Nenda Twiga, nenda Afrika! Tupeni raha Watanzania

Jamii Africa

“TUTASHINDA na tutasonga mbele!” Ndivyo anavyosema kocha wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ akizungumzia ufanisi wa timu hiyo na michezo ijayo.

Kwa sasa, Twiga Stars ndiyo timu pekee tunayoweza kujivunia kwa mafanikio katika michuano ya soka ya kimataifa. Inatia moyo.

Akina dada hao, ambao Jumapili Januari 29, 2011 wanawakabili Namibia katika mechi ya marudiano ya raundi ya awali kuwania kucheza fainali kwa mara ya pili nchini Afrika mwaka huu, wameonyesha mafanikio ya kuridhika tangu walipoanza kushiriki mashindano hayo miaka 10 iliyopita.

Fainali za mwaka huu zitafanyika tena Afrika Kusini ambapo zinaweza kuondoa taswira ya ubingwa huo ambao daima umekuwa wa Nigeria baada ya kuutwaa mara nane huku Guinea ya Ikweta ikitwaa mara moja.

Katika mechi ya Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Twiga Stars wanahitaji sare ya aina yoyote ama ushindi ili kufuzu kwa raundi ya kwanza kufuatia ushindi wao wa mabao 2-0 ugenini wiki mbili zilizopita.

Ikiwa inaingia kucheza mechi yake ya 23 ya mashindano hayo tangu mwaka 2002 ilipoanza kushiriki, Twiga Stars inahitaji kuungwa mkono kwani imeonyesha mafanikio makubwa katika soka la wanawake tofauti na wenzao wanaume ambao wameathiriwa na ‘football fitna’ kwa miaka zaidi ya 30 sasa.

Kwa timu ambayo imekuwa haipewi msaada wowote wakati wa maandalizi na kulazimika kutembeza bakuli hata baada ya matokeo mazuri, ni dhahiri inahitaji sapoti ya Watanzania kwa sababu mafanikio yake yako dhahiri.

Takwimu zinaonyesha kwamba, tangu mwaka 2002 timu hiyo imekwishacheza mechi 22, ambapo imeshinda mechi saba na kufungwa 11, huku yenyewe ikipachika wavuni mabao 35 na kufungwa 50 katika mechi hizo!

Huwezi kuyalinganisha mafanikio haya na timu ya wanaume, Taifa Stars, ambayo pamoja na ukweli kwamba viwango vya uchezaji kwa akina dada na wanaume ni tofauti, lakini imekuwa ‘jamvi la wageni’ katika michuano hiyo ya Afrika ikifungwa hata na timu vibonde.

Ni miaka miwili iliyopita tu wakati timu hiyo ilipofanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za mashindano hayo nchini Afrika Kusini, ambapo licha ya kupoteza mechi zake zote tatu kwenye Kundi A ikifungwa mabao 8 na yenyewe ikipachika matatu, bado ilikuwa imefika mahali ambako Taifa Stars imekuwa ikifurukuta bila mafanikio kwa miaka mingi.

Kwa soka ya wanawake ambayo ilianza kucheza mwanzoni mwa miaka ya 1990 hapa nchini kufuatia kuanzishwa kwa klabu ya Sayari, huwezi kulaumu sana matokeo ya akina dada hao ambao maandalizi yao daima ni ya zimamoto huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likitilia zaidi mkazo timu za wanaume kwa kuangalia mapato yatokanayo na mechi hizo kubwa.

Kocha wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa (pichani), anasema kwamba pamoja na mazingira magumu ya maandalizi yao, lakini anawahimiza wachezaji wake kujituma ili wapate matokeo bora zaidi, katika mechi ya Jumapili na hata zijazo.

Charles Boniface Mkwasa, Kocha Mkuu wa Twiga Stars

Anatambua kwamba, timu yake ikiitoa Namibia itakumbana na ama Misri au Ethiopia katika raundi ya kwanza. Misri iliifunga Ethiopia mabao 4-2 Januari 14 jijini Cairo, lakini Ethiopia inaweza kugeuza matokeo nyumbani na kusonga mbele.

Wakikutana na Ethiopia haitakuwa mara ya kwanza, kwani Twiga Stars iliwahi kucheza na timu hiyo katika raundi ya awali 2010 na kuifunga 3-1 jijini Addis Ababa kabla ya kutoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam.

“Hatuangalii tunacheza na timu gani, sisi tunakazana kwenye mazoezi tu japo tunafanya maandalizi katika mazingira magumu.

“Nimewaeleza wachezaji wangu kwamba, pamoja na kuifunga Namibia katika mchezo wa kwanza, sisi tucheze kwa bidii ili tupate matokeo mazuri zaidi. Kila mechi kwetu ni mpya na tunaamini tutafanya vizuri zaidi,” anasema Mkwasa.

Alhamisi Januari 26, 2011 timu hiyo ilipata afueni baada ya kukabidhiwa kitita cha Sh. 10 milioni kilichochangwa na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kulipa posho za wachezaji pamoja na kusaidia maandalizi.

Mbali ya hivyo, wabunge hao waliahidi kununua bao la kwanza la Twiga Stars kwa Sh. milioni moja ikiwa wataanza kuifunga Namibia, ahadi inayowapa hamasa wachezaji wa timu hiyo.

Tangu irudi kutoka Windhoek na ushindi huo, timu hiyo haijapatiwa mechi zozote za kujipima nguvu zaidi ya kucheza na timu za mitaani.

Nahodha wa Twiga Stars, Sofia Mwasikili anasema wamejiandaa vyema kukabiliana na Namibia na akawataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kuwaunga mkono.

“Timu yetu iko vizuri, tumejiandaa vyema japokuwa katika mazingira magumu, kama unavyojua siku zote. Lakini nawaomba wapenzi wa kandanda waje kwa wingi kutushangilia, tutashinda na kusonga mbele,” anasema.

 

Kikosi cha Twiga Stars Jumapili kinaweza kuwakilishwa na: Fatuma Omary,

Rais Jakaya Kikwete akiwa na wachezaji wa Twiga Stars Ikulu, Dar es Salaam. Rais Kikwete atafarijika kuona timu hii inashinda na kusonga mbele.

Fatuma Bushiri, Prukeria Chalagi, Fatuma Hatib ‘Foe’, Sophia Mwasikili (nahodha), Mwapewa Mtumwa, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Eto Mlenzi, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Fatuma Mustapha.

Kiingilio cha chini katika mechi hiyo ni Sh 2,000 kwa viti vya bluu na kijani, watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 Sh 1,000, kwa viti vya rangi ya chungwa Sh 3,000, VIP B na C Sh 5,000 na Sh 10,000 kwa VIP A.

Namibia imewasili Ijumaa (Januari 27 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ndege ya South African Airways.

 

Msimamo wa Twiga Afrika tangu ilipoanza kushiriki mwaka 2002:

 

P       W       D       L        Gf      Ga

22     7       4       11     35     50

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *