Nani wa kupigania haki za walemavu kwenye elimu?

Jamii Africa

Wanafunzi wenye ulemavu wa macho wa shule ya msingi Ruhila ya mkoani Ruvuma wakiwa darasani.

KUMEKUWEPO na kampeni nyingi juu ya haki za Watanzania wenye ulemavu.

Serikali imekuwa ikifanya kwa nafasi na uwezo wake, huku vyama visivyokuwa vya serikali vikitumia nguvu na fedha kupigania haki za walemavu.

Lakini pamoja na juhudi hizo, bado mahitaji ya walemavu ni makubwa.

Wapo walemavu wa macho, viungo, masikio na wote hawa wanakuwa kwenye makundi maalum yanayohitaji namna ya pekee kuwahudumia ili wapate kuishi kama kundi la watu wasiokuwa na changamoto za maungo yao.

Kwa kipindi cha muda mrefu watu wenye ulemavu wamekuwa waathirika wa matatizo mbalimbali yasiyotatuliwa kiasi cha kusababisha kukosa mahitaji yao muhimu wanayoyajitaji katika maisha yao ya kila siku.

Moja ya sehemu ambazo zimekuwa na wakati mgumu kwa watu wenye ulemavu ni sekta ya elimu.

Idadi kubwa ya walemavu hapa nchi hawakubahatika kupata elimu, idadi ya walemavu ambao hawajui kusoma ni kubwa kwani ni mara mbili ya ile ya watu wasio na ulemavu, shule za walemu nyingi hazina vifaa vya kutosha vya kujifunzia.

Inashangaza mno kubaini kuwa hata shule zinazoitwa za walemavu, hazina walimu wenye uwezo maalum wa kuhakikisha watoto wanapata elimu zzuri kulingana na mahitaji yao.

Hali hii imesababisha walemavu wengi kukosa fursa za ajira na wengine kushindwa kujua la kufanya kutokana na kukosa msaada kutoka serikalini na jamii kwa ujumla.

Hatma ya walemavu imekuwa ikihatarishwa zaidi na wengi wao kutokupelekwa shule na wengine kushindwa kuendelea na masomo kwa sababu tofauti tofauti.

Mwaka 2011 takwimu zilionesha watoto walemavu waliondikishwa kuanza darasa la kwanza ilikuwa ni asilimia 0.36 kati ya watoto wote wenye ulemavu waliofikia umri wa kwenda shule, wakati sensa 2012 ilionesha watoto wenye ulemavu walikuwa 3.5%  kati ya watoto wote.

Takwimu hizi hazikuwa na tofauti na zile za mwaka 2004 kwani watoto walemavu ambao walipata nafasi ya kuendelea na shule ilikuwa ni chini ya asilimia moja.

Kwa nyakati za sasa taasisi za watu binafsi na serikali zinapotaka kuajiri, kigezo cha elimu huwa kinapewa kipaumbele sana, lakini hawafikirii uwezekano wa baadhi ya waombaji  kuwa ni walemavu.

“Ni ngumu kukuta kwenye usaili kukuta mtaalamu wa lugha za alama ama machine za kuandikia kwa walemavu wasioona, ukiongeza kigezo cha elimu walemavu na kiwango hiki kikubwa cha walemavu kutopewa elimu, hukosa hizo nafasi na kufanya hatma yao kuwa yenye utata wanapofika umri wa kujitegemea,” anasema Khamis Kamile, mlemavu wa macho ambaye alisoma shule ya wasioona Kericho, Kenya.

Shule za msingi Buguruni Viziwi na Uhuru Mchanganyiko, ambazo FikraPevu ilipata nafasi za kuzitembelea na kuzungumza na baadhi ya walimu.

Shule hizo maalum zina mazingira mazuri ya kujifunzia na hazina tatizo la uhaba wa walimu na zina vifaa vya kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kusoma na kujifunza vyema.

Lakini bado  suala la mitaala ya elimu imekuwa haina usawa kwa walemavu, kwani ilitengenezwa kwa kutokuzingatia  hali ya walemavu.

Hili limesababisha shule hizo kuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa wanafunzi wenye ulemavu, kwa mfano, katika kipindi cha 2010-2016, wanafunzi wengi wa shule hizi wamekuwa wakipata alama za chini kulinganisha na shule za kawaida, kitu ambacho kimesababisha wengi kushindwa kuendelea na shule za sekondari za serikali.

Kwa bahati mbaya, ni ngumu kukuta shule za binafsi zinazotoa elimu kwa walemavu, lakini pia shule binafsi haziajiri walimu ambao wana ujuzi wa kufundisha wanafunzi walemavu.

Kutokana na changamto hizo, shule hizo hazipo kwenye mazingira ya kuhudumia wanafunzi wenye ulemavu, hivyo wanafunzi wengi kukosa mbadala pindi wanaposhindwa kwenda shule za serikali.

Kutokana na hali hiyo kwa wanafunzi walemavu, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, wakati akizungumza na wakuu shule huko mkoani Dodoma, alidai serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata fursa kubwa ya kujifunza vyema darasani.

Hivi sasa Tanzania ina Zaidi ya wanfunzi walwmavu katika shule za awali na msingi wanaofikia 29000.

Kitendo cha kushindwa kuhudumia ipasavyo idadi ndogo sana ya wanafunzi wenye ulemavu hasa shule ya msingi, kimesababisha wengi wao kushindwa kuendelea na masomo.

Kati ya wanafunzi wote wa sekondari, ni asilimia 0.28 tu ndiyo wenye ulemavu.

 Sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 inataka haki sawa kwa watu wenye ulemavu kwenye elimu, ajira, kuboroshewa miundombinu na nafasi za uongozi kwa walemavu.

Aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Vijana, Sera na Walemavu, Dk. Abdallah Possi, akiwa Tanga alikaririwa akisema kuwa serikali ina mkakati kamambe wa kuboresha miundombinu ya elimu na ajira kwa walemavu.

Maneno ya Dk. Possi, mwenyewe akiwa mlemavu wa ngozi, yamekuwa kama wimbo wa taifa, yakirudiwa kila mara na viongozi wa serikali, lakini hakuna mabadiliko makubwa yanayofanywa ili kuwapa urahisi walemavu kupata elimu.

Katika ajira, ni asilimia tatu tu ya wafanyakazi wa serikali ndiyo wenye ulemavu.

Idadi ndogo ya watumishi walemavu serikalini inatokana na kuwa na elimu duni au kutokujua kusoma na kuandika kabisa.

Asilimia 48 ya walemavu Tanzania hawajui kusoma wala kuandika, je, ni mwajiri gani ambaye anaweza kuajiri mtu asiyekuwa na elimu hata kidogo?

Mbali na hilo watoto wanne kati ya 10 ya watoto wenye ulemavu, walio na umri wa kwenda shule hawapelekwi shule, lakini hata hao wachache wapatao nafasi ya kwenda shule, hukumbwa na changamoto ya miundombinu, mitaala isiyo rafiki kwao na hata kuonekana binadamu tofauti na wenzao darasani.

Hivi sasa Tanzania ina shule zenye kuwahudumia walemavu 24 tu na uwepo wa vitengo 233 kwenye shule za kawaida.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) ya mwaka 2000-2015 inaonesha watoto wenye ulemavu milioni 58 hawapo shuleni duniani na watoto milioni 100 hawamalizi shule.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 160 duniani zilizosaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa mwaka 2000 kuhusu kuweka mazingira sawa ya kupatikana kwa elimu baina ya watoto wenye ulemavu na wale wasiokuwa na hali hiyo.

Hali hii inafanya hatma ya watoto wenye ulemavu kuwa yenye utata, serikali inapotunga sera ama sheria, haina budi kuweka utekelezaji kwenye uhalisia na siyo kimaandishi, kwani watoto wenye ulemavu wanaonekana kutengwa katika maeneo mengi; elimu, ajira na hata tiba.

Pamoja na upungufu kwa upande wa serikali nataasisi zngine kuwajali walemavu, wazazi wa watoto wenye walemavu washurutishwe kupeleka watoto shuleni na wawahudumie sawa na watoto wengine.

Inasikitisha kubaini kwamba ni asilimia 13 tu ya kaya zenye watoto wenye ulemavu, ni kaya asilimia moja tu ndiyo zimeweza kuwapeleka watoto wao shuleni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *