Prof. Kabudi atoa ufafanuzi wa mgawanyo wa faida ya 50/50 kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania.

Jamii Africa
IKULU, DAR: Kampuni ya Barrick imekubali kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 300 kwa ajili ya kukuza Uaminifu wa biashara. . Pia, Serikali imesema Kampuni ya Barrick Gold Mine imekubali kujenga Maabara na Kiwanda cha kuchakata Makinikia nchini. Katika majadiliano hayo Kampuni hiyo pia imekubaliana na masharti yote yaliyoko kwenye sheria mpya ya madini #JFLeo

Ikiwa imepita siku moja baada ya serikali na Kampuni ya madini ya dhahabu ya Barrick kukubaliana kugawana faida ya 50 kwa 50, Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Balamagamba Kabudi amejitokeza kutoa ufafanuzi kwa wananchi juu ya makubaliano hayo.

Taarifa hiyo ilitolewa na serikali jana na kuzua mijadala ya wananchi katika majukwaa mbalimbali  ambapo watu wanahoji inawezekanaje Tanzania kupata mgao sawa na Barrick ikizingatiwa kuwa ina hisa ndogo za asilimia 16.

Kwa mujibu wa Barrick walisema wameamua kukubaliana na serikali ya Tanzania kuilipa Bilioni 700 wakati wakiendelea na mazungumzo ambayo hayajafika tamati.

Prof. Kabudi ametoa ufafanuzio huo leo akisema kuwa suala hilo halijaeleweka kwa baadhi ya watu na ametaka waelewe kuwa makubaliano hayo ni ya kihistoria na yana tija kwa taifa.

“Ningependa kufafanua kuhusu makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya Madini ya Dhahabu ya Barrick, na hasa kuhusu swala zima la mgao wa faida wa 50/50. Jambo limekuwa gumu na kwa watu wengine halifahamiki vizuri”,

“Serikali itapata 16% ya hisa ambazo zinapatikana bila malipo yaani free credit interest kwa mujibu wa sheria ya madini kama ilivyobadilishwa. Kwa maana hiyo basi, Barrick wanabaki na asilimia 84% ya hisa”, amesema Prof. Kabudi.

Ameeleza kuwa serikali itapata faida ya asilimia 50 baada ya kampuni ya Barrick kulipa kodi zote na faida hiyo haitahusisha mapato ambayo yako kisheria ambayo kampuni hiyo inapaswa kulipa kwa serikali. Kwa muktadha huo serikali itapata asilimia 70 ya kodi na faida ya mgawo.

“Mapato ya kodi ambayo serikali inayachukua kisheria hayahesabiwi kwenye mgao wa faida wa 50/50. Ile faida iliyosalia baada ya kampuni kulipa kodi zote ndicho kinachogawanywa na serikali 50/50.

Kwa maana hiyo basi, ukijumlisha kodi zote zilizolipwa kabla ya kugawana kwa 50/50 hapo serikali na Watanzania wanakuwa hawapati mgao wa faida wa 50/50 bali wanapata 70/30”, amesema Kabudi na kusisitiza kuwa,

“Kwa hiyo ningependa hilo lieleweke wazi kabisa kwamba tulihakikisha kwamba yale mapato stahili ya serikali yanabaki pale pale kama yalivyo ndani ya sheria na kinachokuja kugawanywa 50/50 ni kile kilichobaki baada ya kodi zote na ushuru wote wa serikali kulipwa”.

Kwa mujibu wa Waziri huyo anasema katika majadiliano na Barrick walivutana sana kuhusu utaratibu wa kupata 50/50 ambao unapatikana nje ya kodi inayotozwa. Kampuni ya Barrick imekuwa ikitumia utaratibu huo katika nchi ambako imewekeza lakini faida ya 50/50 imekuwa ikijumuisha na kodi inayotozwa na serikali za nchi husika.

“Kampuni ya Barrick inatumia mgawanyo wa faida wa 50/50 nchini Dominika, Saudi Arabia na Argentina. Lakini mgawanyo wa faida wa 50/50 wa nchi za Dominika, Saudi Arabia na Argentina unajumlisha pamoja na kodi ambazo serikali inazikusanya ila sisi kipengele hicho tulikikataa na ilikuwa ni moja kati ya mambo ambayo yalikuwa na mvutano mkubwa wakisema kwa nini Tanzania tunataka tuwe tofauti na nchi za Dominika, Argentina na Saudi Arabia”.

Anasema kwa Tanzania tuna kila sababu ya kusema tumepiga hatua kuliko wale ambao walitutangulia katika suala hili.

Rais John Magufuli akishuhudia kuwekwa saini kwa makubaliano kati ya serikali

na Kampuni ya madini ya Dhahabu ya Barrick

 

 

Katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Barrick na Serikali haya ni baadhi ya makubaliano yaliyoafikiwa baina ya pande zote mbili;

1. Kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata makinikia nchini

3.  Wafanyakazi wazawa hawatakaa mgodini lakini barabara itajengwa ili waishi Mwanza

3. Kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yanayozunguka mgodi

4. Kesi na mashauriano yote yatafanyika Tanzania

5. Barrick wamekubali kulipa bilioni 700 wakati mazungumzo ya fidia yakiendelea

6. Serikali kuwa na hisa ya asilimia 16 katika kila mgodi

7. Migodi yote itaweka fedha zake zote za madini katika akaunti za benki zilizopo nchini

8. Ofisi za Barrick zilizopo London na Johannesburg zitahamia Mwanza

9. Kuanzishwa kwa kampuni mpya ya kusimamia na kuendesha migodi

10. Mgawanyo wa faida utakuwa nusu kwa nusu

11. Sehemu kubwa ya kazi za huduma migodini zitafanywa na kampuni za kitanzania.

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *