Milima ya Livingstone yaihamisha reli kutoka Mbamba Bay hadi Ameilia Bay

Jamii Africa

UWEPO wa milima mingi ya Livingstone katika wilaya za Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, umeilazimu Serikali kuihamisha Reli ya Kusini, inayotokea Bandari ya Mtwara, ambapo badala ya kuishia Mbamba Bay, sasa itaishia Ameilia Bay kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa.

Uchunguzi wa FikraPevu umeonyesha kwamba, eneo hilo la Ameilia Bay lipo kilometa chache kutoka Mbamba Bay, lakini itailazimu Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari kuipanua bandari ya Ameilia Bay ili kuwa na uwezo mkubwa wa meli kutia nanga pamoja na kupokea mizigo.

Kulingana na uchunguzi huo, baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu ambao tayari umekwishakamilika, ilionekana kwamba gharama za ujenzi hadi Mbamba Bay zingekuwa kubwa zaidi kuliko kwenda Ameilia Bay.

Meli ya MV Songea ikiwa imetia nanga Mbamba Bay.

FikraPevu ilimuuliza Meneja Uhusiano wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO), Catherine Moshi, ambaye alikiri mabadiliko hayo na kusema kwamba ni madogo na yenye tija zaidi.

“Washauri waelekezi, baada ya kupokea ripoti ya upembuzi yakinifu, walisema kujenga reli hadi Mbamba Bay kungegharimu fedha nyingi kwani ingelazimu kupasua milima, lakini wakasema, ikiwa reli hiyo itaizunguka milima hiyo hadi Ameilia Bay gharama yake itakuwa nafuu kidogo,” alisema bila kutaja gharama zilizoelezwa.

Hata hivyo, akaeleza kwamba, reli hiyo ya Mtwara-Mbamba Bay (Ameilia Bay) pamoja na tawi lake la kwenda Liganga-Mchuchuma itakayokuwa na urefu wa jumla ya kilometa 997, inasubiri tathmini ya fedha kabla ya kuanza kwa ujenzi wake.

Alisema kazi ya upembuzi yakinifu ilikwishafanywa kitambo, lakini serikali haiwezi kutangaza zabuni za ujenzi mpaka ipate gharama halisi za ujenzi huo.

“Upembuzi yakinifu tayari ulikwishafanyika, kinachosubiriwa tu ni gharama halisi za ujenzi ili zabuni ziweze kutangazwa, kwa sababu huwezi kupanga bajeti mpaka ujue gharama halisi,’ Moshi aliiambia FikraPevu.

Urefu wa Reli

Ramani inayoonyesha mahali Reli ya Kusini itakakopita.

Reli hiyo inaelezwa kwamba itakuwa na urefu wa jumla ya kilometa 997 ambazo zinahusisha njia kuu (main line) pamoja na michepuko (spurs).

Moshi ameieleza FikraPevu kwamba, kipande cha reli kutoka Ameilia bay-Songea kitakuwa na jumla ya kilometa 293 ambazo zinahusisha kilometa 164 za njia kuu na zilizobaki ni za michepuko.

Aidha, Songea-Tunduru kutakuwa na jumla ya kilometa 316 zinazohusisha kilometa 211 za njia kuu na 129km za michepuko, wakati kipande cha Tunduru-Masasi kitakuwa na jumla ya kilometa 180 za njia kuu pekee.

“Kipande cha Masasi-Mtwara nacho kitakuwa na urefu wa kilometa 208 pekee,’ alisema Moshi.

Umuhimu wa Reli ya Kusini

Kiwanda cha saruji za Dangote kilichoko Mtwara

Umuhimu wa Reli ya Kusini ni mkubwa kwani maeneo ya kusini mbali ya kuwa na utajiri wa mafuta na gesi, lakini pia kuna hazina kubwa ya madini iliyoko Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa.

FikraPevu inafahamu kwamba, mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma unakadiriwa kuwa na hazina ya tani 540 milioni wakati hazina ya chuma cha pua iliyopo Liganga inakadiriwa kuwa tani 45 milioni, ambapo miradi yote pacha imepewa kampuni ya Sichuan Hongda Corporation ya China.

Ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay unakuja takriban miaka 45 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya TAZARA (maarufu kama Reli ya Uhuru) yenye urefu wa 1,860km, mradi uliogharimu kiasi cha Dola za Marekani 500 milioni ambazo zilikuwa mkopo kutoka Serikali ya China, ikiunganisha miji ya Dar es Salaam nchini Tanzania na New Kapri Mposhi, Zambia.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, ujenzi wa reli hiyo utafungua fursa za maendeleo katika Korido ya Maendeleo Mtwara (MDC) inayohusisha mikoa nane ambayo ina idadi ya watu 9,432,285 (karibu 21.6% ya Watanzania wote), na pia kukuza mtandao wa biashara kati ya Tanzania na nchi za Malawi, Msumbiji na Zambia kwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha uchumi kwa bidhaa za ndani na nje.

Malawi kwa kiasi kikubwa inategemea njia mbili za reli zinazoiunganisha na bandari katika Bahari ya Hindi – Reli ya Trans-Zambezia yenye urefu wa 269km ikitokea kwenye ukingo wa kusini wa Mto Zambezi hadi kwenye reli kuu ya kutoka Beira kwenda Zambia, na reli ya kwenda bandari ya Nacala nchini Msumbiji, hivyo endapo reli ya Mtwara-Mbamba Bay itajengwa inaweza kuisaidia Malawi kwa kiasi kikubwa.

Madini, mafuta na gesi Kusini

Uchimbaji wa Uranium katika eneo la Mto Mkuju wilayani Namtumbo.

Rasilimali za madini, mafuta na gesi katika Korido ya Maendeleo ya Mtwara, ni nyingi kwa sasa na kwa mujibu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), korido hiyo ina hazina kubwa ya madini huku kampuni nyingi za kigeni zikiwa zimeingia mikataba mbalimbali ya uchimbaji na utafiti.

FikraPevu inatambua kwamba, katika Pori la Akiba la Selous ambalo ni Urithi wa Dunia, tayari uchimbaji wa urani kwenye Mto Mkuju wilayani Namtumbo umekwishaanza tangu mwaka 2013 chini ya kampuni ya Uranium One inayomilikiwa na kampuni ya Atomredmetzoloto (ARMZ) iliyo chini ya Rosatom State Atomic Energy Corporation inayomilikiwa na serikali ya Russia.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uranium One iliyofanya utafiti katika eneo hilo, Chris Sattler, alikaririwa Juni 21, 2011 akisema kiwango cha uzalishaji wa urani kinaweza kuwa kati ya tani 1,900 na 2,700 kwa mwaka, lakini kwa wastani unaweza kuzalisha tani 1,600 za urani ya manjano (yellow cake) kwa gharama ya Shs. 34,545 kwa paundi moja, hivyo kuifanya Tanzania nchi ya tatu kwa uzalishaji wa urani barani Afrika.

Wakati akizindua ofisi mpya za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) jijini Arusha Mei 7, 2010, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema Tanzania ilikuwa inaingia katika orodha ya nchi zinazozalisha kwa wingi urani duniani.

"Kama akiba yote tuliyonayo itatumiwa vizuri, Tanzania itakuwa nchi ya saba duniani kwa uzalishaji wa urani," alisema Kikwete. Kwa ujumla, Tanzania ina akiba ya tani 20,769 za urani ghafi.

Takwimu kutoka NDC, ambazo FikraPevu imeziona, zinaeleza kwamba kuna maeneo yenye makaa ya mawe Mbamba Bay kwenye ukingo wa Ziwa Nyasa ambayo yana hazina ya tani 29 milioni ingawa iliyothibitishwa ni tani 2.4 milioni ambazo zinaweza kuchimbwa na wachimbaji wadogo na kuzalisha tani 75,000 za ujazo kwa mwaka, hivyo kuzalisha Shs. 4.2 bilioni kwa mwaka.

Uchimbaji wa makaa ya mawe katika eneo la Ngaka wilayani Mbinga

Takwimu hizo zinathibitisha kuwepo kwa mradi wa makaa ya mawe Namwele-Nkomolo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa wenye tani 1.5 milioni zilizothibitishwa na hazina ya tani 17.2 milioni ambazo zinaweza kuzalisha Shs. 19.8 bilioni kwa mwaka.

FikraPevu inajua kwamba, utafiti huo ulifanywa na kampuni ya Edenville Energy ambayo pia ndiyo iliyofanya utafiti katika maeneo ya Muze mkoani Rukwa.

Aidha, machimbo ya makaa yam awe ya Ngaka wilayani Mbinga yanatajwa kuwa na akiba iliyothibitika ya tani 97.7 milioni na tani 200 milioni za akiba huku yakitajwa kwamba yanaweza kuliingizia taifa kiasi cha Shs. 5.3 bilioni kwa mwaka.

“Mradi wa makaa ya mawe wa Muze ambao unaweza kuzalisha umeme kwenye ukingo wa Ziwa Rukwa una akiba ya tani 3.41 milioni na hazina ya tani 56.59 milioni ambazo zinaweza kuzalisha 300MW za umeme. Pato la mwaka linakadiriwa kufikia Shs. 188.4 bilioni,” takwimu hizo zinaonyesha.

Pato la taifa kuongezeka

Watafiti mbalimbali wameiambia FikraPevu kwamba, endapo serikali itajenga kilometa hizo za reli na kuboresha huduma katika Reli ya Uhuru (Reli ya Tazara) yenye urefu wa 1,860km kutoka Dar es Salaam hadi New Kapri Mposhi kule Zambia, pato la taifa linaweza kuongezeka kwa usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kuchochea maendeleo kwa wananchi wa Korido ya Maendeleo ya Mtwara na maeneo mengineyo.

Enoch Ugulumu, mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Iringa, anasema miradi hiyo haiwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa miundombinu bora, reli ikiwa mojawapo.

“Reli hiyo itasaidia eneo lote la kusini mwa Tanzania kwa sababu uzalishaji utakapoanza italazimu kusafirisha mali… Kuna uwanja mpya wa ndege wa Mbeya, lakini mbali ya barabara zinazoendelea kujengwa, tunahitaji reli ya uhakika,” anasema.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, anaamini kwamba mafanikio ya uwekezaji wa Wachina kwenye migodi ya Liganga na Mchuchuma yatachangia ongezeko la ajira mpya kwa wazawa na pia kuongeza pato la taifa na maslahi zaidi ya kijamii kwa wananchi wa Korido ya Mtwara.

“Reli hii na uwekezaji huu ni muhimu kwa maendeleo ya korido hii, tunakaribisha uwekezaji wowote unaokuja kwenye eneo letu na kwa upande wangu naona Wachina wamefanya jambo jema sana,” anasema Mwambungu.

Tunachokijua FikraPevu

Sehemu ya Milima ya Livingstone wilayani Mbinga.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonesha kwamba, ujenzi wa reli hiyo ulikuwa uanze tangu mwaka 2015, kwani tayari upembuzi yakinifu ulikuwa umekamilika na wakati huo mradi huo ulikuwa katika hatua ya ubunifu wa ujenzi chini ya Mshauri Mwelekezi kampuni ya Dong Myeong Engineering Consultant ya Korea Kusini.

Wakati huo ilielezwa kwamba, ujenzi wa reli hiyo ungegharimu Dola za Marekani 3.6 bilioni (takriban Shs. 7.2 trilioni) na taarifa zilisema ulitarajiwa kujengwa na kampuni ya China Railway No. 2 Engineering Group (CREGC) ambayo ni kampuni tanzu ya China Railway Group Limited.

Mwaka 2013 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Injinia Bernhard Tito, alikaririwa na vyombo vya habari akisema zabuni zilikuwa zimetangazwa kwa wawekezaji wenye sifa kujitokeza kuwekeza kwenye mradi huo kupitia uhandisi, manunuzi, ujenzi na masuala ya fedha, zabuni ambazo zilifunguliwa Juni 21, 2013.

"Kampuni 12 ziliomba zabuni lakini sisi tumeteua kampuni sita kuzishindanisha," alisema Tito bila kufafanua kuhusu kampuni hizo na mahali zinakotoka.

Upembuzi yakinifu wa mradi huo ulipangwa kugharimu TShs. 8 bilioni, na kwa mujibu wa tangazo la zabuni, ulipangwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2013/2014 kabla ya kutathmini umuhimu wa kiuchumi na taratibu nyingine za utekelezaji wa mradi huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *