GAVANA wa Benki kuu ya Tanzania (BoT)Prof Benno Ndulu, amezungumzia ubora wa noti mpya zilizotolewa hivi karibuni na kukanusha taarifa za kuibiwa kwa sehemu ya noti hizo zilipowasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo, Gavana Ndulu amesema noti mpya zina ubora na viwango vya kimataifa.
Akifuatana na wataalamu wake wa ndani na mmoja kutoka kampuni iliyotengeneza noti hizo, Gavana Ndulu aliwahakikishia Watanzania kwamba hawatapata hasara na wala uchumi hautaathiriwa na noti mpya zilizotolewa hivi karibuni.
Mtaalamu huyo kutoka kampuni ya Crane Currency ya Sweden, Peter Brown, alitoa mifano ya noti mbalimbali ikiwamo Dola za Marekani zilivyo na ubora unaofanana na noti mpya za Tanzania katika ubora.
Taarifa kamili ya BoT ni kama ifuatavyo:
1. Mwezi Januari 2011 Benki Kuu ya Tanzania ilitoa toleo jipya la noti za Shilingi 500, 1000, 2000, 5,000 na 10,000. Baada ya kipindi cha takriban mwezi mmoja sasa, pamejitokeza dukuduku na maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi. Kwa kuwa ni maswali ambayo yakijibiwa yatasaidia kuelimisha jamii katika ufahamu wa noti hizi tumeona ni vyema tukayajibu kupitia kwenu.
2. Maswali yaliyopokelewa au kuandikwa katika vyombo vya habari yameonekana kutaka kutoa uelewa zaidi katika maeneo yafuatayo:
2.1 Noti mpya zikisuguliwa kwenye karatasi nyeupe zinaacha rangi na kwamba zikilowa zinatoa rangi. Je hali hii haitokani na uduni wa noti hizi mpya?
Hali ya kuacha rangi noti zinaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe ni ya kawaida kwa noti zote zilizochapishwa kwa teknolojia maalum inayojulikana kwa kitaalamu kama “Intaglio Printing”. Aina hii ya uchapishaji (Intaglio Printing) inazifanya noti kuwa na hali ya mparuzo zinapopapaswa. Teknolojia hiyo imetumika ili kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kuchanika na kuchakaa haraka. Miparuzo hii huacha rangi noti inaposuguliwa kwa nguvu kwenye karatasi nyeupe kitendo ambacho kinathibitisha kuwa noti hiyo ni halali. Hali hii pia ni moja alama ya usalama (security feature) inayothibitisha kuwa noti siyo ya bandia.
Aidha, noti halali hazichuji zikilowekwa kwenye maji kama inavyodaiwa kwa kuwa wino uliotumika hauyeyuki katika maji. Vilevile noti hizi zimetengenezwa kwa teknolojia ya kuwekewa kinga dhidi ya uchafu inayojulikana kitaalamu kama “Anti Soiling Treatment” ili kupunguza uwezekano wa kunasa uchafu inapokuwa katika mzunguko.
Teknolojia hizi mbili zinalenga kuongeza uhai wa noti katika mzunguko.
2.2 Je noti za zamani bado ni halali na zinaendelea kutumika?
Noti za zamani bado ni noti halali na zitaendelea kuwa katika mzunguko pamoja na zile mpya mpaka zitakapotoweka kwenye mzunguko kwa sababu za uchakavu wake. Kwa hiyo wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia noti za toleo la zamani bila wasiwasi wowote.
2.3 Kwa kuwa noti mpya ni ndogo kuliko za zamani kwa umbo je thamani ya noti hizo siyo pungufu kulizo zile za toleo lililotangulia?
Thamani ya noti ni ile iliyoonyeshwa kwa tarakimu zilizoandikwa kwenye noti yenyewe bila kujali ukubwa wake. Kwa hiyo thamani ya noti za zamani na za sasa haitofautiani.
2.4 Kwa kuwa kumekuwa na matatizo ya upatikanaji wa noti mpya, je Benki Kuu ina mipango gani kuhakikisha noti mpya zinapatikana nchi nzima?
Benki Kuu huingiza noti mpya katika mzunguko kwa kupitia benki za biashara. Benki Kuu inaendelea kutoa noti hizo mpya kupitia benki hizo lakini kwa kuwa mtandao wa baadhi ya matawi ya benki hizo ni mpana imechukua muda mrefu kwa baadhi ya maeneo kufikiwa na noti hizo. Hata hivyo kwa kuwa biashara nchini haina mipaka, noti hizo zitaendelea kusambaa nchini kote kupitia mzunguko wa kibiashara na kuongezeka siku baada ya siku.
2.5 Je noti halali zinatofauti gani na noti bandia?
Ili kuhakiki uhalali wa noti tunawashauri wananchi kuzichunguza kwa makini noti kwa kutumia alama za usalama kama zilivyoainishwa kwenye matangazo na vipeperushi vilivyotolewa na Benki Kuu ama kuwasiliana na ofisi zetu kwa ufafanuzi zaidi pale mtu anapokuwa na mashaka na noti hizi.
2.6 Je Benki kuu ina mikakati gani ya kuelimisha jamii na hasa vijijini kuhusu toleo jipya la noti?
Mtakumbuka baada ya uzinduzi wa noti mpya tarehe 17 Desemba 2010 nilisema noti hizi zitaanza kuingizwa katika mzunguko Mwezi Januari 2011. Hii ililenga kutoa kipindi cha kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari kuhusu toleo jipya kabla ya kuliingiza katika mzunguko. Aidha Benki Kuu ina mikakati endelevu ya kufikisha elimu ya “tambua noti zako” kwa wananchi wote kupitia matangazo, semina, ushiriki katika mikusanyiko mikubwa kama Sabasaba na nanenane na kwenye masoko pamoja na minada mikubwa ya mifugo. Tovuti ya benki kuu www.bot-tz.org vilevile imetoa maelezo mazuri kuhusu kutambua alama muhimu katika noti.
2.7 Kwa kuwa Benki Kuu inabadilibadili fedha kila baada ya miaka mitano hadi saba. Je ni kwa nini isiwe na toleo la kudumu kama ilivyo kwa fedha ya Uingereza au ya Marekani?
Kubadili noti husababishwa na maendeleo ya teknolojia ya uchapaji wa noti katika kuongeza uhai wa noti katika mzunguko na kuweka alama bora zaidi za usalama ambazo ni ngumu kuzighushi. Aidha sio kweli kwamba Uingereza na Marekani hazijabadili noti zake. Kuna mabadiliko makubwa na mengi tu yaliyopita na yanayotarajiwa kwa noti za nchi hizi.
2.8 Kwa nini Benki Kuu haikutoa noti kubwa zaidi ya 10,000 ili kurahisha malipo katika biashara?
Benki Kuu haikuona haja ya kutoa noti yenye thamani kubwa zaidi kwa sasa kwani malipo makubwa yanahimizwa kufanywa kupitia njia nyingine za kibenki. Noti ya Shilingi 10,000 bado inakidhi mahitaji ya malipo ya kawaida katika biashara kwa sasa.
Ni matumaini yetu kwamba ufafanuzi huu utaondoa wasiwasi uliokuwepo na kujenga imani kuhusu noti zetu mpya. Na Benki Kuu na matawi yake iko tayari kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu noti zetu mpya.pindi unapohitajika
Asanteni sana
Prof Benno Ndulu
Gavana
Benki kuu ya Tanzania
3 Februari 2011
Hata hivyo, wadau mbalimbali katika mtandao wa JamiiForums wamehoji kwanini Prof. Ndulu asitanabaishe kiasi gani kimetumika katika katika kuziandaa noti mpya mpaka zinatoka.