Sakata la bei ya sukari, mafuta ya kula latikisa tena bungeni. Spika Ndugai amshukia Waziri wa Viwanda

Jamii Africa

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai  amelazimika kuingilia kati mvutano ulioibuka bungeni kuhusu tofauti ya bei ya sukari kati ya Tanzania bara na Zanzibar  na kuitaka serikali itoe majibu yaliyojitosheleza ili kuondoa utata uliopo.

Ndugai alifikia hatua hiyo baada ya kuibuka mvutano kati ya Waziri wa Viwanda, Charles Mwijage na  Mbunge wa Mpendae, Salim Hassan Turky ambaye alitaka kujua ni kwanini bei ya sukari ni tofauti kwa pande mbili za Muungano.

Akijibu swali hilo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage  alisema tofauti hiyo ni matokeo ya gharama kubwa za uzalishaji upande wa Tanzania bara.

Kufuatia majibu hayo, Mbunge Turky hakukubaliana nayo, ndipo Spika Ndugai aliingilia kati na  kusema swali alilouliza Mbunge huyo halijapata majibu na kuitaka serikali ijipange na kutoa majibu ya uhakika ili kuondoa utata huo.

“Kwa hiyo tutalipanga tena kwenye maswali ya wiki ijayo ili Serikali ituletee majibu ya uhakika. Kama kweli wananchi wa Tanzania bara wanalazimika kulipa mara mbili ya bei inayouzwa Zanzibar kisa kulinda wenye viwanda, ha ha ha, haiwezekani hiyo, tunahitaji majibu ya uhakika zaidi, ‘Chief Wheep’ wiki ijayo tutalipanga swali hili tupate majibu hasa ya uhakika nini hasa kinachoendelea kwenye jambo hili” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema, haiwezekani wananchi wa Tanzania bara wauziwe sukari kwa bei ambayo ni mara mbili ya bei wanayouziwa wananchi Zanzibar.  Ameitaka Serikali wiki ijayo itoe majibu ya uhakika kuhusu jambo hilo kwa kuwa hata kama lengo ni kulinda viwanda vya ndani jambo hilo haliwezekani.

“Bei ya sukari ina maana kubwa kwa maisha ya watanzania, haiingii akilini bei ya Tanzani Bara kuwa tofauti na ile ya Zanzibar,” amesema Spika.

                              Bei ya sukari ina maana kubwa kwa maisha ya watanzania

Wakati anauliza swali la nyongeza, Mbunge wa Mpendae, Turky alitaka jibu la Serikali ni kwa nini sukari ya kilo 50 inauzwa kwa bei ya sh. 110,000/- Tanzania bara wakati Zanzibar kuna kiwanda cha sukari kinachouza kilo hizo wa bei ya sh. 65,000/-

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, kwenye soko la dunia kilo ya sukari inauzwa kwa dola 390 za Marekani na ikitozwa ushuru wa asilimia 25 na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bidhaa hiyo inauzwa kwa sh.65, 000/- hivyo alitaka kufahamu kwa nini inauzwa kwa sh.110, 000/-

Turky pia alihoji kwa nini Serikali haiwaelezi wabunge gharama za uzalishaji viwandani wakati walishataka ifanye hivyo kwa miaka mingi.

Wakati anajibu swali hilo, Waziri wa Viwanda, Biashara, Charles Mwijage alisema gharama za uzalishaji sukari kwa viwanda vya Tanzania ni kubwa kuliko kwa viwanda vya Zanzibar.

“Mheshimiwa Turky ulipewa kibali na serikali kuagiza sukari kwa nini hukuuza kwa bei rahisi” alisema Waziri Mwijage na akaenda kukaa.

Hata hivyo, Waziri Mwijage ametoa hofu wananchi kuwa hakuna upungufu wa sukari nchini na kwamba wameviagiza viwanda vinne kuzalisha sukari ili kuongeza ulimaji wa miwa katika mashamba yao.

 

Sakata la Mafuta ya Kula laibuka tena

Kufuatia serikali kutoa ahadi siku ya jana bungeni kuwa ingetoa majibu ya uhakika kuhusu kuzuiliwa kwa meli iliyobeba mafuta ya kula kwasababu ya kutokuwepo kwa maelewano ya kodi, Spika Ndugai aliingilia kati tena suala hilo  leo na kuitaka serikali kutoa majibu yanayoeleweka.

Ndugai amesema, kwa namna serikali inavyoshughulikia suala la bei ya mafuta inaifikisha nchi mahali pagumu kwa mambo madogo madogo ambayo yanaweza kutatuliwa.

“Mambo madogo mno, hivi kweli nchi hii leo wale tuliosoma kemia pamoja na mimi, hivi kweli kupima , kupima mafuta kujua kama haya ni semi refined (safi kigodo ) ama ni crude (ghafi) hiyo nayo ni rocket science (sayansi ya roketi)?, kitu cha dakika 15? Watu wanazunguka wanazunguka…” amesema.

Spika amesema, kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawaliamini  Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mkemia Mkuu na maabara zake, ni vema  mafuta hayo yakapimwe Afrika Kusini, London au Nairobi ili kuondoa utata  ambao unawaumiza wananchi.

“Mkiligeuza Bunge hili likawa ni mahali pa kubangaiza bangaiza hivi haitakuwa sawasawa kwa hiyo saa 11 mje na maelezo ya jambo hili” amesema na kuongeza kuwa,

“Tukitengeneza mazingira ya TRA, mbabe mmoja anakaa anasema mimi, haiwezi kuwa hivyo, haiwezi kuwa hivyo, kama ni semi refined ipigwe kodi semi refined, kama ni crude ni crude, sasa ubishi wa nini, hakuna sababu ya ubishi, kwa hiyo tunategemea serikali saa 11 mtakuja na majibu, tunaumiza wananchi.”

Jana Waziri Mwijage aliahidi bungeni kuwa jana au leo angetoa taarifa ya Serikali kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, na leo ameahidi kabla ya saa 11 jioni atampa Spika Ndugai taarifa kuhusu uchunguzi unaofanywa.

Kauli ya serikali ilikuja siku chache baada ya kuwepo kwa malalamiko ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kutokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuzuia meli ya mafuta kushusha mzigo bandarini mpaka zilipe kodi kulingana na sheria mpya ya kodi iliyopitishwa Februari mwaka huu.

Ukileta mafuta kwa sheria tuliyopitisha sisi Tanzania kwa mafuta ghafi tunamtoza asilimia 10.

Utaratibu wa kodi uliopo wa kodi ni kwamba mafuta safi yanayoagizwa toka nje yanakatwa kodi ya asilimia 25 na mafuta ghafi (crude oil) hutozwa asilimia 10.

Lakini kwa mujibu wa waziri Mwijage, vipimo vya Kamishna wa forodha katika bandari ya Dar es Salaam vilionyesha mafuta hayo yaliyozuiliwa tangu mwezi uliopita kuwa sio ghafi wala safi. Kutokana na msimamo huo wa idara ya forodha wanadai kodi inayotakiwa kulipwa ni asilimia 25 lakini wafanyabiashara walikataa.

“Kinacholeta tatizo ni kutokukubaliana katika viwango vya kodi. Ukileta mafuta kwa sheria tuliyopitisha sisi Tanzania kwa mafuta ghafi tunamtoza asilimia 10. Vipimo vilivyopimwa na kamishna wa customs (forodha) vinamuonyesha kwamba hii sio crude oil (mafuta ghafi) au finished oil (mafuta safi) ambayo inamuonyesha kamishana basi hivi ni mafuta safi anataka kutoza asilimia 25,” alisema Mwijage.

Kutokana na utata huo, wafanyabiashara walikataa kulipa kodi ya asilimia 25 kwasababu wanaamini mafuta hayo ni ghafi na yanapaswa kutozwa kodi ya asilimia 10 na si vinginevyo. Mafuta hayo yamezuiliwa tangu mwezi Aprili mwaka huu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *