hospitali, vituo vya afya na kununua vifaa tiba na madawa. Hospitali zimeongezeka kutoka 5 hadi 12, vituo vya afya 36 hadi 158 kwa mwaka 2017, na serikali inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo majengo, dawa na vifaa tiba.

Mchakato wa kuimarisha usawa wa kijinsia  unaendelea ambapo kesi 176 zimefunguliwa dhidi watu ambao wamekutwa na makosa ya uvunjaji wa haki za binadamu huku kesi 90 zikiwa kwenye upelelezi. Pia serikali inatekeleza Mpango wa Taifa wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na watoto ulizinduliwa Julai mwaka 2017. 

Sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa kwa kuondoa elimu ya kibaguzi na kuunda mfumo wa elimu kwa wote. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 25,572 mwaka 1963 hadi 377,821 kwa 2017.  Ujenzi wa jengo la sayansi na teknolojia  umefikia asilimia 85% na kukamilika kwake kutachochea mageuzi ya viwanda visiwani humo.

Sekta ya utalii nayo imepata mafanikio makubwa kwa idadi ya watalii wanaotembelea kisiwa hicho kuongezeka hadi kufikia 433,116 mwaka 2017. Pia mauzo ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hiyo yameongezeka na kufikia bilioni 94.94 mwaka 2016 huku sekta ya viwanda ikichangia asilimia 16 ya pato la ndani ambapo mwaka 2017 imechangia milioni 489 kutoka milioni 417 mwaka 2015. Serikali ya Zanzibar inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujenga barabara ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

 

Hali ilivyokuwa uwanjani

Sherehe hizo za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilianza mapema leo asubuhi ambapo wananchi kutoka maeneo mbali ya Zanzibar walikusanyika katika uwanja wa Aman uliopo mjini Magharibu wakiongana na viongozi mbali wa serikali na wastaafu.  

Baaba ya wananchi kuingia uwanjani hapo vikosi vya majeshi ya Tanzania vilijipanga uwanjani huku viongozi wa kiingia kwa awamu kulingana na nyadhifa zao.

Ilipofika saa 2:38 rais wa Tanzania, John Magufuli aliingia uwanjani hapo huku akishangiliwa na umati wa watu waliojitokeza kwenye sherehe hizo ambapo alipewa heshima kutoka kwa vikosi vya majeshi ya Tanzania na wimbo wa taifa uliimbwa kuonyesha mshikamano uliopo baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Rais aliungana na viongozi wengine jukwaa kuu wakimsubiri rais wa Zanzibar.

Muda mfupi baadaye rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Mohamed Shein anaingia akiwa kwenye gari la wazi akiongozwa na pikipiki. Wananchi wanampungia mikono kuonyesha furaha waliyonayo juu miaka 54 ya Mapinduzi.    

Baada ya kuwasili uwanjani hapo, rais Shein akiwa kwenye gari la wazi akisindikizwa na piki zaidi ya tano. Alielekezwa kwenye jukwaa dogo lilokuwa uwanjani na kupigiwa mizinga 21 kutoka kikosi maalumu cha jeshi ikiwa ni heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu.

Kama hiyo haitoshi Dk. Shein amekagua vikosi mbalimbali vya majeshi vikiwemo vya anga, nchi kavu na majini vilivyokuwepo uwanji hapo. Rais alipanda kwenye jukwaa kuu na kusalimiana na viongozi mbalimbali waliofika katika sherehe hizo.

Kilichofuata ni maandamano ya wananchi kutoka mikoa ya Zanzibar kupita mbele ya mgeni rasmi huku wakionyesha mabango yenye jumbe mbalimbali kusifu  mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Moja ya bango lililobebwa na vijana kutoka Baraza la Vijana Zanzibar limesomeka “Hongera Dk. Shein kwa kuanzisha mabaraza ya vijana ambayo ni chachu ya maendeleo Zanzibar”.

Mshehereshaji alitoa fursa kwa  gwalide maalumu la vikosi vya ulinzi nchini likijumuisha Jeshi la Wananchi (JWTZ), Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Jeshi la Polisi kupita mbele ya rais Dk. Shein kutoa salamu za utii kwa Amiri Jeshi Mkuu.

Sherehe hizo pia zimeshuhudia Haraiki ya vijana chipukizi wakiwa wamevalia nguo zenye rangi ya bendera ya Zanzibar wakipita uwanjani hapo huku wakishangiliwa kwa umahiri na ukakamavu wao wa kutembea kwa mwendo wa haraka.Kumalizika kwa gwalide hilo maalumu kulitoa nafasi kwa Makamu wa Rais wa Zanzibar, Seif Idd kutoa salamu na kumkaribisha rais, Dk. Mohammed Shein kuhutubia taifa.

Baada ya kumaliza hutuba yake ambayo imeelezea mafanikio yaliyopatikana katika miaka 54 ya mapinduzi, rais Shein alishuka kutoka jukwaa kuu na kuondoka uwanjani hapo na kufuatiwa na viongozi wengine ikiwa ni ishara ya kuahirishwa

Kilele cha sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar zimefanyika leo katika uwanja wa Aman mjini Magharibi Zanzibar ambapo zilitanguliwa na shughuli mbalimbali zikiwemo Kombe la Mapinduzi, kuzinduliwa kwa miradi 33 ya maendeleo katika kisiwa hicho.

                              Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Julius Nyerere akiwa na rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Aman Abeid Karume

 

Sherehe hizo zilihudhuriwa na rais wa Tanzania, John Magufuli; Makamu wa rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na  viongozi mbalimbali wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania. Pia marais wastaafu; Jakaya Kikwete, Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Aman Abeid Karume walikuwepo katika sherehe hizo.

 

Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar

 Machafuko ya kisiasa yaliongezeka ndani ya Zanzibar na Pemba tangu kifo cha Sultani Khalifa  mwaka 1960. Sultani Khalifa alitawala Zanzibar kwa karibu ya miaka 50, tangu mwaka 1911 ambapo utawala wake uliwaumiza na kuwatumikisha wananchi kwa kazi ngumu bila kupata manufaa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Baada ya udanganyifu mkubwa wa majimbo ya uchaguzi na mseto katika chaguzi kuu mbili za mwaka 1961 vyama vikuu vilishindwa kujipatia wingi wa kura kwa kila kimoja na kuhitimisha utawala wa Waingereza. Waingereza ambao waliitawala Zanzibar kwa miaka 70 waliondosha majeshi yao kikiwemo kikosi maalumu cha Kiarishi ambacho kilikuwa kimewekwa karibu na uwanja wa gofu na mpaka wa mji Mkongwe mapema mwaka 1963.

Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar tarehe 12 Disemba 1963, aliadhimisha uondokaji wa Gavana wa kiingereza Zanzibar na mwisho wa ukoloni Zanzibar.  

Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ukiipa ushindi mdogo wa kura Muungano wa vyama viwili ZNP(Chama cha Kizalendo Zanzibar) na ZPPP (Chama cha Watu wa Pemba na Unguja). A.S.P (Chama cha Afro shirazi) kilitakiwa kiwepo katika Serikali iliyo na chini ya nusu ya wabunge kwa mtindo wa bunge la Kiingereza na Sultani, akiwa kama ni mtawala tu lakini sio mtawala mwenye maamuzi ya mwisho. Hakikupata fursa ya kuwepo katika serikali ya mseto kutokana na kutokubaliana na sera za ukandamizaji zilizokuwa zikifanywa na watawala wa Zanzibar.

Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatajwa kuanza Oktoba, 1963 ambapo Zanzibar ilipata uhuru wake wa bendera, kutoka kwa Waingereza lakini bado ikaendelea kukaliwa kimabavu na utawala wa sultani. Miezi michache baada ya Waingereza kuondoka, ndipo vuguvugu la mapinduzi lilipoanza, hatimaye Wazanzibar wakaingia mitaani na kupambana kwa saa 9, kabla ya kufanikiwa kuuangusha utawala wa sultani, Januari 12, 1964.

Mapinduzi hayo yaliongozwa na viongozi mbalimbali wa ASP chini ya Sheikh Aman Abeid Karume ambaye baadaye alikuja kuwa rais wa kwanza wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kufariki mwaka 1972 na maadui wa kisiasa.

Miezi mitatu baadaye, Aprili 26, 1964, Tanganyika na Zanzibar viliungana na kuunda Tanzania, muungano ambao umeendelea kudumu hadi leo na kuwa mfano wa kuigwa duniani kote.

Hata hivyo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuitambua Zanzibar kama nchi huru yenye mamlaka kamili inayoweza kutambulika katika jumuiya za kimataifa. Suala hili bado liko kwenye mjadala ili kuhakikisha muungano huo unazinufaisha pande zote mbili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *