Neema ya Korosho yashuka Tunduru, adha ya usafiri kukwamisha mapato ya wakulima

Jamii Africa

Licha ya msimu mpya wa ununuzi wa zao la Korosho Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma kuanza, wakulima walalamikia ubovu wa barabara na uchache wa magari ya kusafirisha korosho kwenda sokoni.

Malalamiko hayo yametolewa na wakazi wa Kijiji cha Namakambale tarafa ya Nakapanya mbele ya  Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Zuberi Homera alipotembelea kijiji hicho kuelezea msimu mpya wa ununuzi wa korosho ambao utaleta neema kwa wakulima kutokana na kuimarika kwa soko.

Wakulima hao wamemtaka Mkuu huyo wa Wilaya kutatua changamoto ya uchache wa magari ya kubebea Korosho inayosafirishwa kutoka katika Vyama vya Msingi hadi katika ghala kuu la Chama Kikuu Cha Ushirika Tunduru (TAMCU) ambalo linapatikana Tunduru Mjini.

Tunduru ni miongoni mwa Wilaya zinazozalisha kwa wingi zao la korosho nchini, lakini Wilaya hiyo inakabiliwa na ubovu wa miundombinu ya barabara hasa wakati wa mvua ambapo wakati mwingine hazipitiki kabisa.

Kutokana na hali hiyo madereva wa magari hushindwa kuyafikia maeneo mbalimbali ya wakulima ili kukusanya korosho na kuzipeleka katika ghala la Wilaya.

Suala la ubovu wa barabara na uchache wa magari linaathiri mwenendo wa soko, ambapo wakulima hutumia gharama kubwa za usafirishaji ili kuhakikisha mazao yao yanafika kwa wakati na kujipatia mapato yatakayokidhi mahitaji ya kifamilia.

Neema hiyo ya kuongezeka kwa mavuno ya korosho inaweza kugeuka kilio kwa wakulima kwasababu ya gharama kubwa zinazojitokeza tangu korosho itakapovunwa, kusafirishwa, kuhifadhiwa na kuuzwa.

Licha ya adha ya usafiri, wakulima wa korosho wanakabiliwa ushuru na makato mengi ambayo yanatozwa na serikali ikiwa ni sehemu ya kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo. Mathalani, kwa kilo moja ya korosho wanayouza wanatoa ushuru wa Halmashauri wa shilingi 50, Mchango wa Elimu sh. 50, Ushuru wa Vyama vya Ushirika (Amcos) sh. 90 na Mfuko wa Wakfu (CDTIF) sh. 10.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika Wilaya ya Tunduru (TAMCU), Hashim Twalib Mbalabala amesema zoezi la ununuzi linafanyika kwa uwazi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali kuhakikisha mkulima anafaidika na kilimo cha korosho.

“Zoezi hili linafanyika kwa uwazi ili kuondoa migogoro miongoni mwa wakulima, serikali na vyama vya msingi”, amesema Mbalabala na kuongeza kuwa makato ya ushuru na michango ya maendeleo anayokatwa mkulima yako kisheria.

Makato hayo yanaelezwa kumuumiza mkulima ambaye anawajibika kulima zao hilo na kubeba gharama zote pasipo kusaidiwa na mtu yoyote. Ukitazama makato yote hayo ni jumla ya sh. 200 ambayo hukatwa kwa kilo moja ya korosho ambapo katika msimu huu wa 2017/2018 inauzwa sh. 3,950 kwa kilo moja.

Kwa muktadha huo mkulima atabakiwa na sh. 3,750. Fedha hiyo bado haijamfikia mkulima moja kwa moja kwa sababu ya kuwepo madalali, kuongezeka kwa gharama za kuhifadhi na usafiri. Lakini bei ya soko huwa inabadilika kulingana na upatikanaji wa korosho.

Hata hivyo, machungu hayo ya wananchi wa Tunduru yanaweza yakapungua katika msimu huu mpya wa ununuzi wa korosho kutokana na kuongezeka kwa bei ikilinganishwa na msimu uliopita.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Zuberi Homera akiongea na wananchi wa kijiji cha Namakambale tarafa ya Nakapanya mkoani Ruvuma wakati akitangaza msimu mpya wa ununuzi wa korosho.

Mkuu wa Wilaya Anena

Akitangaza msimu mpya wa Korosho, Mkuu wa wilayaya Tunduru, Juma Zuberi Homera, amesema katika msimu huu 2017/2018 mnada wa kwanza umeanza kwa bei ya tsh 3,950, bei ambayo ni tofauti na bei ya 3,750 ya msimu uliopita ambayo ndio ilikuwa bei ya juu kabisa hadi kumalizika kwa msimu.

Bei hiyo imeongezeka kwa sh. 200 ambayo ni sawa na asilimia 2 ya bei ya msimu uliopita wa 2016/2017.

Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kuyashughulikia matatizo yote ya wakulima, ambapo amewataka kuichambua korosho vizuri na kuipanga katika madaraja ili ziendane na thamani halisi ya bei ya soko.

Viongozi wa vyama vya Ushirika na Vyama vya Msingi wametakiwa kujiepusha na vitendo vyote vya kuwaibia wakulima ikiwemo kuchemsha mawe ili kuongeza uzito wa kilo zinazotumika kupima uzito wa korosho.

Pia ameishukuru serikali kwa kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao umelifanya zao la korosho linalozalishwa Tunduru kukubalika katika soko la kimataifa.

“Naishukuru serikali kutoa wigo mpana kwa zao la korosho kuwa kipaumbele na pia kuruhusu wanunuzi kutoka nje ya nchi kuja kununua korosho yetu” amesema Homera.

 Kampuni zilizopata Tenda ya Kununua Korosho

Wafanyabiashara 17 waliwasilisha zabuni (Tender) za kusimamia zoezi la ununuzi wa korosho katika Wilaya hiyo, lakini waliofanikiwa kuingia katika mnada wa awali ni 14 ambapo walijumuishwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Kampuni ya Korosho ya Africa Limited ndio iliyoshinda tenda na kwa makubaliano ya TAMCU kununua tani 544 (sawa na kilo 544,000) za korosho ghafi ambayo haijasindikwa. Kilo 544,000 ambazo zimechukuliwa na kampuni hiyo ni sehemu ya kilo 544,144 ya korosho yote iliyopo ghalani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *