Polisi yawahoji watumishi wa idara ya ardhi Jijini Mwanza

Jamii Africa

MWANZA IJUMAA APRILI 6, 2012:  HATAMAYE  Jeshi la   Polisi  mkoani hapa limeanza kuwakamata na kuwahoji  watumishi  wa idara ya ardhi katika halmashauri ya jiji la Mwanza; ili  siku yoyote wapandishwe kizimbani  kujibu  tuhuma  za kukaidi  amri  ya Baraza la Ardhi na Nyumba.
RPC Mwanza Liberatus Barlow
Watumishi hao ni sehemu ya watuhumiwa  wengine zaidi ya kumi  ambao
inadaiwa kwamba Novemba 23 mwaka jana katika mtaa  wa Pasiansi Mashariki jijini hapa wakiwa  na nyundo pamoja na mapanga  walivamia na kuvunja nyumba  ya mjane mmoja, Moshi  Mzungu(67) ambayo ipo katika kiwanja ambacho mgogoro  wake ulikuwa  haujafikiwa  maamuzi mahakamani.

Hata  hivyo, watumishi  hao wamehojiwa huku  mtumishi  mwenzao ( katika idara hiyo), Asubuhi Otieno,  akiwa nje  kwa dhamana  baada ya kutiwa  hatiani  mwezi uliopita  kwa kosa la kuwasilisha ushahidi wa uongo mahakamani.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya jeshi la  Polisi  jijini hapa kimeliambia  FikraPevu  kwamba  tayari polisi limeshawahoji watumishi 5 kati ya 7   ambao Februari  mwaka  huu  walipatikana na kosa la kupuuza  amri  ya Baraza la Ardhi na Nyumba.

Waliohojiwa  wametajwa  kwamba ni  Victor  Mashamba, Kitia Kagoroba, Abdon Baraka pamoja na  Lazaro Matulanya  ambaye  alikuwa dereva  wa gari pamoja na mfanyakazi mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Kassim.

Habari zinadai watuhumiwa wengine  wawili (Mwita  Wambura pamoja na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mwita)  wanatarajiwa kukamatwa na kuhojiwa  wakati wowote.

Watuhumiwa  hao wamekamatwa  ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa barua
yenye   kumbukumbu namba DLHT/NZ/APP  namba 244/2010; barua ya Februali 17 mwaka huu ambayo iliandikwa na kusainiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba mkoa  wa Mwanza, Christian  Mwashambwa.

Inadaiwa  kwamba barua hiyo iliyotumwa kwenda kwa Mkuu  wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai  wa Mkoa(RCO) wa Mwanza (Fikra Pevu  limepata nakala yake) inasema kwamba kwa makusudi  watuhumiwa hao  walitumia vibaya ofisi  za umma pamoja na mali za umma katika kutekeleza azima zao ovu.

Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na Kamanda wa  Polisi mkoani hapa, Liberatus  Barlow, zinasema   kwamba watu hao  walihojiwa  kwa nyakati na siku tofauti mwezi uliopita.

“ Siyo kwamba polisi  tumekaa kimya  ama tunawaogopa  watumishi  wenzetu wa serikali  walioamriwa kukamatwa kutoka ofisi za halmashauri ya Jiji la Mwanza; hapana, kazi imeanza  na tayari watano wao wameshahojiwa,” kilidai chanzo chetu cha habari kwa sharti la kutotajwa jina.

Hata hivyo, inadaiwa   kuwa zoezi la kuwakamata  watuhumiwa  hao limechelewa  kutokana na kughubikwa na mizengwe  kutoka kwa  baadhi ya wanasiasa pamoja na  maafisa kadhaa wa polisi  mkoani hapa ambao  wamekuwa  wakiwakingia  kifua watuhumiwa hao.

Kwa  mujibu wa habari,  askari hao  wanaodaiwa kutokuwa  waaminifu waliwasilisha taarifa  zilizokuwa  zikipingana na amri  ya Baraza  la Ardhi na Nyumba mkoani hapa.

“Mimi nilishatoa   maelekezo  kwa RCO ( Mkuu  wa Upelelezi wa Jinai wa Mkoa) ili watuhumiwa hao  wakamatwe  na kuhojiwa  na kisha wafikishwe mahakamani kwa mujibu   wa taratibu na sheria  za nchi,” alithibitisha Kamanda wa Polisi  Mkoani hapa, Liberatus  Barlow.

Kamanda  huyo  alisema ofisi yake  inaheshimu  sheria za nchi na kwamba  haifanyi kazi kwa kushinikizwa na wanasiasa  wala watendaji wengine serikalini.

Amri  ya kuwakamata  watumishi hao pamoja  na watu wengine waliohusika katika kubomoa nyumba  namba  410 iliyoko Kitalu L  Pasiansi Mashariki B ilitolewa  Februali mwaka huu.

Imeandaliwa na Juma  Ng’oko,  Mwanza

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *