Sauti za Wananchi: Rushwa yatawala kazini, ushindani waongezeka sekta ya ajira

Jamii Africa
UTAFITI: Asilimia 51 ya Wananchi wanasema kuwalipa Watumishi wa umma posho kwa ajili ya kuhudhuria mikutano ni moja ya aina ya rushwa. - Aidha, 73% ya wananchi wanasema rushwa ni kitendo cha kutoa fedha kwa ajili ya kupata msaada huku 36% wanataja rushwa kuwa ni utoaji wa vitu vya thamani. - Upi mtazamo na ufahamu/uelewa wako kuhusu rushwa?

 Licha ya maoni ya wananchi wengi kuonyesha vitendo vya kutoa na kupokea rushwa kupungua katika sekta ya umma, lakini vitendo hivyo vimeshamiri katika maeneo ya uzalishaji na kuathiri sekta ajira nchini.

Upatikanaji wa ajira umekuwa na changamoto mbalimbali ikizingatiwa kuwa idadi ya watu waliosoma imeongezeka ikilinganishwa na ukuaji mdogo wa soko la ajira ambalo linaleta ushindani kwa wahitimu wa fani mbalimbali.

Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Shirika la Twaweza (2017) uitwao: ‘Hawashikiki? Mitazamo na maoni ya watanzania juu ya rushwa’ uliotolewa mapema leo unaonyesha kuwa rushwa katika sekta ya umma na binafsi imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, utafiti huo ambao unatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,705 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara, unaonesha rushwa imeongezeka katika sekta ya ajira huku ikifuatiwa kwa karibu na Jeshi la Polisi ambalo linaongoza katika nafasi ya juu licha ya viwango hivyo kupungua kila mwaka.

“Sekta pekee ambayo rushwa iliripotiwa kubaki vilevile ni sekta ya ajira. Asilimia 34 ya wananchi waliripoti kuombwa rushwa mwaka 2014 huku asilimia 36 wakiombwa rushwa mwaka 2017” inaelezwa sehemu ya ripoti hiyo ya Twaweza na kubainisha kuwa rushwa imepungua katika maeneo mbalimbali,

“Wananchi wanaripoti kuwa viwango vya rushwa vimepungua nchini. Mwaka huu wa 2017, ni asilimia 85 ya wananchi walioripoti ukilinganisha na mwaka 2014 ambapo asilimia 78 walisema viwango vya rushwa vilikuwa vikubwa kuliko miaka 10 iliyopita”.

Inaelezwa kuwa kupungua kwa viwango vya rushwa ambako wananchi wanaripoti katika maeneo mbalimbali kunatokana na juhudi za serikali ya awamu ya tano ambayo imekuwa ikijinasibu kuwashughulikia watu wote wanaojihusisha kutoa na kupokea rushwa kwa kurejesha nidhamu katika taasisi zinazotoa huduma za kijamii.

“Pengine kutokana na uzoefu wa viwango vikubwa vya rushwa, wananchi wengi wamepata matumaini juu ya mapambano dhidi ya rushwa; mwaka 2014, nusu ya wananchi (asilimia 51) walisema rushwa haiwezi kupunguzwa nchini, wakati mwaka 2017, asilimia 63 ya wananchi wanasema itaweza kupunguzwa kwa kiwango Fulani.

Wasemavyo Wadau

Aliyewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Hesabu za Serikali (CAG) katika serikali ya awamu ya nne,  Ludovick Uttoh amesema kwa uzoefu alionao wa kufanya kazi kama mtumishi wa umma anaamini rushwa imepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita. Pia imezitaka mamlaka zinahusika na kupambana na rushwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Ili kutokomeza rushwa katika jamii, wananchi wametakiwa kushirikiana na serikali ambayo imeonyesha dhamira ya kupambana na  ufisadi kwa kutoa taarifa sahihi za watu wote ambao wanatoa na kupokea rushwa ili ichukue hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo amesema ili serikali ifanikiwe katika mapambano ya rushwa inapaswa kutengeneza mfumo wa kutoa taarifa za rushwa ambao utawahakikishia usalama wale wanaotoa taarifa hizo.  

“Serikali iweke wazi ni njia zipi zinaweza kutumiwa na wananchi kung’amua na kuripoti vitendo vya kifisadi. OGP imefutwa na njia mbadala haijawekwa wazi na serikali ina jukumu la kuwahakikishia wananchi wanaoripoti taarifa za rushwa usiri wa taarifa zao na usalama wao pia”, amesema Melo na kuitaka serikali kujenga mahusiano mazuri na Asasi za kiraia na vyombo vya habari ambavyo ni wadau muhimu katika mapambano ya rushwa katika jamii,

“Serikali haiwezi ikapambana na rushwa peke yake, vyombo vya habari na Asasi za kiraia wanasaidia kazi hizi lakini ni vema kuwe na uwazi kwa upande wa serikali ili kuboresha ushirikiano”

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Usimamizi kutoka Taasisi ya Kupambana na kutokomeza Rushwa (TAKUKURU), Sabina Seja amesema kiwango cha wananchi kutoa taarifa za rushwa kwa taasisi hiyo  kimeongezeka  ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo taarifa hizo zilikuwa hazifanyiwi kazi.

“Mwaka 2014 kulikuwa na malalamiko takribani 5,000 toka kwa wananchi; kwa 2016/2017 malalamiko yameongezeka kufikia takribani 7,000, hii inaweza kumaanisha wananchi wamepata ujasiri wa kuripoti vitendo vya rushwa”, amesema Sabina Seja.

Hata hivyo amesema wakati mwingine maamuzi ya kesi za rushwa zinazopelekwa mahakamani yanachelewa kwasababu ya uchunguzi huchukua muda mrefu, lakini amewata wananchi katika maeneo yao kuungana na serikali kutoa taarifa n akutojihusisha na vitendo vya kupokea na kutoa rushwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *