Mikoa 10 Tanzania Bara vinara maambukizi ya Malaria

Jamii Africa

Aprili 25 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya Ugonjwa wa Malaria. Lengo hasa ni kutathmini hatua zilizopigwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa ambao unaua maelefu ya watu kila mwaka.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Niko tayari kutokomeza Malaria, Wewe Je?”

Kwa mujibu wa Shirika la Afya (WHO) Malaria bado inaua mtoto mmoja aliye chini ya umri wa miaka 5 kila baada ya dakika 2 ambapo ni sawa na kusema kila baada ya saa 1 mtoto mmoja hufariki kwa maradhi ya malaria.

Mwaka 2015, WHO ilibaini kesi za Malaria zipatazo milioni 214 na vifo 438,000 ambapo vifo 306,000 vilikuwa vya watoto chini ya umri wa miaka 5. Pia inakadiria kuwa asilimia 43 ya watu walio katika hatari ya kupata Malaria hawana neti na dawa za kuulia mbu katika nyumba zao.

Hadi kufikia mwaka 2015, nchi 91 duniani zilikuwa na maambukizi ya Malaria. Hata hivyo, kati ya mwaka 2010 na 2015 maambukizi ya Malaria yalipungua kwa 21%. Bara la Afrika lilikuwa linabeba 90% ya kesi zote za Malaria duniani na 92% ya vifo vyote vinavyotokana na Malaria.

Akizungumza mjini Geneva Uswis, Mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa wa Malaria, Pedro Alonso amesema kuwa mwaka 2016 ulipata visa milioni 216 vya malaria huku vifo 445,000 viliripotiwa kutokana na ugonjwa huo hatari. Hiyo ikiwa na maana kuwa kati ya 2015 na 2016 viliongezeka vifo 7,000.
Amesema dunia inapaswa kutumia rasilimali chache zilizopo kukabiliana na ugonjwa huo ili kuhakikisha binadamu wote wanakuwa salama dhidi ya tishio lolote la kiafya.

Hali ikoje Tanzania?
Serikali imetangaza kupiga hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria, ambapo kiwango cha maambukizi kimepungua kutoka asilimia 14 mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania (2017) uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliozinduliwa Aprili 25, 2018 mjini Kasulu Kigoma unaonyesha kiwango cha maambukizi ya Malaria nchini kimeshuka kwa zaidi ya nusu kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3.

Mafanikio haya yametokana na mipango na mikakati mizuri iliyowekwa na Serikali kuhakikisha malaria inadhibitiwa na hatimaye inatokomezwa kabisa.

Matokeo ya utafiti huo yanabainisha kuwa mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuwa na maambukizi ya kiwango cha 24.4% huku kiwango cha maambukizi ni kikubwa vijijini kwa 9.5% wakati mijini ni 2.2%.

Hata hivyo, bado kuna kazi kubwa ya kupambana na malaria kwasababu mikoa 10 kati ya 26 ya Tanzania Bara ina viwango vikubwa vya maambukizi ya ugonjwa huo. Mikoa hiyo ni Kigoma (24.4%), Geita (17.3%), Kagera (15.4%) Mtwara (14.8%), Ruvuma (11.8%), Lindi (11.7%), Tabora (11.7%), Mara (11.2%), Morogoro (9.5%) and Mwanza (8.9%).

 

Uelewa na mikakati ya serikali

Akizungumza katika maadhimishi ya Siku ya Malaria Duniani, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema, sio kila homa ni Malaria au homa ya tumbo (Typhoid). “Malaria inachangia chini ya asilimia 30 ya homa zote Tanzania na Typhoid hivyo hivyo. Tujenge tabia za kwenda hospitali kupima kabla ya kunywa dawa za Malaria. Tushirikiane kutokomeza Malaria”

Ameongeza kwa kusema kuwa, “Serikali imejikita kupunguza mazalia ya mbu; usambazaji wa vyandarua; matumizi ya viuadudu na dawa ukoko; kinga ya Malaria kwa wajawazito na matibabu sahihi ya Malaria. Tunasisitiza ushiriki wa jamii katika hatua hizi. Kwa pamoja tutatokomeza Malaria.”

Amezitaka halmashauri zote kutunga sheria ndogo za kumlazimisha kila mwananchi kuweka mazingira safi huku akitoa onyo kwa wananchi wanaotumia vibaya vyandarua ikiwemo kuvulia samaki, shughuli za kilimo cha bustani.

Malaria ni nini?
Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea parasiti vinavyoenezwa na mbu jike aina ya Anofelesi aliyeathiriwa. Wajawazito na watoto wako katika hatari zaidi ya kupata na ugonjwa huu.

Dalili za Malaria huanza kuonekana siku 10-15 baada ya kung’atwa na mbu mwenye maambukizi. Dalili za mwanzo ni pamoja na homa, kichwa kuuma na kuhisi baridi.

Kwa watoto wenye Malaria kali hupata dalili mojawapo ya hizi; upungufu mkubwa wa damu, kushindwa kupumua vizuri au Malaria kupanda kichwani. Ni vyema kupima kabla ya kuanza kutumia dawa kwa maana dalili hizi zinaweza kuonekana kwenye magonjwa mengine.

Kwa maeneo yenye maambukizi makubwa ya Malaria, WHO inapendekeza matumizi ya vidonge vya SP kwa watoto na wajawazito walio na ujauzito wa miezi mitatu na kuendelea.

Hata hivyo, WHO imetoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kurejesha vita dhidi ya malaria katika mstari unaotakiwa baada ya kwenda kombo, ili kufikia lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *