Ni wakati sahihi kwa wanaume kutumia vidonge vya uzazi wa mpango?

Jamii Africa

Kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa wakiwajibika kutumia njia za uzazi wa mpango kuzuia mimba zisizo tarajiwa. Wengine wanatumia njia za muda mrefu kama vipandikizi, kukata mirija ya inayosafirisha mayai ya uzazi.

Lakini wengine wanatumia vidonge, sindano na kondomu za kike. Wanaume nao wana njia mbili  yaani kutumia kondomu au upasuaji na kuziba mirija inayosafirisha manii kwenda kwa mwanamke. Kimsingi mwanamke anabeba jukumu kubwa la  kufahamu wakati sahihi wa kupata ujauzito na idadi watoto anaowataka.

Kwa karne nyingi sasa hazijavumbuliwa njia mpya za uzazi wa mpango kwa wanaume. Lakini huenda hali hiyo ikabadilika kutokana na majaribio ambayo wanasayansi wanafanya ili kuongeza njia za uzazi wa mpango kwa wanaume. Lengo kuu ni kuleta usawa katika matumizi ya njia za uzazi kwa wanaume na wanawake.

Wanasayansi wanaamini kuwa ni wakati muafaka wa kubadili hali iliyopo na tayari wameanza kufanya majaribio ya njia mbalimbali ikiwemo vidonge na mafuta ambayo wanaume watatumia kuzuia mimba kwa wanawake.

 

Majaribio yaliyofanyika kwa wanaume

Tafiti zinaeleza kuwa takribani asilimia 50 ya wanaume watatumia njia mpya za uzazi , na walio kwenye ndoa wanakusudia kutumia zaidi njia ya vidonge. Baadhi ya wanasayansi wanafanya majaribio  ili kuangalia namna wanavyoweza kuzuia homoni ya ‘testosterone’ na uzalishaji wa mbegu za kiume bila kuathiri afya ya mwanaume.

Wanasayansi  nchini India wamefanikiwa kutengeneza dawa ya sindano ambayo inazuia mbegu za kiume kutoka kwenye korodani lakini wanasubiri ruhusa ya serikali ili waanze kusambaza kwa watu.

Hivi karibuni, wanasayansi nchini Marekani waliifanyia majaribio dawa  iitwayo ‘dimethandrolone undecanoate’ (DMAU) kwa kuwapa vidonge wanaume 83, ambavyo vinazuia na kudhoofisha hamoni ya ‘testosterone’ inayoitajika katika uzalishaji wa mbegu.

Utafiti huo mdogo ulibaini kuwa ikiwa kidonge kimoja kitatumika kila siku kitasaidia kupunguza uzalishaji wa mbegu za kiume na matokeo yake mwanaume hawezi kumpa mwanamke mimba.

Mkazi wa jimbo la Califonia, Kristoffer Thordarson ambaye alishiriki kwenye utafiti huo amesema ujio wa njia za uzazi hasa vidonge vitasaidia wanaume kuwa sehemu muhimu ya kuzuia mimba zisizotarajiwa.

“Nafikiri wanaume na wanawake wakiwajibika kuzuia mimba zisizotarajiwa itasaidia kuondokana na dhana ya kuwachukia na kuwatenga wanawake,” amesema  Thordarson.

Hata hivyo, watafiti wanaendelea kuchunguza madhara ya kiafya ambayo yanaweza kutokea endapo mwanaume atatumia vidonge au sindano za uzazi wa mpango.

                            Sindano ni njia mojawapo ya njia ya uzazi wa mpango kwa wanaume

 

Pia Taasisi ya Taifa ya Afya (NIH) ya nchini Marekani kwa kushirikiana na vyuo mbalimbali duniani, wanapanga kuanza majaribio makubwa ya njia za uzazi wa mapango kwa wanaume ambapo yatahusisha mafuta maalum.

Utafiti uliopo nyuma ya njia ya mafuta ni kwamba yanatembea haraka kuliko vidonge ikiwa yatapitia kinywani yatadhoofisha homoni ya testosterone kwa haraka. Watafiti wa NIH wanaeleza kuwa ikiwa mafuta hayo yatapakwa kwenye ngozi yatapenya haraka na kukaa kwenye mishipa ya damu kwa muda mrefu kuliko vidonge.

Majaribio ya mafuta hayo yatahusisha wanaume 400 walio katika ndoa kutoka nchi 6, na watapaka mafuta hayo kwenye mabega ya mikono yote miwili mara moja kwa siku. Mafuta hayo yana mchanganyiko wa kemikali za ‘nestorone’ ambazo zinazuia korodani kuzalisha mbegu za kutosha na kuhakikisha kunakuwa na msawazo mzuri wa homoni mwilini.

Baada ya mbegu za wanaume hao kufika kiwango cha chini cha uzalishaji, wanaume na wake zao wataamua kutumia mafuta hayo kama njia mbadala ya uzazi wa mpango. Tayari wameanza usajili wa watu ambao watakuwa sehemu ya utafiti huo.

Changamoto iliyopo kwenye matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa wanaume ni kwamba zinahusisha mchakato mrefu. Njia za kuzuia mimba kwa wanawake zinafanya kazi zaidi kuzuia uchavushaji wa yai moja mara moja kwa mwezi. Lakini mwanaume anazalisha mbegu nyingi kila siku, na kuzizuia zisizalishwe kunahitaji umakini mkubwa wa majaribio, homoni, ratiba ya kuzitumia njia hizo.

Daniel Dudley (28) ambaye anashiriki katika utafiti wa njia za uzazi kwa wanaume anasema, “Nafikiri utafiti unaendelea, wanaume wengi watafunguka hasa wale wanaopendelea haki za kijamii au wanaopenda kuwasaidia wenza wao wa kike,” amesema Dudley.

“Jamii yetu inasonga mbele zaidi kuelekea kwenye usawa wa kijinsia katika maeneo mbalimbali,” amesema Dudley na kuongeza kuwa, “Hii ni hatua isiyopingika”.

 

Kulingana na taasisi ya Viashiria vya Soko la Dunia (Global Market Insights), ikiwa njia za uzazi kwa wanaume zitapitishwa na kukubalika kwa miaka mitano ijayo, inakadiriwa soko lake litategeneza faida ya Dola za Marekani bilioni 1 ifikapo 2024.

 

Kwanini  njia za kuzuia mimba kwa wanaume

Tangu kuanza kutumika kwa njia za uzazi wa mpango kwa wanawake mwaka 1960, hakujasaidia kutatua tatizo la dunia la mimba zisizotarajiwa. Tafiti mbalimbali zimekuwa zikipendekeza wanawake kutumia kujaribu njia mbalimbali za uzazi kabla ya kuamua kubaki na njia moja ambayo inafanya kazi kwa ufanisi kulingana na mahitaji ya miili yao.

Licha ya jitihada mbalimbali za serikali na wadau wa afya ya mama na mtoto kuhamasisha matumizi ya njia sahihi za uzazi wa mpango, bado idadi ya wanawake wanaotoa mimba ni kubwa nchini Tanzania. Wanawake 390,000, kati ya milioni moja, nchini Tanzania hutoa mimba kila mwaka kwa njia za kienyeji.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikishirikiana na Taasisi ya Guttmacher na Chuo Kikuu cha Muhimbili mwaka 2015 inathibitisha kuwa “Tanzania ni kati ya nchi zenye viwango vya juu vya wanawake wanaotoa mimba kwa njia zisizo salama”.

Utafiti huo unaeleza kuwa, Mwaka 2013 pekee, wanawake 6 kati ya 10 wenye mimba zisizotarajiwa katika Nyanda za Juu Kusini waliishia kuzitoa kwa njia za kienyeji na baadhi waliripoti hospitali kupata matibabu baada ya kupata matatizo ya kiafya.

Adrienne Ton (25) binti  anayesomea kozi ya Uuguzi katika Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani anasema wanawake wanabeba mzigo mkubwa wa maamuzi ya kupata mimba na wakati mwingine hushindwa kujizuia.

“Wanawake wanatumika kubeba huo mzigo, na jamii inamini kuwa ni wajibu wetu,” amesema. “Lakini nafikiri tunahitaji ulinzi zaidi”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *