Mkwamo wa elimu nchini ni matokeo ya usimamizi wa shule usioridhisha

Jamii Africa

Benki ya Dunia imeeleza kuwa watoto wengi wanaondikishwa katika shule za msingi nchini hawapati maarifa ya msingi kutokana na kukosekana kwa usimamizi wa walimu na wanafunzi wawapo shuleni.

Kulingana na ripoti ya utafiti iliyotolewa na Benki hiyo leo jijini Dar es Salaam kuhusu, Kuangalia Mbele: Elimu na Kujifunza barani Afrika inaelezwa kuwa watoto wengi waliopo shuleni hawapati maarifa ya msingi na ujuzi kuwawezesha kushindana katika soko la ajira.

Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo, Maneja wa Benki ya Dunia anayesimamia Elimu katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Africa, Dkt. Sajitha Bashir amesema katika utafiti huo wamebaini changamoto hiyo ya elimu inasababishwa na usimamizi mbovu wa shule na uwekezaji usioendana na mahitaji ya wanafunzi, ongezeko la wanafunzi shuleni na uwezo mdogo wa walimu kufundisha.

“Mwishoni mwa darasa la 2 watoto wanatakiwa kusoma vizuri maneno 45 hadi 60 kwa dakika na wakifika darasa la 4 wanatakiwa kusoma insha ambayo hawajawahi kuiona na kujibu maswali ya imla kwa ufasaha lakini wanafunzi wengi hawawezi kusoma”.

Ameongeza kuwa watoto wa Tanzania wanaweza kusoma vizuri somo la Kiswahili kwasababu ni lugha ya kufundishia lakini kwenye somo la kiingereza hawafanyi vizuri. “Kama hawawezi kusoma aya moja una uhakika kwamba hawawezi kuendelea kwasababu hawataweza kusoma vitabu”.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kitengo cha Elimu, Dkt. Jaime Saavedra amesema  kikwazo cha wanafunzi kujifunza ni  kutosimamiwa vizuri kwa utekelezaji wa mitaala ya elimu na walimu ikiwemo walimu kushindwa kumudu majukumu yao ya kufundisha.

“Katika mifumo mbalimbali ya elimu duniani, mtu wa kwanza anayewajibika katika usimamizi wa shule kwa kawaida ni mwalimu”, amesema na kuongeza kuwa walimu hawawezi kufundisha kama hawajawekewa utaratibu mzuri wa kufundisha, motisha na kukubali mchango walionao katika sekta ya elimu.

            Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akizungumza leo kwenye uzinduzi wa ripoti ya Benki ya Dunia

 

Serikali yatoa tamko

Akizungumza kwenye  uzinduzi wa ripoti hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema utafiti huo unatoa mwanga wa mageuzi ya elimu nchini na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa ya msingi wawapo shuleni.

“Naishukuru Benki ya Dunia kwa uzinduzi wa ripoti hii muhimu kwa mageuzi ya elimu nchini. Lengo la kitabu hiki ni kusisitiza wanafunzi waliopo shuleni kupata maarifa yaliyokusudiwa kwasababu baadhi ya wanafunzi hawapati stadi muhimu”.

Ameongeza kuwa serikali imepokea changamoto zilizotolewa na utafiti hasa kwa wanafunzi ambao hawapati stadi za msingi na inafanya juhudi za kuboresha mitaala ya elimu na kuajiri walimu wenye sifa.

“Tunafanya juhudi mbalimbali ikiwemo kuimarisha mitaala ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata maaarifa sahihi. Pia tunajitahidi kuboresha utoaji wa elimu bora kwa kuajiri walimu wenye uwezo mzuri wa kufundisha na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo hayana walimu wa kutosha”, amesema Prof. Ndalichako.

Amefafanua kuwa wamefanikiwa kuongeza ruzuku kwa wanafunzi wa shule za msingi ambapo wizara yake inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma katika mazingira mazuri. 

“Kupitia mpango bila malipo tumeweza kuongeza idadi ya wanafunzi waliopo shuleni na tunaendelea kukabiliana na msongamano wa wanafunzi hao shuleni”, amesema Prof. Ndalichako.

 

Wadau wa elimu nao watoa ya moyoni

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema ili kutatua changamoto ya ujifunzaji shuleni, serikali haina budi kuongeza wigo wa utolewaji wa huduma za jamii kama maji, umeme, chakula kwa wanafunzi wa shule zilizopo pembezoni mwa nchi.

Amesema elimu ya Tanzania haitolewi kwa usawa ambapo wanaofaidika zaidi ni wanafunzi wa shule za mjini huku wale wa vijijini wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za ukosefu wa walimu na usimamizi wa shule usiorodhisha.

Ripoti ya Twaweza (2017) inaeleza kuwa, “Mkoani Dar es Salaam, nusu ya shule (51%) zina huduma ya umeme, lakini Geita ni shule 2 tu (4%) kati ya 50 zinazopata huduma hiyo. Mkoani Geita, shule moja kati kumi (12%) ina huduma ya maji safi na salama lakini mkoa wa Kilimanjaro karibu shule 8 kati ya 10 (78%) zina huduma hiyo”.

Mgawanyo huo usio sawa wa huduma za kijamii unawaathiri zaidi watoto wanaosoma katika shule zilizopo pembezoni mwa nchi hasa maeneo ya vijijini ambako wazazi wengi hawajaelimika na wanakabiliwa na umasikini wa kipato.

Kwa upande wake, Mwalimu Halima Kamote amesema ili kuboresha elimu nchini ni muhimu kuimarisha nidhani ya kazi, kutoa masomo ya ziada kwa wanafunzi, ushirikiano mzuri kati ya wazazi na wanafunzi, kutolewa kwa ushauri na mwongozo wa maisha kwa wanafunzi na mwisho kuwawezesha wanafunzi  kupitia klabu ili wajengewe uwezo wa kujiamini.

Akiahirisha uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Benki ya Dunia kuhusu Elimu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema utafiti huo umetoa mwanga kwa Tanzania na amewataka wadau wa elimu kushikamana na serikali katika mageuzi ya elimu nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *