Mlima wa hifadhi wauzwa bila ridhaa ya wananchi!

Albano Midelo

MLIMA ambao umetengwa kwa ajili ya hifadhi ya msitu katika kijiji cha Nkali kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoani Ruvuma umeuzwa na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya kijiji hicho bila ridhaa ya wananchi.

Habari za uhakika zilizoifikia Fikra Pevu zinaeleza kwamba mlima huo umeuzwa kimya kimya miaka kadhaa iliyopita na sasa mnunuzi ameanza kuharibu mazingira kwa kufanya shughuli za kibinadamu.

Mlima huo wenye ukubwa wa  hekta zaidi ya 100 unaofahamika kwa jina la Hitombi hiveli yaani mlima wenye vilele viwili uliopo kilometa mbili kutoka fukwe za ziwa Nyasa  umeuzwa hekta 20 tangu mwaka 2008 na mnunuzi  ameanza  shughuli za kibinadamu juu ya mlima huo hali ambayo inahatarisha usalama wa viumbe hai waliomo katika msitu huo.

mlima-hitombi

Sehemu ya mlima wa Hitombi hiveli ambao sehemu yake imeuzwa bila kuwashirikisha wananchi

Hitombi hiveli ni mlima wenye msitu mnene uliotengwa na kijiji kwa ajili ya hifadhi kutokana na mlima huo kuwa  makazi ya wanyama  pamoja na viumbehai wengine wakiwemo wadudu,mimea na wanyama adimu  kama mbega wenye rangi nyeupe na nyeusi  ambao wapo hatarini kutoweka.

Victor Komba ni mwenyekiti wa kamati ya mazingira katika kijiji cha Nkali anawataja Viumbe wengine ambao wanapatikana katika msitu huo ni sungura pori, ngedere, nyani, digidigi na  mbweha.

Anawataja viumbe wengine wanaopatikana katika mlima huo kuwa ni pamoja na  nungunungu, panya buku wakubwa wenye uzito hadi kilo 25.

Anasema mlima huo pia ni  makazi ya  wadudu wa aina mbalimbali, utajiri wa mimea mingi ya asili kama uyoga wa asili na makazi ya ndege maarufu aina ya ngwazi mwenye uwezo wa kuvua samaki.

Kaimu mtendaji wa kijiji cha Nkali Barnaba Mbele anasema  mlima huo  ulitengwa na kuhifadhiwa kuwa moja ya maeneo ya hifadhi ya msitu wa kijiji hicho lengo likiwa ni kuuhifadhi  kutokana na ukweli kuwa mlima huo umekuwa chanzo cha mvua katika vijiji vinavyozunguka kata ya Liuli.

Amevitaja vijiji ambavyo vinazunguka kata ya Liuli na vinautegemea mlima huo kwa ajili ya mvua kuwa ni pamoja na  Hongi,Nkali,Liuli,Puulu na Nkalachi na kwamba kitendo cha baadhi ya viongozi kuuza sehemu ya mlima huo bila ridhaa ya wananchi wote hakikubaliki na kwamba mnunuzi anatakiwa kusimama kuendelea kufanyakazi za kibinadamu katika mlima huo hadi hapo mgogoro huo utakapokamilika.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nkali, Menas Kilimo anadai kuwa viongozi watatu wa Halmashauri ya kijiji hicho wanadaiwa kuuza  sehemu ya mlima huo tangu mwaka 2008 ambapo mnunuzi ameanza kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye mlima huo bila kujali athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza.
 
Viongozi wanaotuhumiwa kuuza mlima huo ni wajumbe watatu wa Halmashauri ya kijiji hicho ambao ni Aidan Mbungu, Desderius Mbunda na Mathias Chilambo ambao kwa pamoja wanadaiwa kuuza eneo la ukubwa wa hekta 20 kati ya hekta 100 za mlima huo.

Kaimu mtendaji wa kijiji cha Nkali  Barnaba Mbele  alidai kuwa viongozi hao kwa kushirikiana na mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Mathayo Konjakonja pamoja na mtendaji mstaafu wa kijiji hicho Sarah Chitunji, inadaiwa katika kipindi cha mwaka 2007/2008 waliuza  sehemu ya mlima bila ridhaa ya wanakijiji .

Mbele alibainisha kuwa tangu wakati huo hadi sasa wananchi walikuwa wanalalamika kuhusu kitendo hicho huku mnunuzi wa sehemu ya mlima huo ameanza kufanya shughuli za kibinadamu tangu mwaka 2011 .

Hivi karibuni wananchi  wa vitongoji vya  Mshale na Muungano wanaozunguka mlima huo  baada ya kubaini mnunuzi anaendelea na kazi juu ya mlima huo  waliamua  kwenda kwa mwenyekiti wa sasa wa kijiji cha Nkali, Venancy Kilimo wakidai mlima huo urudishwe mikononi mwa wananchi na uendelee kuwa hifadhi.

Bernad Challe,Amoni Bwanga,Musa Haule na Joseph Sangana wakazi wa kijiji cha Nkali wamemtaka afisa mtendaji wa kijiji cha Nkali Denis Mangwea asimamie sakata hilo ili viongozi hao wanaotuhumiwa wapelekwa katika vyombo vya sheria huku wakitoa rai kwa mwenyekiti wa kijiji hicho  kufufua kamati ya ulinzi na usalama ili kuongeza ulinzi  dhidi ya mlima huo.

Charles Chawila diwani wa kata ya Liuli amekiri ofisi yake kupata taarifa za  sehemu ya mlima huo wa asili kudaiwa kuuzwa na kwamba ofisi yake inatarajia kufanya mazungumzo na mnunuzi wa sehemu ya mlima huo ili  asiendelea kufanya shughuli za kibindamu hadi mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi.

“Mlima huu ni muhimu katika kata yangu kwa kuwa unachangia kwa asilimia 90 mvua zinazonyesha kila mwaka hivyo siwezi kukubali  uharibifu wa mazingira kuendelea kufanyika katika mlima wa hifadhi hata kama mnunuzi anadai ameuziwa kihalali na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya kijiji ambao hawakuwashirikisha wananchi’’,alisisitiza Chawala.

mwanakijiji

Mmoja wa wazee maarufu katika kijiji cha Nkali akielezea kuhusu mlima wa hifadhi wa Hitombi hiveli ulivyouzwa bila ridhaa ya wanakijiji

Hata hivyo sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999 fungu la nane inaelekeza kuwa Halmashauri ya kijiji ina jukumu la kusimamia ardhi yote ya kijiji kwa kuzingatia utunzaji wa ardhi,maliasili na mazingira na kwamba Halmashauri ya kijiji itagawa ardhi baada ya kuruhusiwa na mkutano wa kijiji na sio vinginevyo.

Kulingana na sheria hiyo mkutano wa kijiji unatakiwa kuwa na wanakijiji wasiopungua 100 ambao wanaweza kupeleka malalamiko yao ya namna Halmashauri ya kijiji inavyoshindwa kusimamia ardhi ya kijiji kwa Halmashauri ya wilaya ambayo itamtaarifu kamishina wa ardhi ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Dk.Rugemeleza Nshala ni mtaalamu wa ardhi na mwanasheria anabainisha kuwa kisheria mtu binafsi anaruhusiwa kumiliki ardhi na kutahadharisha kuwa  haruhusiwi kumiliki visiwa vya karibu,fukwe au mlima  ambapo sheria ya ardhi ya mwaka 2004 inazuia mtu kufanyakazi eneo la meta 60 kutoka kingo za mito,maziwa na bahari ambapo kiulimwengu hairuhusiwi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya meta 200.

Injinia Stella Manyanya ni mbunge na mjumbe wa Bodi ya utalii mkoa Ruvuma anatoa wito kwa wadau wote wa sekta ya utalii  mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa wanayalinda maeneo yote yaliohifadhiwa ili yasiendelee kuharibiwa na hatimaye kuathiri kwa namna moja au nyingine mazingira na sekta ya utalii  katika ukanda wa kusini.

Tangu serikali ilipotangaza kufunguliwa kwa Mtwara korido pamoja na kutangazwa kwa wilaya mpya ya  Nyasa  wawekezaji wengi wamekuwa wanajitokeza kutafuta maeneo ya uwekezaji mwambao mwa ziwa Nyasa huku baadhi yao wakipata maeneo kwa njia haramu ikiwemo   kuwatumia viongozi wa vijiji  bila kuwahusisha wananchi.

1 Comment
  • Hali hii inatokana na serikali kuendeleza mfumo wa kikoloni iliyourithi mfumo uliotaka maamuzi yote yaanzie juu kuja chini(top down Approach.

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *