Mtwara: Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi!

Zitto Kabwe

Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara.

Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.

Ikumbukwe kwamba, katiba ya nchi ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.

Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.

maandamano

Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanaodai haki yao ya kikatiba.

Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa Mtwara ni kitendo kinachoweza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “Kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.” (Ibara ya 28, 1)

Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana pia Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu ‘wameshapata chao’ na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.

Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu!

Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani! Kwanini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine miwili, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi!

Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastani wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).

Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalotegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.

Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayopendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania haki yao. Hii ni vita ya uwajibikaji! Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.

8 Comments
  • jamani kiongozi mkuu wa nchi yetu abadilishe mawazo ya kuwa saivi watanzania ni wategemezi wa kifkra kama alivyozoea, ufisadi na ubinafsi wa serikali yake imetusimamisha kidete kujitetea wenyewe kudai haki zetu kwani tumegundua aliyeshiba hamjui mwenye njaa, kwa serikali yetu maji ni nzito kuliko maji.

  • Naimba serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano chini ya Jemadari wake Mkuu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete iwasikilize wananchi wa Mtwara na ni busara sana ukiwasikiliza wananchi wako kilio chao. Pia ikumbukwe kuwa Ken Sarowiwa wa Naigeria alikufa kwa kutetea raslimali inayopatikana katika eneo lao, hivyo si ajabu kwa wananchi wa Mtwara kufia haki yao. Mimi binafsi sioni ugomvi huu unatokea wapi kwani kwanini serikali isijenge mtambo wa kufua gesi Mtwara badala ya kusafirisha gesi. Nasema wananchi wa mtwara hawazuii gesi ili isiwanufaishe watanzania wengine kama serikali inavyotutangazia, bali wanachotaka ujengwe mtambo wa kufua gesi kisha kupata umeme mtwara na kisha ukasafirishwa sehemu nyingine ya Tanzania badala ya kuelekeza kila kitu Dar. naseme serikali mkilazimisha bomba hilo litahujumiwa na wananchi wenyewe na hivyo Dar itapokea hewa badala ya gesi

  • Dar es salaam siyo Tanzania, Dar es salaam ni mkoa kama ilivyo mingine. 

    Y? kila ki2 Dar.

    Tuliyakataa hayo wakati wa ukoloni, kuwa mgawanyo mbaya wa rasilimali huleta ununeven devpt, tusilambe matapishi

  • your openness we aprecate,superiority complex is problemes of our leeader.unwises speeches

  • Hivi karibuni nilisoma habari za mapokezi hafifu ya waziri wa Viwanda ndugu Kigoda na hasa upokeaji wa hotuba yake kwa kuzomea pale alipsema gesi ya Mtwara ni nyingi hivyo ni vyema viwanda vya Dar vinavyotumia mafuta kama kuni kama kiwanda cha bia nk vifaidi gesi hii.

    Hili ni jambo zuri lakini bado naumga mkono kujenga Gridi nyingine ya umeme kama gesi hiyo ni nyingi , Gridi hiyo inaweza kupitia Songea Mbeya Tabora hadi Kigoma kwa ajili ya maendeleo ya sehemu hizo.

    Najua Gesi hii kupelekwa Dar itasaidia kukuza ujenzi mwingine wa viwanda katika maeneo ya Dar/ Bagamoyo, Tanga Kilimanjaro na Arusha

    Mheshimiwa Kigoda umepewa tena dhamana na serikali ya Kikwete kufufua viwanda na kujenga vipya  baada ya ile ya Benjamini Mkapa ambayo ilikuwa na uuzaji wa viwanda ni vyema ukawaonyesha watanzania kuwa kweli sasa una mpango wa kuendeleza viwanda ili kuwapatia watanzania AJIRA

    Mungu ibariki Tanzania

  • Suala la Mtwara kutaka kujitenga lilianza toka enzi za Mwl Nyerere kwa akina Stephen Nandonde kulieleza bunge waziwazi

  •       Suala la Mtwara kutaka kujitenga lilikuwepo toka enzi ya Mwl Julius Nyerere na wabunge wa kusini chini ya Stephen Nandonde walishawahi kutoa malalamiko ya kujitenga tena wakiwa bungeni. Inadhaniwa kuwa serikali ilitelekeza eneo la kusini hasa Mtwara na Lindi kwa kuwa eneo hilo lilitumika kama uwanja wa mapambano wa ukombozi wa nchi kusini mwa Afrika, wakatelekeza kujenga barabara na kisha serikali ya Mwalimu wakaing'oa reli, wakang'oa pampu ya maji, wakaondosha kiwanda cha soda Pepsi, na hata baadae kuondoshwa kiwanda cha ku-assamble Land Rover nk. toka enzi hizo wakawa na fikra za kujitenga ama kwa jujiunga na Msumbiji ama kwa kujiendesha wenyewe, hivyo hamasa hizi zilikuwapo toka enzi hizo za awamu ya kwanza.

          Utakapozungumza na wananchi wenyewe wanahisi kutengwa, kudharauliwa na kupuuzwa na serikali kabla na baada ya uhuru na msingi wa serikali ya ukoloni na serikali huru inatokana na imani yao ya dini na kwa dharau hiyo ndio ilikuwa sababu ya waokushiriki katika vita ya majimaji ndivyo wanavyotazama mapambano haya ya kuondosha rasilimali kutoka kusini ikiwamo Gesi ni vita ingine ya majimaji kwao. Kipindi hicho watu wenye silaha dhaifu walipambana na nguvu ya dola wenye silaha na "magwanda' ya khaki na hata viongozi wa dini waliowaungana na wakoloni.

          Pamoja na serikali kudhamiria kujenga mtambo wa kufua gasi asilia LNG huko Madimba, kiwanda cha cement Dangote, kiwanda cha mbolea na viwanda vingine takribani 43 bado hawaridhishwi kama kutakuwa na bomba la kuitoa gesi hiyo kwenda DSM kuongeza uzalishaji wa umeme na kutumika gasi hiyo kwa viwanda na natumizi mengine katika eneo lote litakalopita bomba hilo kama Lindi, Pwani na DSM kisha Tanga na Mbeya nk. kuna minong'ono na inaaminika kuwa gasi hiyo inapelekwa Bagamoyo kuchakatwa na kusafirishwa kupitia bandari hiyo.

          Ingawa ukizungumza na wananchi watakwambia sisi hatupingi watanzania kufaidika na gasi bali wanataka isitoke gesi kama gesi ila ijengwe gridi ya umeme kutoka Mtwara kuja DSM na kwingineko, sasa matumizi ya gasi hii katika viwanda vya ndani ya nchi itakuwa ni kwa umeme tu?

          Watakwambia sisi hatupingi gasi kwenda DSM, Ingawa anaekwambia maneno hayo atakuwa ameshika bango kubwa likiwa limeandikwa Gesi Haitoki Mtwara Hata kwa Bomba la Peni, atasema sisi tunataka kujua namna tutakavyofaidika. Ukizungumziwa namna watakavyofaidika watasema hizo ni ahadi tu walikwisha wahi kudanganywa na mkakati wa Mtwara  corridor wa Bakili Muluzi na Benjamin Mkapa "BM  and BM"  wakiona wanapwaya katika mashiko ya namna watakavyofaidika watasema hatujashirikishwa, Wakishirikishwa viongozi wao wa kijamii na kidini wanasema tunataka tuzungumze nao sisi wenyewe, Akija kiongozi kuzungumza nao wanamshinikiza aanze kwa kukiri kuwa gesi haitoki Mtwara akichelewa kukiri wanamkimbiza na kupiga, pengine hata wakihisi kuna kiongozi anakuja kuzungumza nao wanashambulia gari yake kabla hata hajawafikia wala hata kama hawapata uhakika kama kweli gari hiyo ni moja ya gari ya viongozi wanaowataka kuzungumza nao juu ya kadhia hiyo.

          Mwisho wa kadhia hii wataibuka mashujaa wa muda mfupi na mashujaa wa kudumu, wanaosimamia ukweli hata kama ni mchungu kwa wananchi na wapiga kura wao. Naamini nawe Mhe Zitto utachagua kuwa upande wa ukweli kama uliokuwa nao wakati wa sakata la Tanesco juu ya kununua mitambo ya Dowans, Makamanda wa vita ya ufisadi walibaki na magwanda yao na misimamo yao hali taifa likiendelea kupata hasara hadi leo kwa kukodi na kununua mafuta kwa ajili ya mitambo hiyo. makamanda wengi wakaizika hoja hiyo kimya kimya na magwanda yamewapyaya. hali wakiacha ukweli ukiibuka kuwa mshindi. tusizifanye jazba kuwa ndio nguvu ya umma wala utaalamu unapopingana na nguvu za hisia za waliowengi bado historia itahukumu kwa haki.

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *