MJADALA: Ni sahihi kufunika au kukiacha kidonda wazi?

Jamii Africa

Nakumbuka nikiwa mdogo, nilikuwa naambiwa kama nimepata jeraha au kidonda basi nikiache wazi ili kipate hewa safi hasa kama kidonda ni kibichi. Sikuwa na ufahamu kuhoji maelekezo hayo lakini nilitii nikiamini kukiacha kidonga wazi ni jambo jema.

Jambo la kushangaza baada ya miaka yote hiyo, bado nawaona watu wengi wanaviacha vidonda vyao wazi ili vipone haraka.

Lakini ukienda hospitali na kidonda kibichi, jambo la kwanza ambalo Muuguzi atafanya ni kukisafisha kidonda na kukifunika au kukifunga. Kwanini anafanya hivyo?

Ikiwa kukiacha kidonda wazi ni jambo jema ili kipone haraka, sasa kwanini madaktari wanashauri kufunika kidonda kwa nguo, kitambaa na bendeji (bandages)?

Ndiyo! Kukiacha kidonda wazi ili kipone haraka ni makosa, lakini siyo kwa majeraha madogo, au michubuko, ni jambo zuri kukifunika.

 

Gaga (Scabs)

Mwili wa binadamu ni kama mashine, lakini utofauti wake ni kwamba umeumbwa kwa miunganiko ya biolojia. Ina njia mbalimbali za kukabiliana na majeraha lakini njia ambayo imezoeleka kukitibu kidonda ni utengenezaji wa gaga (scab).

Mchakato wa kutengeneza gaga unaanza muda mfupi baada ya kupata jeraha na damu zinapotoka.  Chembechembe nyeupe damu ambazo ni mahususi kuzuia uvujaji wa damu  hujikusanya pamoja kwenye eneo lenye jeraha (ulipojikata, mchubuko au alama ya kipigo) na kuganda juu ya ngozi.

Kuganda kwa hiyo damu juu ya kidonda ni ulinzi wa kibaolojia na husaidia kuzuia uvujaji zaidi wa damu. Mgando huo wa damu juu ya kidonda hukauka na kuwa mgumu na kuunda gaga. Na wakati mwingine mgonjwa hulitoa gaga likikauka.

                                       Gaga ni ulinzi asilia dhidi ya vimelea vya wadudu

Gaga ni ulinzi asilia dhidi ya vimelea vya wadudu lakini kiukweli sio njia nzuri ya kutibu kidonda. Gaga linahatarisha mchakato wa uponyaji kwa kuweka kizuizi cha ukavu na seli zilizokufa. Ngozi yenye afya inatakiwa ifanye mchakato yenyewe ndani kwa kuunda tishu mpya ili kuziondoa seli zilikufa na kuharakisha uponyaji.

Kukiacha kidonda wazi eti kipate hewa, sio wazo zuri hasa kama kinavuja damu.

 

Kwanini inashauriwa kufunika kidonda?

Ikiwa kidonda kibichi kikifungwa au kufunikwa, kinaepusha  seli za ngozi kukauka na kutengeneza gaga, jambo linalopunguza uwezekano wa kupata kovu kwenye eneo la kidonda.

Kukifunga kidonda kuna faida nyingi ikiwemo kutunza unyevunyevu ambao unasaidia uponyaji mzuri wa ngozi.

           Bendeji au kitambaa kinaongeza ulinzi kwenye kidonda

Pia inapunguza uwezekano wa kupata maambukizi kwasababu inazuia vimelea vya wadudu, vumbi, uchafu na maji kukutana na jeraha. Kukiacha kidonda wazi kunaweza kutenegenza tatizo kubwa zaidi la kiafya.

Zaidi, ni rahisi kwa gaga lililofunika kidonda kutoka kama tulivyogusia awali kuwa baadhi ya watu wanatoa gaga likikauka, katika hali hiyo unaweza ukajitonesha na kuibua jeraha tena.

Kinyume chake bendeji au kitambaa kinaongeza ulinzi kwenye kidonda. Pia inakukinga kujiumiza tena.

Kwa vyovyote vile, ni muhimu kukifunika kidonda kwasababu inasaidia kukilinda na inaharakisha mchakato wa uponyaji.

1 Comment
  • Inategemea na aina ya kidonda/jeraha, mfano jeraha la kukatwa na kitu chenye makali kama vile kisu au wembe huweza kutibiwa kwa kusafishwa vizuri na kufungwa. Ila majeraha ya kung’atwa na wanyama kama mbwa n.k au vidonda sugu vinavyoendelea kutunga usaha sio vema kuvifunika kwa muda mrefu maana kuvifunika ni kuwapa nafasi na mazingira mazuri bakteria kuzaliana zaidi na kufanya hali ya mgonjwa kuwa mbaya zaidi na hivyo kuchelewesha uponaji wa kidonda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *