Miss Tanzania Yaomba Radhi janga la meli

Jamii Africa

Waandaji wa mashindano ya Ulimbwende ya Miss Tanzania yaliyofanyika siku ya Jumamosi tarehe 10 Septemba 2011 wametoa tamko la kuomba radhi kwa kuendelea na mashindano hayo wakati taifa lilikuwa limeingia kwenye msiba mzito kufuatia kuzama kwa meli iliyoua watu 201 huko Nungwi Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashindano hayo Bw. Hashim Lundenga uamuzi wa kuendelea na mashindano hayo ulikuwa ni wa kampuni yake ya Lino International ndiyo iliyokuwa inawajibika na uandaaji na uendeshaji wa mashindano hayo. “Kama waandaaji tunapenda kusisitiza kwamba tunawajibika kwa hayo yaliyotokea na si taasisi yoyote au kampuni yoyote” imesema taarifa hiyo katika kile kinachoonekana kuingilia kati na kukinga wadhamini wakubwa wa mashindano hayo wa Vodacom.

Mara tu baada ya tukio la kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders usiku wa kuamkia Jumamosi hiyo watu wengi walikuwa wameanza kutoa wito kwa mashindano hayo kuahirishwa kwani yasingekuwa yanaonesha kujali kama yangeendelea wakati taifa limegubikwa na msiba mzito. Ilikuwa ni mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe ambaye alielezea mpango wake wa kugomea kampuni ya Vodacom kwa siku ya Jumatatu kuonesha kutofurahishwa na uamuzi wa Miss Tanzania kuendelea.

Wadhamini wengine wa mashindano ya Miss Tanzania ni pamoja na Shivacom, StarTV, TANAPA na Redds. Hata hivyo kampeni ya kugomea ilihusu Vodacom zaidi bila ya shaka kwa sababu wao ndio wadhamini wakuu na ambao jina lao linabeba mashindano hayo.

Hata hivyo katika maelezo yake Bw. Lundenga amesema kwamba uamuzi wa kuendelea na mashindano hayo ulifanyika baada ya kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo uamuzi wa serikali kutangaza siku tatu za maombolezo zikiwa yamebakia masaa machache kabla ya mashindano. “Wenzetu wa TFF waliendelea na mechi ikiwemo ya Yanga na Ruvu Shooting stars” imesema taarifa hiyo ya Bw. Lundenga na kuwa “Katika kumbi za starehe ikiwemo mabaa na burudani za muziki wa bendi na kumbi za disko ziliendelea kama kawaida.

Bw. Lundenga amesema pia kuwa pamoja na kuendelea na mashindano hayo washindani wote na wote waliokuwepo ukumbini walijulishwa juu ya hali hiyo. Kwa mujibu wake walimbwende wote walipoingia mara ya kwanza walikuwa wamevaa vitambaa vyeusi mkononi kuashiria ishara ya msiba na kuwa kabla ya kuanza mashindano yenyewe ukumbi mzima ulisimama kwa dakika moja kuonesha heshima kwa waliokufa katika ajali hiyo kubwa zaidi ya meli kutokea katika visiwa vya Zanzibar katika kumbukumbu.

Pamoja na hayo waandaji hao wanakiri kuwa kuendelea kwa mashindano hayo kumeonekana kuwakwaza Watanzania wengine na bila kujiuma maneno wamekubali kubeba lawama zote. “Kwa sababu hiyo na pia hali halisi ya janga hilo na kwa niaba ya viongozi wenzangu na wadau wa shughuli zetu tunatoa tamko la dhati kwa familia za ndugu wote waliokumbwa na maafa haya, wale wote walionusurika katika ajali hii na Watanzania wote kwa ujumla kwamba TUNAWAOMBA RADHI KWA MKANGANYIKO WOTE ULIOTOKEA HADI KUFIKIA HALI HII.  Hatuna neno zaidi ya kusema na kusisitiza “TUNAOMBA RADHI” Imemaliza taarifa hiyo.

Inatarajiwa kuwa baada ya uongozi husika wa serikali ya Visiwani na wadau mbalimbali radhi hiyo inayoombwa na kina Lundenga yumkini yaweza kutolewa na hivyo kusafisha njia ya mahusiano mapya kati ya wadhamini, waandaji wa mashindano hayo na wahanga wa ajali hii. Hata hivyo hadi taarifa hii inatolewa kauli ya kukubaliwa kwa radhi hiyo haijatolewa na inahisiwa kutokana na shughuli za Miss Tanzania yawezekana ikawa ngumu kupatikana kwani mashindano hayo ya Miss Tanzania yanaangaliwa na baadhi ya watu kama ni mashindano ya aibu na hivyo kukubali radhi hiyo ni sawa na kuyatambua au kuyakubali.

3 Comments
  • Ni upumbavu na udhaifu kuhalalisha udhaifu wako eti tu kwa sababu kuna watu wengine wanakosea kama wewe, sisi tunaweza kuwasamehe, lakini sidhani kwa roho za waliokufa kama zitakuwa tayari kufanya hivyo kwa sababu hawa jamaa waliamua kufanya makusudi kwa sababu walijua wataomba msamaha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *