Nchi za Afrika zinahitaji madaktari mara 50 zaidi kukabiliana na vifo vya upasuaji

Jamii Africa
Dr. Wodome, graduate DESSO is doing an evisceration surgery on his project, Projet de Rehabilitation des Handicap s in Lom Togo. He is assisted by Dr. Moges Teshome (CBM coworker based in Lom ) on the left and with his medical staff

Mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye mafuta na kutofanya mazoezi umeongeza idadi ya watu wanaofanyiwa upasuaji katika nchi za Afrika na kuwaweka katika hatari ya kufariki mara mbili zaidi kutokana na uhaba wa madaktari  waliobobea kwenye taaluma ya upasuaji.

Kulingana na utafiti mpya  uliochapishwa kwenye jarida la Afya la Lancet (2018) umegundua kuwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa aina yoyote katika nchi za Afrika wana uwezekano mara mbili zaidi kufa ukilinganisha na wastani wa wagonjwa hao wanaofariki duniani.

Hali hiyo husababishwa na uhaba wa madaktari bingwa wa upasuaji ambapo nchi za Afrika na Kusini Mashariki mwa Amerika zina madaktari milioni 2.1 sawa na asilimia 12 ya madaktari  bingwa duniani. Na inakadiriwa kuwa watu 2 kati ya 3 duniani hawapati  huduma za uhakika za upasuaji.

Kutokana na changamoto hizo za kitabibu kila mwaka watu milioni 16.9 hufariki kwa maradhi yanayohitaji upasuaji na vifo hivyo hutokea zaidi katika nchi zinazoendelea. Kwa muktadha huo Afrika inahitaji madaktari mara 50 zaidi kukabiliana na vifo vya upasuaji.

 “Taarifa hizo zinaogopesha,” amesema Prof. Bruce Biccard, kiongozi mwandishi wa utafiti huo ambapo ameongeza kuwa vifo vingi vya wagonjwa  vinatokea kwasababu ya uangalizi usioridhisha wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji.

Utafiti huo ulihusisha wagonjwa 11,400 kutoka hospitali 250 zilizopo kwenye nchi  25 za Afrika zikiwemo nchi masikini zaidi za Burundi na Zimbabwe na nchi zenye uchumi wa kati kama Afrika Kusini na Ghana. Matokeo yalibaini kuwa asilimia 1% ya vifo hivyo husababishwa na maambukizi wakati wa kuuguza majeraha ambapo kiwango hicho ni kikubwa kuliko kile cha 0.5% ambacho hutokea duniani kote.

 

Idadi hiyo ya vifo huchangiwa pia kwa watu wanaofariki  kabla ya kufanyiwa upasuaji kutokana na kuchelewa kufanyiwa upasuaji na wengine kukosa kabisa huduma hiyo. Utafiti huo unaeleza kuwa  mwaka 2017 upasuaji wa watu 212 ulifanyika kati ya 100,000 ambapo idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na watu 5,000 kati ya 100,000 ambao walikuwa wanasubiri kufanyiwa upasuaji.

Prof. Biccard anaeleza  kuwa utafiti huo umeakisi hali halisi iliyopo katika nchi za Afrika na hatua za haraka zinahitajika kuokoa maisha ya watu kwa kuwapatia huduma za uhakika za upasuaji,

“Tutafute njia ambazo tunaweza kuwafunza wataalamu na kupata idadi itakayokidhi mahitaji”, ameshauri na kuongeza kuwa mafunzo hayo yahusishe wafanyakazi wengine wa afya kuliko kutegemea madaktari bingwa pekee. Kuna fursa nyingi kwa wauguzi kushirikishwa kwenye huduma za  kuwatunza wagonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji”,ameshauri Prof. Biccard.

 Matokeo hayo ni mwanzo wa utafiti mwingine ambao utafanyika 2019 ambao unalenga kutafuta njia mbadala za kuboresha huduma za upasuaji na kuwaelimisha watu juu ya kubadili mtindo wa maisha ili kujikinga na magonjwa yanayohitaji upasuaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *