Ruvuma: Wanafunzi zaidi ya 8,000 Kidato cha Nne wapata SIFURI

Albano Midelo

WANAFUNZI 8365  kati ya 11364 wamefeli mtihani wa  Taifa wa kidato cha nne katika mkoa wa Ruvuma kwa kupata alama sifuri.

Taarifa ya Afisa Elimu wa mkoa wa Ruvuma Mayassa Hashim ambayo ameitoa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Ruvuma (RCC) inaonyesha kuwa katika mtihani huo uliofanyika mwaka jana wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 13, daraja la pili 96, daraja la tatu 273 na daraja la nne wanafunzi 2,617 huku wanafunzi 8,365 wakipata sifuri.

Taarifa hiyo ya elimu inaonyesha kuwa shule iliyokamata nafasi ya kwanza kimkoa ni sekondari ya Mtakatifu Luis inayomilikiwa na watawa wa jimbo Katoliki Mbinga ambayo daraja la kwanza wapo wanafunzi wawili, daraja la pili 10, daraja la tatu18, daraja la nne tisa hakuna mwanafunzi alifeli.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo nafasi ya pili imekamatwa na seminari ya Likonde inayomilikiwa na jimbo katoliki la Mbinga ambapo daraja la kwanza wapo wawili, daraja la pili 11, daraja la tatu12, daraja la tatu 13 hakuna mwanafunzi aliyefeli.

Shule ya sekondari ya Ndongosi ambayo mwaka 2011 ilikuwa ya mwisho kitaifa baada ya kufelisha wanafunzi wote, mwaka jana shule hiyo imekata nafasi ya mwisho katika shule za sekondari 163 za mkoa wa Ruvuma baada ya kufelisha wanafunzi wote wa kidato cha nne

Kufuatia matokeo hayo mabaya, Afisa Elimu wa mkoa wa Ruvuma aliitaja mikakati ambayo inachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuwa ni pamoja na kutoa vifaa vya kujifunzia, kufundishia, kukuza taaluma kwa ufanisi na kutoa motisha kwa wanafunzi.

“Nawaomba wazazi na walezi wasisahau wajibu wao kwa wanafunzi ikiwemo kujenga tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto wao, kuwanunulia mahitaji muhimu ya shule, kuangalia tabia za watoto wao na kushirikiana na walimu ili kuboresha taaluma katika shule zao’’, alisisitiza.

Baadhi ya changamoto ambazo ziliibuliwa katika kikoa hicho na kutajwa kuwa zinachangia kushusha taaluma ni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu, mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia, baadhi ya wakuu wa shule kutoishi shuleni na utoro wa baadhi ya walimu.

Akizungumza wakati anafungua kikao hicho cha RCC mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu aliwakumbusha wadau wote umuhimu wa kudumisha amani,upendo, utulivu na mshikamano wa kitaifa  ambao alisema siku za karibuni kumekuwa na vitendo vya wazi kushabikia machafuko.

“Kwa bahati mbaya sana kuna watu wachache wanaendesha vitendo vya uchochezi kupitia imani za kidini kwa kuhubiri chuki miongoni mwa wananchi katika nyumba za ibada na nje ya nyumba hizo kupitia mihadhara ya kidini, kutumia kanda za kaseti na video kwa mwamvuli wa kueneza elimu ya dini kwa waumini wao’’, alisema.

Alisisitiza kuwa machafuko hayafanyiwi majaribio na kwamba hakuna aliyefanikiwa kupitia machafuko akatahadharisha kuwa gharama ya kupoteza amani ni kubwa kuliko kitu chochote hivyo amewataka wananchi kuwakataa wote wanaohubiri chuki za kidini, kikabila na itikadi za kisiasa kwa lengo la kuwagawa watanzania na kuleta machafuko.

“Serikali haitamvumilia mtu yeyote, kundi lolote, kiongozi wa kidini au siasa atakayeonekana kuchochea machafuko na chuki mkoani kwetu, serikali kupitia jeshi la polisi itamkamata na kumfikisha mbele ya sheria’’, alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *