Polisi warudisha maiti walopora, washitaki viongozi wa Chadema

Jamii Africa

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya Mkoani Mara kupora mwili wa marehemu, Mgosi Magasi Chacha (30), aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi wanaolinda mgodi wa North Mara wilayani humo, polisi wameelezwa kuupeleka mwili wa marehemu nyumbani kwao na kuwageuzia kibao viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU)

Imeelezwa kwamba polisi wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa kwenye magari yapatayo manne wakiwa na silaha  zikiwamo bunduki aina ya SMG, mabomu ya machozi na marungu, waliutekeleza mwili huo baada ya kuufikisha nyumbani kwao kutoka chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya hiyo, ambapo waliutoa kwa nguvu na kuusafirisha chini ya ulinzi mkali.

Wakati hayo yakijiri, polisi wamewafikisha mahakamani, viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wilaya ya Tarime, kwa tuhuma za kufanya fujo na kuchochea ndugu na jamaa wa marehemu Chacha wasichukue mwili huo kutoka Mochwari.

Viongozi hao wa Chadema waliofikishwa katika mahakama ya Mwanzo ya wilaya hiyo ni Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Tarime, Lucas Ngoto, Katibu wake, Mroni Mwita pamoja na Diwani wa Kata ya Sabasaba, Christopher Chometa (Chadema), lakini wamedhaminiwa na kesi yao Na. 239/2012 itatajwa tena Juni 12 mwaka huu.

Taarifa zilizopatikana kutoka nyumbani kwa marehemu Chacha, zimelaani kitendo cha polisi kuutoa kwa nguvu hospitalini mwili wa ndugu yao huyo, na kwamba baada ya polisi kuufikisha nyumbani waliushusha ndani ya gari kisha kuutelekeza.

Marehemu Chacha aliuawa Jumanne Juni 4, 2012 saa 1:45 asubuhi, ambapo ulimaliza siku mbili akiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti, na kwamba siku ya tatu polisi waliutoa kwa nguvu kisha kuupeleka nyumbani kwao Kijiji cha Nkende, ambapo inadaiwa ulitelekezwa na kuachwa bila kuzikwa, kutokana na familia hiyo kutokukamilisha taratibu za maziko.

Mmoja wa wanafamilia (jina tunalihifadhi), aliiambia FikraPevu leo kwamba, mara baada ya polisi kuupeleka mwili wa ndugu yao huyo, askari wote waliondoka na kwamba marehemu huyo hakuzikwa siku hiyo kutokana na taratibu za mazishi kutokukamilika.

“Walikuja polisi wakauweka mwili wa marehemu kisha wakaondoka wote na magari yao kwa mbio. Huu ni unyama kabisa wanafanya polisi. Tarime tumekuwa watumwa kwa sababu tupo karibu na mgodi wa Mzungu.

“Hatukumzika ndugu yetu siku hiyo kwa sababu familia ilikuwa haijakamilisha taratibu za mazishi. Tunatarajia tumzike leo, maana”, alisema kisha akaanza kulia kwa uchungu.

Baadhi wakazi wa wilaya ya Tarime, wameitaka Serikali kuufunga mgodi huo wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick, kwa madai kwamba uwepo wa mgodi huo umekuwa chanzo cha watu wengi kuuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi waliopewa dhamana ya kulinda usalama mgodini hapo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi na jana, baadhi ya wakazi hao wa Tarime walisema: “Ni heri huu mgodi ufungwe, maana watu wanauawa ovyo kama wanyama. Polisi wameshindwa kulinda usalama wa raia na mali zao, badala yake wamegeuka kama wapo Darfu kwa kuua raia wasio na hatia”.

Kwa mujibu wa wananchi hao ambao majina yao tumeyahifadhi, mgodi huo umekuwa ukisababisha raia wengi kuuawa kwa kupigwa risasi, na kwamba wanataka kuona Serikali inaufunga mgodi huo wa dhahabu ili kunusuru maisha ya wakazi hao.

Wananchi hao walikwenda mbali zaidi na kusema, wananchi wa Nyamongo wamekuwa wakiishi kwa shida kubwa, kwani usiku milio ya risasi ya bunduki husikika kila siku, hivyo wameanza kuishi kwa woga kama watumwa ndani ya nchi yao.

Juzi mke wa marehemu Chacha alilazimika kukaa kwenye mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti, kwa lengo la kutaka kuzuia polisi wasiuchukua mwili wa mumewe bila ndugu na yeye kuridhia, jambo ambalo polisi walimburuza kwa nguvu kiasi cha kusababisha baadhi ya nguo za mwanamke huyo aliyekuwa akilia kwa sauti na uchungu kudondoka na kumwacha wazi baadhi ya sehemu za maeneo ya mwili wake, jambo ambalo lilionekana kama ni udhalilishaji mkubwa.

Katika vurugu hizo, polisi walifanikiwa kuuchukua mwili huo wa marehemu Chacha na kuuondoa hospitalini ukiwa umepakiwa kwenye gari la Halmashauri ya Mji wa Tarime lenye namba SM 5241, huku likisindikizwa na askari hao wa FFU waliokuwa na silaha za SMG, wakitumia magari yenye namba PT 2036, PT 1873, PT 1863, T 754 BLF, pamoja na pikipiki moja ya doria.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi Kanda hiyo Maalumu ya Tarime na Rorya, Sebastian Zacharia, hakupatikana mara moja kuzungumzia tukio hilo.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Tarime.

9 Comments
  • jaman hivi hii nchi inakwenda wapi?mbona hatuthaminiwi kabisa na serikali iliyopo madarakani?kwa unyama huo unaofanyika maisha bora yenye usawa kwa kila mtanzania yako wapi?siku watanzania tukisema imetosha!tutapigana kwa faida ya watoto wetu hata mkituua na nyie mtahukumiwa kwa kichozi litakalomwagika.anza kujipanga sasa kwa mapinduzi 2015.

  • hayo ndio matunda ya kutotii sheria bila shuruti kama wangekua waelewa wasingeshindana na polisi wasubiri waiazibu serekali yao kwenye masanduku ya kura 2015.

  • Tunakuwa wakimbizi katika nchi wenyewe, lakini matukio kama haya yateendelea kutukumbusha watanzania kuwa kuna haja kubwa saana ya kufanya mabadiliko. Tutakapo kuwa na uongozi ambao tumeuchagua sisi wenyewe, tutakuwa na uwezo na mamlaka ya kuuwajibisha. Lakini hawa waliopata uongozi kwa kwa kupewa na tume ya uchaguzi matokeo yake ndo kama haya.

  • Hii ni habari ya kuhuzunisha sana! nashindwa kuelewa uongozi wa nchi hii unapeleka wapi?? hivi ni kweli polisi hawaelewi kwamba vitendo kama hivo ni hatari sana kwa ustawi na usalama wa taifa?? au ndo kutii na kufuata matakwa ya watawala??

    Polisi wao watadai wanafanya kazi yao lakini sio kweli hata kidogo kazi bila kufikiria kwa kweli watawala na polisi msipogeuka na kufuata utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu sio tu kwamba mnajichimbia kabuli ila mnamwaga mafuta amabayo yanasubiria kuwashwa na hapo kutakuwa hakuna cha mwanaccm, mwanachadema cuf wala mwekezaji sote tutaungua!!

  • Kiukweli inatia uchungu kuwaabudu wazungu waliovaa ngozi ya uwekezaji hata kwenye nchi yetu.uhuru wetu upo wapi?faida za rasilimali zetu zipo wapi?ni nini maana ya kuendelea kujiita kisiwa cha amani ilihali watu wanakufa?ccm kwanini mnatufanyia hivyo?tuliwaamini ila imani yangu tena sio kwenu hata mfanye mabadiliko kila siku.TUMEWACHOKA TUACHIENI NCHI YETU

  • kesi hyo ilipelekwa mahakama ya wilaya baada ya makada wa chama hicho kukataa kesi hyo kupelekwa mahakama ya mwanzo,kwani mahakama ya mwanzo ndio inaongoza kwa unyanyasaji wa haki za raia hususan wanachadema kwan mahakama inaendeshwa kibabe na kisiasa sana huku hakimu mkaz wa mahakama hyo samwel gimeno akitoa lugha za matusi mahakaman bila ya kujari dhamana alyonayo,pia aktoa maneno ya kudhihak wana cdm,na hata kipindi viongoz hao wa cdm waliposomewa shtaka na kukana.

    Mwendesha mashtaka anayeitwa kazen, alisimama kupinga maombi ya dhamana kwa visingzio alvyotoa kichwan mwake ya kwamba anaomba waspewe dhamana kwan kupewa kwao dhamana kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani mjini hapa, ndipo hakimu akakubariana na hoja za pande zote mbili ila maamzi yatatolewa tarehe 12/6 baada ya hapa ndipo baadhi ya viongoz wa kipolic mkoa na wilaya kutofurahshwa na kitendo hicho ilibidi waombe mahakama kuwapatia dhamana viongoz hao.

  • Jeshi la police Tanzania Lina roho mbaya sana, limetawaliwa na Chama tawala. Kila kitu kina mwanzo na mwisho, mwisho utafika siku moja.

  • Wazungu wamekuwa kama Mungu mtu bongo hii!! ila kila marefu ya ncha yake, tunasubiri siku tu ifike hata wakija na mab52 haitasaidia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *