MSIMU WA MAVUNO: Tanzania inavyoweza kufaidika na soko la mazao Pembe ya Afrika

Jamii Africa

Serikali ya Tanzania imeshauriwa kufungua milango kwa wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi ili kufaidika na ukuaji wa bei ya soko katika nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.

Ushauri huo unakuja wakati ikiwa imebaki miezi michache kwa wakulima hasa wa mahindi na maharage kuanza kuvuna mazao hayo katika maeneo mbalimbali ya nchi yanayopata msimu mmoja na mwili ya mvua.

Kulingana na Ripoti ya Mapitio ya Usalama wa Chakula katika nchi za Pembe ya Afrika, inaeleza kuwa bei ya mazao ya chakula itaongezeka mara dufu katika kipindi cha miezi miwili ijayo ya uvunaji kutokana na  mafuriko, wadudu na magonjwa yaliyoripotiwa katika maeneo hayo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kaya katika nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, Somalia na Sudan ambazo zinategemea soko la chakula, zitakabiliwa na ongezeko la bei kwasababu ya kupungua kwa chakula cha mazao sokoni.

Kwa muda mrefu sasa, nchi za pembe ya Afrika zimekuwa zikikabiliwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukame na mvua kubwa  ambazo zimepunguza uzalishaji wa mazao na kuzilazimisha kuagiza chakula katika nchi zingine ikiwemo Tanzania.

“Wastani wa juu wa bei ya chakula utaendelea kuathiri nguvu ya soko ya kaya maskini nchini Uganda, Rwanda, Somalia na Sudan, ambazo zinaelekea kwenye msimu wa mavuno,” imeeleza ripoti hiyo.

Wiki iliyopita tani moja ya mahindi iliuzwa kwa Dola za Marekani 402.14 (Tsh. 915,962) katika mji wa Kisumu Kenya, wakati Ruhuha, Rwanda tani moja iliuzwa kwa Dola 319 (Tsh. 729,562) na katika mji wa Kabale, Uganda ilikuwa dola 271.02.

Miezi sita iliyopita, tani1 ya mahindi iliuzwa kwa dola 540.28 (milioni 1.230) katika Mji wa Ruhuha na Nairobi (Milioni 1.009). Nchini Burundi, asimilia 60 tu ya kaya ndiyo zina chakula.

                     Nchi za pembe ya Afrika zitalazimika kuagiza mazao toka nchi nyingine

Upungufu wa chakula katika nchi za pembe ya Afrika unatokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni ambapo ziliharibu kwa kiasi kikubwa mazao yaliyokuwepo shambani.

 

Miundombinu ya Barabara

Kwa upande mwingine, mvua zilizonyesha katika maeneo hayo zimeharibu barabara na kuhatarisha soko la mazao kwasababu  usafiri wa barabara toka mashambani umekuwa mgumu, jambo linakwamisha wakulima kusambaza mazao yao sokoni.

Kikao cha Usalama wa Chakula kilichofanyika Katika kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Igad jijini Nairobi wiki iliyopita, kiliwataka wakulima wa Uganda, Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia kuwa makini na viwavi jeshi ambavyo zinavamia mazao. Wadudu hao ambao hushambulia mazao yakiwa machanga, wamesababisha hasara kubwa kwa wakulima wa nafaka.

Mdudu huyo ambaye anaharibu mazao anapatikana katika wilaya zote 121 za Uganda, kaunti 47 za Kenya, mikoa 17 ya Burundi. Pia katika wilaya 30 za Rwanda na nchi yote ya Ethiopia.

                                       Viwavi jeshi wakivamia mmea ukiwa mchanga

Nchini Kenya, mdudu huyo ameharibu hekta kati ya 11,000 hadi 15,000 za mahindi na Rwanda zaidi ya hekta 15,300. Pia nchini Ethiopia, hekta milioni 1.7 za mahindi zimeharibiwa.

Wakulima pia wamekumbushwa kujiandaa na kuibuka kwa magonjwa ya wanyama kutokana na hali ya maji maji katika maeneo mbalimbali ya malisho.

Hata hivyo, Tanzania itatumia vizuri fursa hii ya soko la mazao ya chakula katika nchi za Pembe ya Afrika au itaendelea na sera yake ya viwanda ambayo inasisitiza kusindikiza mazao na kuuza bidhaa zilizokamilika?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *