Mwanza: Gari la wagonjwa lawekwa juu ya mawe!

Jamii Africa

NAIBU Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Charles Kitwanga ameeleza kukerwa na uongozi wa hospitali na halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, kwa kushindwa kununua tairi za gari la wagonjwa la hospitali hiyo, badala yake gari hilo limewekwa juu ya mawe huku likiharibika.

Kufuatia hali hiyo, Kitwanga ametishia kuunyang’anya uongozi wa hospitali hiyo ya wilaya gari hilo lenye namba SM 6704, ili alipeleke hospitali ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, iwapo utaendelea kulitelekeza kwa kushindwa kulinunulia tairi.

Gari la kubeba wagonjwa (Ambulence), katika hospitali ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, likiwa nimewekwa juu ya mawe, baada ya kudaiwa kukosa tairi mbili za nyuma

Waziri Kitwanga aliyaeleza hayo hii leo wilayani Misungwi, katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa mbali mbali vikiwemo vitanda 50 kwa ajili ya upasuaji, gari na pikipiki ya kubeba wagonjwa kwenye vituo vya afya na zahanati 20 zilizopo wilayani humo, hafla ambayo ilifanyika hospitali ya wilaya.

“Hivi ninyi DMO (Mganga mkuu wa wilaya), na wenzako mmeshindwa kabisa kununua tairi za gari hili la wagonjwa hadi mmeliweka kwenye mawe namna hii?. Au mnataka niwanyang’anye niwape Sekou Toure?”, aling’aka Waziri Kitwanga ambaye ndiye aliyelitoa kama msaada hospitalini hapo mwaka 2009.

Charles Kitwanga

Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Charles Kitwanga, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa kukabidhi vifaa mbali mbali vya hospitali wilaya ya Misungwi. Alikerwa kuona gari la wagonjwa likiwa juu ya mawe

Hata hivyo, Waziri Kitwanga ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Misungwi kupitia CCM, aliagiza kuhakikisha gari hilo linafanyiwa matengenezo ili liweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Kufuatia hali hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Misungwi, Xaviery Tilweselekwa walitofautiana waziwazi na Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Dk. Marco Mwita mbele ya Waziri huyo, katika maelezo juu ya ubovu wa gari hilo, ambapo Mkurugenzi alidai ubovu wa gari hilo si tairi pekee, bali linahitajika kununuliwa vipuli vingine vyenye fedha nyingi.

Kauli hiyo ya Mkurugenzi ilizimwa na Kaimu Mganga Mkuu, Dk. Mwita, ambaye alisema mbele ya Waziri Kitwanga kwamba: “Mimi ndiyo ninayejua, hili gari limekosa tairi tu kwa wiki nne sasa, na siyo vipuri vingine kama alivyosema Mkurugenzi. Kama wanabisha watoe fedha za tairi waone kama gari halitafanyakazi yake”.

Akizungumzia msaada huo wenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 4.52 uliokabidhiwa kwa uongozi wa hospitali hiyo ya wilaya kwa ajili ya kusambaza kwenye vituo husika, Waziri Kitwanga alilipongeza shirika hilo la nchini Denmark na kusema, limekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wananchi wa Misungwi katika sekta mbali mbali za kimaendeleo.

Waziri Kitwanga alisema, kupatikana kwa vifaa hivyo itasaidia zaidi kupunguza kama si kuondoa kabisa adha ya upungufu wa vifaa hivyo, hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma nzuri punde wanapofika kwenye vituo vya afya na zahanati kwa ajili ya kupata huduma za kitabibu.

“Kwanza nilipongeze sana shirika hili la Green Youth Production School kutoka Denmark kwa msaada huu mzuri. Kimsingi limetusaidia sana, maana vifaa hivi tutavisambaza kwenye vituo vya afya na zahanati za Misungwi”, alisema Waziri Kitwanga.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo ya Misungwi, Dk. Marco Mwita, alivitaja vituo vya afya vilivyonufaika na msaada huo kuwa ni pamoja na Mbalika, Misasi, Koromije, Nyang’homango Igokelo, Mwaniko pamoja na Ibongoya.

Kwa mujibu wa Dk. Mwita, vituo vingine ni Mwagala, Mwamboku, Kaunda, Gambajiga, Mahando, Nkinga, Lubili, Nguge, Mwamazengo, Mondo, Misungwi, Bukumbi na Busongo Heath Center, na kwamba vifaa hivyo vitaanza kusambazwa kwenye vituo husika haraka sana iwezekanavyo.

Alisema, kabla ya vifaa hivyo baadhi ya vituo vya afya na zahanati wilayani humo vilikuwa na uhaba mkubwa wa vifaa, na kwamba msaada huo gari na pikipiki ya wagonjwa, vitanda 50, meza 100 baiskeli za kubeba wagonjwa, magodoro 40 nakadhalika vitasaidia kuondoa adha iliyokuwepo.

Habari hii (pamoja na picha) imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

4 Comments
  • akili kali hiyo?waziri na akili zako pikipiki na baiskeli kubeba wagonjwa au ni kudanganya wananchi kwa ajiri ya kura?kuweni waungwana na si kywaibia na kuwafanya wananchi wajinga.bora ununue gari moja au mbili za wagonjwa kuliko kufanya wananchi wajinga kwa kuwapa baiskeli na pikipiki.nakupongeza kwa biyanda kwani nilitembelea hospitali ya mkoa mwanza watu walikuwa wanalala chini wakiwa wamefanyiwa upasuaji.

  • Cha muhimu hapa ni wananchi kuelimishwa wajue haki zao ama sivyo wataendelea kudanganywa kwa kura. Je yeye kama waziri atakubali kupelekwa hospital kwa baskeli? Kama binadamu mwenye utu na akili timamu huwezi kutoa msaada wa baskeli au pikipiki kubebea wagonjwa.

    Hata hilo gari la wagonjwa kuwa kwenye mawe ni kosa na wahusika walitakiwa wachukuliwe hatua kali kwa kuhatarisha maisha ya wagonjwa ambao wangetumia gari hilo kupelekwa hospital.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *