Rais John Magufuli: Sifahamu wizara ya madini ina ugonjwa gani

Jamii Africa
Rais Magufuli: Mimi si mwanasiasa mzuri wa kubembeleza bembeleza, nikitoka mimi mtapata wa kubembeleza - Asema Sheria ya Madini iliyopitishwa alisaini siku hiyo hiyo lakini kanuni mpaka leo bado hazijasainiwa - Amtaka Waziri wa Sheria, Prof. Kabudi akalifanyie kazi suala hilo, atafute watu wa kumsaidia na wakayamalize hayo

Licha ya serikali kuitenganisha wizara ya Nishati na Madini ili kuongeza ufanisi, inaelezwa kuwa wizara ya madini bado inakabiliwa na changamoto nyingi zinazokwamisha upatikanaji wa mapato na kuwatumikia wananchi.

Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam, rais John Magufuli amesema baadhi ya watendaji wa serikali waliopo katika wizara ya madini hawatimizi majukumu ya kikamilifu na kushindwa kuendana na dhamira yake ya kuwatumikia wananchi na kupunguza umaskini katika taifa.

 “Wizara ya madini ina changamoto nyingi na hata hivi sasa ina changamoto nyingi. Bado wizara ya madini haifanyi kazi vizuri sana, najua nikizungumza kwa kupamba nitakuwa mnafiki. Sifahamu wizara ya madini ina ugonjwa gani, wapo baadhi ya watu niliowateua hawajui ninataka nini”, amesema rais Magufuli.

Amebainisha kuwa  moja ya changamoto iliyopo ni kukosekana kwa kanuni zinaaoongoza sheria mpya ya madini iliyopitishwa na bunge mwaka 2017 ambazo zitalenga kuboresha utendaji wa wizara hiyo na kuimilikisha nchi rasilimali asilia ikiwemo madini yanayochimbwa maeneo mbalimbali nchini.

Sheria mpya ya Madini ilisainiwa mwaka jana na rais na kuanza kutumika lakini watendaji wa wizara hawajakamilisha kanuni na kuikwamisha serikali kufaidika na mapato yatokanayo na sekta ya madini.

“Bunge lilipitisha sheria ya madini kubadilisha ile sheria iliyokuwepo, mkapitisha sheria namba 7 ya mwaka 2017 ambayo bunge na watanzania wengi tuliamini kwamba kupitia sheria hii mambo mengi ya nchi yatanyooka ikiwa ni pamoja na kupata mrabaha na faida ya madini yetu”, ameeleza rais na kuongeza kuwa,

“Baada ya kufika mezani mimi niliisaini siku hiyo hiyo, nikatoa maagizo kwamba watendaji wangu wapitishe ‘regulations’ (kanuni). Sasa kuanzia mwezi wa 7 baada ya kupitisha sheria namba 7 mpaka leo hii ‘regulations’ hazijasainiwa, Waziri yupo, Naibu Waziri yupo na Kamishana ambaye ndiye mshauri mkuu wa waziri yupo”.

Amesema hatari iliyopo ya kutumia sheria bila kanuni ni kushindwa kuwatia hatiani wanaokiuka sheria hiyo, “Kama zile regulations hazijasainiwa mpaka leo mnategemea nini? Usipokuwa na ‘regulations’ mtu yeyote atakapokosa atapelekwa kwenye mahakama ipi?” ameuliza rais Magufuli na kuwatupia lawama baadhi ya watendaji wa serikali ambao wameshindwa kuwajibika kwenye nafasi walizoteuliwa.

                             Naibu Waziri wa wizara ya Madini, Dotto Biteko akihutubia mkutano wa hadhara kabla ya kuteuliwa kuingia kwenye wizara hiyo.

 

Hatua aliyochukua

Ili kuongeza ufanisi wa wizara ya madini, rais alimteua Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko na kumuapisha leo kuwa Naibu Waziri wa pili wa wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Angellah Kairuki na Naibu Waziri Stanslaus Haroon Nyongo.

Naibu Waziri mteule wa madini, Biteko ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati maalum ya Bunge la Tanzania iliyoteuliwa na Spika Job Ndugai kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite ambapo uteuzi wake utaongeza nguvu kwa wizara hiyo ikizingatiwa kuwa kamati yake ilifanikiwa kuibua upotevu wa mapato ya Tanzanite unaotokana na kutozingatiwa kwa sheria.

“Na ndio maana nikaona labda ngoja niongeze Naibu Waziri aliyekuwa kwenye kamati ya madini ili ushauri uliokuwa unatolewa na bunge atatoa changamoto kwa watu ambao bado wamelala ndani ya serikali”, amesema rais.

Pia ameigiza wizara hiyo kupitisha na kusaini kanuni za madini kabla ya ijumaa ya wiki hii ili zianze kutumika na kuondokana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amemfuta kazi Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na kumteua Prof Shukrani Manya kuchukua nafasi hiyo kuwa msimamizi wa Tume ya Madini.

“Nimeambiwa Kamishana wa Madini ni tatizo, inawezekana yupo hapa, nimeamua kumteua Profesa Shukrani Elisha Manya atakuwa Kamishna wa madini na ndiye atakuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini”, amesema rais.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema amefurahishwa na aumuzi wa serikali kukubali ushauri wa bunge wa kutenganisha wizara ya nishati na madini ili kuipunguzia majukumu ya kiutendaji.

“Sisi bunge tumekuwa tukishauri kwa muda sana kwa serikali kuwa wizara ya nishati na madini imekuwa wizara kubwa na nzito sana na nashukuru umeifanyia kazi kwa kuweka wizara mbili za madini na nishati”, amesema Spika Ndugai.

Naye Naibu Waziri, Dotto Biteko amemshukuru rais kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo ili kuongeza tija kwa taifa na kuahidi utendaji uliotukuka.

“Mheshimiwa rais nina bahati kubwa sana na hata wewe umelishuhudia kwenye mikutano mingi sana, umenipa sifa kubwa kwa kuhudumu chini ya mwanamke ambaye ni mchapa kazi sana. Niko tayari kufanya kazi kwa bidii na namuomba Mungu usije jutia uamuzi wako”, amesema Naibu Waziri Biteko.

 

Wizara ya Nishati na Madini

Wizara ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu nchini kutokana na mchango mkubwa katika pato la taifa baada ya sekta ya kilimo na utalii. Lakini wizara hii imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji ambazo zimesababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu kwa kashfa za ufisadi wakiwemo Prof. Sospeter Muhongo, George Simbachawene na Willium Ngereja.

Hata hivyo, Tanzania haijafaidika na sekta ya madini licha ya kuwa hazina kubwa ya madini ikiwemo Tanzanite ambayo hayapatikani mahali popote duniani. Kwa kutambua hilo serikali imepitisha Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2017 ambayo inawapa nguvu watanzania kumiliki rasilimali asilia.

Pia serikali inapitia mikataba ya wawekezaji katika sekta hiyo ili kubaini mapungufu ya kisheria yaliyopo na kurekebisha. Mathalani imezuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi na kuitaka Tume ya Madini kujenga mtambo wa kuchenjua madini hayo nchini ili kudhibiti upotevu wa mapato.

Mazungumzo na kampuni ya dhahabu ya Barrick yanaendelea ili kufikia muafaka wa kugawana faida ya 50 kwa 50 ya mapato yote yanayopatikana kwenye uwekezaji wa madini hayo.  

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *