WAJIBIKA: Sekta ya manunuzi kinara wa rushwa serikalini, sekta binafsi nchini

Jamii Africa

Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)aliyestaafu, Ludovic Utouh amesema  mapambano ya rushwa nchini yanakwamishwa na biashara baina ya serikali na sekta binafsi hasa kwenye manunuzi ya huduma na bidhaa yasiofuata taratibu za kisheria.

Akizungumza  katika mjadala wa uwajibikaji uliondaliwa na Taasisi ya Wajibu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro, Utouh ambaye alihudumu kama CAG katika serikali ya awamu ya nne amesema watanzania wanapaswa kutambua kuwa rushwa haitokei tu serikalini bali hata sekta binafsi imeathirika na tatizo hilo.

“Rushwa bado ipo na si tu serikalini bali hadi katika sekta binafsi, tunafanya makosa  mara nyingi tunainyooshea vidole serikali. Rushwa ipo kote kwenye sekta ya umma na sekta binafsi”, amesema Utouh.

Amesema tatizo rushwa nchini limejikita zaidi kwenye biashara inayofanywa na serikali na sekta binafsi ambapo baadhi ya watumishi hupindisha taratibu za manunuzi ili kujipatia fedha isivyo halali.

“Tunapozungumzia rushwa duniani kote serikali zinafanya biashara kubwa na sekta binafsi hasa kwenye ununuzi wa huduma na bidhaa”, amesema Utouh na kuongeza kuwa sekta za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara na majengo ya mashirika ya umma zinakabiliwa na changamoto ya manunuzi.

“Kama ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya serikali, mara nyingi ni kupitia miamala hiyo ya manunuzi kunakozalisha vitendo vya rushwa kubwa nchini”,

Amebainisha kuwa mtazamo wa jamii dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka na mali ya umma umeendelea kuwa kichocheo cha rushwa kushamiri katika sekta mbalimbali nchini na kupotosha maana halisi ya uwazi na uwajibikaji.

“Jamii ya kitanzania bado inashabikia vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya madaraka na ukwepaji wa kodi”, amefafanua Utouh.

Hata hivyo, amesema vitendo vya rushwa vimepungua kwa kiasi kikubwa katika awamu ya tano lakini sio tafsiri kuwa uwajibikaji na uwazi wa matumizi ya serikali na urahisi wa upatikanaji wa huduma za umma ni dhamira ya viongozi wa serikali kukemea vitendo vya kifisadi.

“ Bado ni changamoto kusema moja kwa moja kama kushuka kwa viwango hivi kutokana na ongezeko la uwajibikaji ama ni uoga tu unaotokana na ukali wa serikali na viongozi kukemea rushwa au vimesababishwa na uwazi au urahisi wa upatikanaji wa huduma za serikali. Tunachoweza kusema kwamba rushwa bado ipo”, amesema Utouh.

Kwa upande wake, Annastazia Rugaba kutoka taasisi ya Twaweza amesema,  “Wananchi wengi wanapenda kuona vitendo vya Rushwa vinatokomezwa nchini lakini wanachukizwa na uminywaji wa Demokrasia unaoendelea”.

Amesema serikali inapaswa kuheshimu misingi ya demokrasia na kuwapa wananchi uhuru wa kujieleza ili kuongeza uwajibikaji miongoni kwa viongozi wa sekta ya umma.

Serikali kupitia Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi  wa Umma na Utawala Bora, Mathias Kadungulile  amesema rushwa bado ni tatizo kwa nchi nyingi za Afrika na njia pekee ya kuitokomeza ni kuongeza uwajibikaji na uwazi wa matumizi ya serikali.

“Suala la Rushwa siyo la Tanzania peke yake ila dunia nzima. Katika bara la Afrika tatizo hili ni kubwa zaidi. Upo ushahidi wa kudhihirisha hali ambayo naamini mzee Utouh atalizungumza kwa upana kwa upana zaidi. Ni kweli kwamba rushwa ipo na uwajibikaji ukisisitizwa ndio utakaoipunguza. Hatusemi kuwa rushwa haipo ila tujitahidi kuipunguza.”, amesema  na kuongeza  kuwa,

“Jukumu la uwajibikaji na kupambana na rushwa hatuwezi kuiachia TAKUKURU peke yake. Tataweza kutokomeza rushwa kama sote tutashiriki katika mapambano haya. Nitoe rai kwenye taasisi za elimu za juu hapa nchini na taasisi za kiraia hapa tuendelee kusimamia uwajibikaji na kupambana na rushwa”.

Taasisi ya Wajibu ilanzishwa mwaka 2015 kwa ajili ya kukuza uwajibikaji na utawala bora hapa nchini. Taasisi ya Wajibu ina dira ya kusaidia uwepo wa usimamizi mzuri wa rasilimali za umma kwa manufaa ya wananchi wote na  dhima ya kuendelea kukua kama taasisi fika.

Taasisi hiyo haifungamani na upande wowote wa kisiasa, kidini ama kijamii pamoja na kusimamia uadilifu, usawa na uwajibikaji ambapo inaratibu mijadala na makongamano ya uwajibikaji na uwazi katika jamii.

Pia inafanya tafiti mbalimbali na inakusudia  kufanya utafiti wa fedha za mfuko wa vijana na wanawake zinazotolewa kwenye halmashauri mbalimbali nchini na  imejipanga kuendelea kutoa ripoti za uwajibikaji kwa mwaka 2018 kwa kushirikiana na kamati za kudumu za Bunge la Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *