Sh. 30 ya wakulima wa korosho kujenga vyoo, madarasa wilayani Tunduru

Jamii Africa

Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 umeweka wazi  majukumu ya wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi na serikali katika utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Majukumu ya wazazi katika waraka huo ni kugharamia masuala ya sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia kama vile madaftari, kalamu/penseli, na gharama za chakula kwa wanafunzi wa kutwa. Madhumuni ya wazazi kuchangia gharama kidogo ni kwasababu ruzuku inayotolewa na serikali kwa wanafunzi  haitoshelezi mahitaji yote ya wanafunzi na shule.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la HakiElimu (2017) juu Matokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Ada kwa Elimumsingi nchini Tanzania umebaini kuwa ruzuku ya wanafunzi iliyopokelewa na shule ilitofautiana kulingana na makundi ya shule. Kwa wastani, wakati shule za sekondari zilipata 13% zaidi ya kiasi tarajiwa cha Sh. 12,500 katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2016, shule za msingi zilipokea 7% pungufu ya kiasi kinachotarajiwa cha Sh.3,000.

Kwa muktadha huo ni muhimu kwa wazazi kuchangia gharama kidogo kwasababu elimu ni suala mtambuka lazima kila mdau afanye sehemu yake kuinua ubora wa elimu inayotolewa nchini.

Kwa upande mwingine, utayari wa wazazi kuchangia unaweza kutafsiriwa kama fursa kwa serikali kuhamasisha wazazi kuisadia serikali kugharamia elimu, ambayo inaweza kusaidia pia kutatua matatizo yanayotokana na elimu bila ada.

Mbali na kusaidia matumizi ya serikali kwenye elimu, michango ya wazazi pia inakuza hisia ya umiliki wa shule, kitu ambacho ni muhimu sana kwenye kuboresha ushiriki wa wazazi, uboreshaji wa miundombinu ya shule na hatimaye kuboresha kiwango cha ufaulu wa shule.

Kutokana na umuhimu wa kuchangia elimu, wakulima wa korosho katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma walikubaliana na uongozi wa Halmashauri yao kutoa shilingi 30 kwa kila kilo moja ya korosho inayouzwa ili kuchangia ujenzi wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu.

Ukusanyaji wa fedha hizo ulianza katika msimu wa uuzaji wa korosho wa mwaka 2017/2018 ambapo wakulima wote walikatwa fedha kwenye mauzo ya korosho ili kuwa sehemu ya kuinua kiwango cha elimu katika wilaya hiyo inayopatikana Kusini mwa Tanzania.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari na mawasiliano katika Halmshauri ya Tunduru, mfuko maalumu wa elimu uliundwa ambapo mpaka sasa zimekusanywa milioni 600.8 kutoka kwa wakulima wa korosho.

Akiwasilisha matumizi ya fedha hizo katika kikao cha baraza maalum la madiwani la kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa niaba ya Mkuregenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru Afisa Mipango wilaya, Rudrick Chale amesema fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto za elimu wilayani humo ikizingatiwa kuwa zimekuwepo kwa muda mrefu bila kupata suluhisho la kudumu.  Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru wakiwa kwenye kikao cha kupitisha  rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kilichofanyika hivi karibuni wilayani humo.

Amesema kuwa kati ya fedha zilizokusanywa elimu msingi wamepata milioni 359 na elimu sekondari wametengewa milioni 240 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu wilayani Tunduru.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera aliwataka madiwani ambao watapata mgawo wa fedha hizo kukamilisha miradi ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na vyoo kwa wakati ili kuwawezesha wanafunzi kusomea katika mazingira bora.

 "Nawataka madiwani msimamie miradi iliyopendekezwa na wataalamu wetu na tukumbuke hizi fedha ni za wananchi waliokatwa katika mazao yao hivyo tunaomba usimamizi wa pamoja kati ya madiwani na halmashauri ili kupunguza matatizo ya wanaolundikana kwenye vyumba vya madarasa", amesema Homera.

Amebainisha kuwa changamoto ya miundombinu ya shule katika wilaya hiyo ni kubwa na wanakusudia kujenga madarasa 70 katika awamu ya kwanza ya mpango huo ili kupunguza upungufu wa vyumba vya madarasa.

Naye mbunge wa Tunduru Kaskazini, Eng. Ramo Makani amesema, “ni vyema  kuona ni namna gani tunaweza kutumia mazao mengine ambayo yanalimwa wilayani Tunduru katika kuchangia mfuko wa elimu na tusiegemee tu kwa zao moja la korosho ili kuongeza wigo mpana wa kupunguza changamoto za elimu na kukuza Elimu kama mikoa mingine ambayo waliwekeza katika elimu”.

Pia akichangia rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 amesema changamoto kubwa ilibainishwa na wataalam ni ukosefu wa fedha, hivyo ni vyema madiwani kuwahamasisha wananchi kuendelea kulima kilimo chenye tija ili kuongeza uzalishaji na halmashauri kukusanya zaidi mapato kwasababu fedha za ndani ndio zenye uhakika wa kuendesha miradi ya maendeleo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *