Ofisa Usalama wa Taifa auwawa kwa kuchinjwa kinyama Mbeya

Jamii Africa

AFISA Usalama wa Taifa mstaafu wa mkoani Mbeya Joseph Mwasokwa (76) amekufa baada ya kuchinjwa nje ya nyumba yake eneo la Block T , Mbeya mjini.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia siku ya Uhuru wa Tanganyika, Disemba 9, 2012, baada ya mwili wake kugundulika  saa 12.45 Asubuhi.

Akisimulia mkasa huo, mtoto wa kiume wa marehemu Mwasokwa, Mpoki Mwasokwa (37), amesema kuwa Baba yake aliondoka nyumbani siku ya Jumamosi Desemba 8, mwaka huu kwenda kuangalia mpira ligi ya Uingereza.

Alisema alipokuwa akiondoka alimuaga na kumsihi kuwa asiondoke na gari bali aliingize ndani kwasababu hakukuwa na mafuta ya kutosha.

"Baada ya hapo hatukumuona mpaka nilipokuja kuambiwa na mama kuwa kulikuwa na mtu ameuawa nje ya geti letu,’’ alisema Mpoki.

Aliendelea kusimulia kuwa Mama yake alimpa taarifa kuwa kuna binti alienda nyumbani hapo kwa ajili ya kununua mahitaji ya nyumbani katika kiosk kilichopo nyumbani hapo na kuukuta mwili wa marehemu nje na kutoa taarifa kwa mama yake.

"Mama alienda katika chumba anacholala Baba hakumkuta ndipo akaja na kuniambia kuwa kuna mtu ameuawa nje ya nyumba yetu na tulipotoka nilipojaribu kuugeuza mwili ule kwa mguu nikagundua kuwa ni Baba ambapo mwili wake ulikuwa na majeraha ya kukatwa katwa,’’ alisema mtoto huyo wa marehemu.

Ametanabaisha kuwa alimkuta baba yake yupo kifudifudi huku mwili wake na ardhini kukiwa kumetapakaa damu na wakachukua hatua ya kuwapigia Polisi na Polisi walipofika na kumpekua waliukuta mwili huo ukiwa na pesa Dola za kimarekani 200 na Shilingi za Kitanzania 110,000/= na simu ya kiganjani.

Alisema mwili wa marehemu utasafirishwa siku ya Jumanne Disemba 11, mwaka huu kwenda wilayani Kyela mkoani hapa kwa ajili ya mazishi. Marehemu ameacha mjane na watoto saba.

Habari hii imeandikwa na mwandishi wa FikraPevu, Mbeya

1 Comment
  • Hakika Tanzania si salama na wanajidanganya kwa kawimbo ka amani na utulivu vinafanya Tanzania kisiwa cha Amani, waendelee kujidanganya!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *