Sakata la Lwakatare: Wanasheria CHADEMA ‘wafunguka’!

Jamii Africa

Kiongozi wa jopo la wanasheria watano (5) wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, Wakili Tundu Lissu, akiwawakilisha wenzake, ameongea na vyombo vya Habari akiwa Makao Makuu ya CHADEMA na kuzungumzia masuala kadhaa kutokana na sakata hili.

Lengo kuu la mkutano huo na wanahabari lilikuwa ni kuutarifu umma wa Watanzania kupitia kwa wanahabari juu ya hatua ambayo mawakili hao wameamua kuchukua kwa kupeleka ombi Mahakama Kuu ya Tanzania, chini ya hati ya dharura ili Mahakama hiyo ya juu iitishe mafaili yote mawili yaliyofunguliwa kuhusu kesi ya Lwakatare, yaani faili la kesi iliyofutwa na faili lililofunguliwa baada ya kesi ya awali kufutwa, wakiiomba mahakama iangalie na kujiridhisha…

Kupitia hati hiyo ya dharura, mawakili hao wanaiomba Mahakama Kuu:

– Ifute hati ya DPP iliyotolewa jana ikifuta mashtaka ya awali
– Ifute amri ya mahakama ya iliyotolewa kumaliza kesi iliyofunguliwa awali kabla ya kufutwa jana
– Ielekeze Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itoe maamuzi kama ilivyokuwa imepanga kutoa kabla 'haijaingiliwa' kwa DPP kuifuta kesi mahakamani.
– Na pia wameiomba Mahakama Kuu, itamke kuwa hicho walichofanya waliomfungulia kesi Lwakatare ni matumizi mabaya ya;

1. Mamlaka ya DPP
2. Mfumo wa Mahakama na
3. Kuingilia uhuru wa Mahakama

Mbali ya maelezo hayo, Wakili Lissu pia amejibu maswali ya wanahabari, ambapo walitaka kujua masuala mbalimbali kuhusu kesi na mashtaka yanayomkabili Lwakatare, akisema:

Mosi, Ili kosa liwe la kigaidi, ni lazima kuwepo maelezo yanayofafanua kuwa kuwa mtuhumiwa alikuwa na malengo au nia ya kigaidi; lakini hakuna maelezo ya namna hiyo kwenye hatia ya mashtaka kueleza ‘terrorism intention’. Alifafanua kuwa kwa maoni yake, Lwakatare amefunguliwa mashtaka ya kigaidi kwa nia tu ya kutaka asote gerezani, kwa sababu waliofungua mashtaka wametaka hivyo… ateseke!

Pili, Nolle prosequi iliyowasilishwa jana na DPP kufuta kesi iliyofunguliwa Jumatatu Machi 18, 2013 kwa ridhaa yake inazua maswali sana (questionable) sana kwasababu hakuna mahali mazingira yanaonesha iliwasilishwa kukidhi masuala mawili muhimu, maslahi ya umma na kuboresha utendekaji wa haki.

Amedai inazua maswali zaidi kwa sababu kadhaa; mbali ya kwamba ilitolewa wakati ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikuwa inakuja kutoa uamuzi kutokana na mabishano ya kisheria yaliyoibuka siku ya Jumatatu, hati mpya ya mashtaka haina kitu kipya isipokuwa hakimu na namba ya kesi. Vitu vingine vyote, ikiwemo aina, idadi ya mashtaka hadi nukta vimebaki vile vile kama vilivyokuwa kwenye hati ya mashtaka ya awali.

Lissu alisema ndiyo maana jopo hilo linaiomba Mahakama Kuu ihoji dalili za uingiliwaji uhuru wa mahakama kwa DPP kuamua kutoa nolle prosequi, siku ambayo mahakama ilikuwa inakuja kutoa maamuzi juu ya mabishano ya kisheria.

"Ingawa mimi sijui mahakama ilitaka kusema nini… wenzetu wana taarifa za kiintelejensia, inawezekana wamejua hakimu angekuja kuamua nini kutokana na mabishano ya kisheria yaliyotokana na hoja za upande wa utetezi, hivyo wakaamua kuleta hiyo hati ya kufuta mashtaka. Kwa sababu haiingii akilini mawakili kama hawa wa serikali ambao wawili ni mawakili wakuu na mmoja wakili mwandamizi, walikosea waliyokosea," alisema Lissu na kuongeza;

"Ingawa watu wengi wanasema na kweli inaonekana hivyo kuwa mamlaka ya DPP kuingilia kesi yoyote na wakati wowote kabla haijatolewa hukumu ni makubwa sana, lakini ikumbukwe kuwa kuna kumbukumbu za maamuzi ya mahakama ambazo zinasema wazi kuwa mamlaka hayo ya DPP yana mipaka, hayawezi kufanyika isipokuwa iwe kwa ajili ya maslahi ya umma au kwa ajili ya kuboresha utendekaji wa haki, lakini kilichofanyika jana ni matumizi mabaya ya mamlaka ya DPP."

Kuhusu video
Wanahabari walitaka kujua maoni yake kuhusu video na namna kesi hiyo ilivyo, hasa kutokana na alivyoielezea ‘charge’ ilivyo ‘defective’, ambapo Wakili Lissu kwa maoni yake, alisema kuwa kuna masuala mengi yanatakiwa kuwekwa wazi kuhusu video yake, akihoji maswali kadhaa:

– Nani aliyemrekodi Lwakatare? Je, Lwakatare alijua kuwa anarekodiwa? Je, aliruhusu? Kama hakuruhusu, ilifanyika kihalali? Je, haivunji katiba ya nchi inayozungumzia privacy ya mtu? Je, baada ya kurekodiwa mkanda huo ulipelekwa wapi? Nani alikuwa nao? Je, umefanyiwa uhariri (editing) na nani? Je, aliyemrekodi alitumwa na nani?

Ushahidi mwingine
Ameongeza kuwa, video inaonekana imechukuliwa tarehe 28 Desemba, siku iliyofuata, Desemba 29, kwenye kipindi cha TV, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba akaanza kusema kuwa anayo video ya viongozi wakuu wa CHADEMA wakipanga mipango ya mauaji ya dhidi ya Watanzania.

Amezungumzia mawasiliano ya mtu anayeitwa Michuzi, kuwasiliana na watumishi wenzake wa OBR, akiwapongeza na kutoa kudos kwa TISS kwa kazi nzuri, akiwataka wenzake wapige sana kelele kwani hiyo ni kete muhimu kwa CCM. Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa, hawaruhusiwi kufanya surveillance dhidi ya wapinzani wa kisiasa wa CCM, kwa sababu upinzani wa kisiasa ni suala lililoruhusiwa kisheria nchi hii.

Aidha, Lissue ameongeza kusema wamepata mawasiliano ya simu yakionesha kuwa siku hiyo hiyo ambayo video imerekodiwa, majira ya saa 5.59, mtu aitwaye Ludovick alimpigia simu mtu aitwaye Mwigulu Nchemba.

Kwa mujibu wa Wakili Lissu, yamepatikana pia mawasiliano ya mtu aitwaye Dennis Msacky akimpigia simu Lwakatare, ambapo wamemuuliza Lwakatare iwapo ni kweli aliwasiliana na mtu mwenye jina hilo (ambaye kwenye charge sheet ya pili, polisi wameonesha ndiye aliyekuwa akipangiwa kutekwa/kufanyiwa vitendo vya ugaidi), naye amekubali kuwa ni kweli alimpigia simu siku moja kabla ya tukio la kurekodiwa, akimuuliza kama amerudi Dar es Salaam, naye akamwambia alikuwa njiani kutoka Bukoba.

Amemaliza kwa kusema kuwa kesi hii ni kama kesi nyingine za kupikwa, ambazo polisi wamekuwa wakifungua dhidi ya CHADEMA na viongozi wa chama hicho, kwa nia ya kuiokoa CCM, kwasababu chama hicho kimekaliwa vibaya na hakiwezi tena kufanya siasa za ushindani dhidi ya wapinzani wao wakuu, CHADEMA.

"Ni mambo yale yale, walianza chama hiki cha familia ya Mtei na Mbowe, ikashindikana, chama hiki cha kikabila, cha Wachaga… ikashindikana, wakasema chama hiki cha kaskazini, imeshindikana, wamesema chama hiki cha wakatoliki, ikashindikana, wamesema chama hiki cha wakristo bado Watanzania wamekataa, iemshindikana pia… Sasa unafanyaje? Tengeneza hii kitu, sasa kiwe chama cha magaidi…ITASHINDIKANA pia," alisema Wakili Lissu.

27 Comments
  • Ni kweli ccm wameishiwa sera hawajui ndiyo kuwapa wapinzani wao umaarufu, waache siasa za kudanganya watanzania

  • Kama mipango na njama kila chama kina njia zake akuna chama kisicho na mipango wala njama chadema nyie sio wataka tifu mseme mnatenda haki kiuwalali ili ni fundisho muamini kuwa Duniani akuna siri tena nyie habari za wenzenu kuya hanika ni vizuri za kwenu mipango ya ccm kukiyumbisha chama chenu alafu jinsi mtavyo kuwa wakali wakati wenzenu makosa sio ya chama mnasema chama ila kwaili tunaendelea kuwagea masikio yetu mtudanganye maana mmezoea kutufanya vipofu kwa kutumia wasomi wasio na huruma na jamii ya kitanzania

  • Hata wafungwe viongozi wote wa chadema ccm tukiwapambanisha na jiwe tunalipigia kura jiwe. Vijana wapo wengi kwa ajili ya chadema

  • There is wise words”you can fool people for sometimes but not all the time”ipo siku ukweli wa haya yote utajulikana.God is not bias.

  • ccm watanzania wamewachoka sana mumezidi kutumia mbinu za kigaidi ili chadema ionekane mbaya ktk jamii kumbe mnazidi kujipalilia kaburi mafisadi

  • Mm naona private ya mtu km vile kumrecord mtu akiwa anaoga,au tendo la ndoa lkn mtu apangae kuangamiza wenzie kung’oa meno na kucha kwa nn asirecordiwe hii ngoma cdm haiwezi kutoka coz ludo ni mfanyakazi wao,hawa cdm wauwaji wakubwa

  • ktk siasa kila kitu kinawezekana.tusishabikie ujinga uliofanyika,mahakama ndo itaamua hatma ya kesi na si kuweka uchama mbele.hv ingetoka clip ya njama ya kumuua ndugu yako ungehoji uhalali wa hyo video clip? Au ungetaka sheria iwe mbele?

  • Tanzania letu hatuta endelea kama tukiendeleza siasa kuwa vita na sio changamoto.kiukweli chama makini chadema kimetufumbulia macho sana kuhusu nchi yetu hasa vijana wasomi kuingia bunge pongezi kwa wote.video iliyorushwa mtandaoni ni kashfa kubwa sana kwa chama but due 2 technology tunaweza kusema it can be editing of some worlds, the only issue watanzania tunaitaji ni maendeleo na inaonekana chama kilichopo akitutimilizii haja za watanzani pia wajue kuwa kizazi cha sasa ni cha wasomi. maoni yangu kuwa na democracy ya kweli na sio kungangania vyeo wakati nochanges zinazotokea hasa increase in economically na tunajivunia na kuwa na mali asili nyingi Africa

  • Hi video mmeshajaribu kuingalia njama kama za kigaidi haziwezi kupangiwa sehemu kweupe kama hio na hao mnaotetea ccm hiki ni chama tawala lazima shutuma nyingi zielekezwe kwa hicho chama tawala nia ya vyama pinzani ni kuhahikisha kinang'olewa madarakani

  • Jamani haya mambo mbona siyaelewi, I cant tell "white and Black"  ee Mungu nipe macho ya kuona na ubongo wa kuchanganua kila jambo linalotokea, naiachia mahakama iseme ijapokuwa napata wakati mgumu kuiamini mahakama, mihimili yetu haifanyi kazi kwa uhuru kutokana na mfumo uliopo

  • Ata nelson mandela alinyanyaswa sana na makabulu (ccm) ila alifanikiwa kuikomboa south na ubaguzi wa langi naamini chadema ipo cku itawakomboa na ccc (mafisadi wasiokuwa na huruma)

  • Mi natambua ccm wameishiwa,unajua akuna jambo lislokuwa na mwsho ivyo ccm lazma wakubli kuwa mwsho wao umefka. Kwli mfa maji haish kutapatapa.

  • Ukitaka kujua kama hiyo video ni kweli au si kweli kwanza angalieni nyuma ya muhusika kuna nn, kama kuna artficial picha kama barabara, nyumba, shamba au kitambaa pili body language ya muhusika na anachoongea ni sawa. Hivyo ni vitu vichache vinaweza kupima huo mgogoro wenu

  • Watanzania tunaipeleka wapi nchi yetu? Michezo michafu itakoma lini katika nchi inayohubiri kila siku kuwa inazingatia utawala wa sheria na demokrasia? Ifike mahali watanzania tuache siasa za fitina na ushabiki ambao hauna maana!

     

  • Achani mahakama zifanye kazi, msigombane. Kama mnavyofahamu, mahakama sasa zinajitahidi sana kutoa haki. na nadhani mawakili wote wanauwezo wa kuwatetea wateja wao

     

  • Ukweli mahakama na mawakili ndio watakao badili mada hii. Kwani akipatikana na hatia mtasema hakutendewa haki mtapanga kuandamana na kufanya vurugu kwa mslahi ya huyo kumanda. Akiachiwa mtasema mbinu za CCM zimeshindwa pia mtafanya maandamano

  • Tundu hivi sahihi kuzungumzia kujadili ushahidi wa kesi iliyo mahakamni mbele ya waandishi wa habari? Si uache mahakama iamue juu ya uthabiti wa ushahidi?

  • (blood is for changes), twapaswa kugangamala vyema, we need to change our mind for the real direction and the the way is to ignore the false and stand for the truth. God bless Citizen, God bless Tanzania.

    • ndio mala ya kwanza najiunga jf forum mimi ni jembe! nilikuwa nafanya tafiti za mambo yanayoendelea duniani ili nipate cha kusema PEOPLEEEEEEEEEEEEEEEEEEZ NGUVUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUUU, mc Kuzacha

  • hatimae nchemba anaumbuka. ukikosa maadili kwenye jamii basi kila ufanyacho kitakurudia mwenyewe. ewe mguru wa chemba fanya siasa na sio umafia kwa viongozi wa siasa wa vyama pinzani

  • Uchunguzi wa jukwaa la wahariri wa habari Tanzania (TEF) juu ya kadhia za ugaidi kwa mwandishi wa habari Absolom Kibanda wametahadharisha juu ya siasa chafu za Chadema na CCM kwa kutaka kuingia madarakani kwa nguvu na hali watawala hawataki kutoka, Tunadhani siasa chafu za vyama hivi zitakuwa zimeanza lini hadi tunataka kuikingia kifua Chadema kutokuwa na magaidi kama Wilfred Rwakatare? Kushinda kesi wakati mwingine hutegemea ujanja "Teknik" ya wanasheria lakini kiukweli gaidi hubaki kuwa ni gaidi tu. Hata kama sheria itakuwa imeshindwa kumkaamata aliyehusika katika issue ya Mhe Chacha Wangwe lakini watu wakawaida si wanajua ukweli.

    Baada ya Absolom Kibanda WHO NEXT!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *