Simba yagonga mwamba FIFA, Yanga yabaki na taji, Kagera na pointi zake

Daniel Mbega

NDOTO za Simba kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara ‘mezani’ zimegonga mwamba baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuitupilia mbali rufaa yake ya kupinga kunyang’anywa pointi na Kamati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) za mchezo wake na Kagera Sugar.

FikraPevu imeiona nakala ya barua ya FIFA kwa Simba iliyoandikwa jana Ijumaa, Mei 26, 2017 ikieleza kwamba haina mamlaka ya kutengua uamuzi ambao umefanywa na Shirikisho la Soka la nchi mwanachama.

Mohamed Fakhi wa Kagera Sugar

Hali hiyo imeifanya Yanga ibaki na ubingwa wake na Kagera Sugar nayo ibaki na pointi zake tatu na kuyeyusha ndoto za vijana wa Msimbazi za kutwaa ubingwa baada ya kuukosa kwa miaka mitano.

Simba na Yanga zimemaliza Ligi Kuu Tanzania Bara zikiwa zimefunga kwa pointi 68 kila moja, lakini Yanga imetwaa ubingwa kwa idadi kubwa ya mabao ambapo ilifunga mabao 57 na kufungwa manne, wakati Simba imefunga mabao 50 na kufungwa 17.

Barua hiyo ambayo FikraPevu inayo nakala yake inasema: “Tunakiri kupokea barua yenu ya tarehe 17 Mei 2017, ambayo Simba iliomba uamuzi wa FIFA kuhusiana na uamuzi uliotolewa na kamati ya nidhamu ya TFF kuhusu hadhi ya kadi za njano ya mchezaji wa Kagera Sugar Mohamed Fakhi.

“Kwa msingi huo, tungependa awali ya yote kueleza kwamba, kulingana na Ibara ya 108 ya FIFA Aya ya 1 ya Mwenendo wa Nidhamu (FDC), masuala ya nidhamu yapo katika kanuni kuu.

“Vivyo hivyo, Ibara ya 108 Aya ya 2 ya FDC inabainisha kwamba, uamuzi wowote unaofanywa na chama kutoka nchi mwanachama kwa mujibu wa sheria zinazokiongoza hauwezi kujadiliwa zaidi katika ngazi ya FIFA.

“Bila kuathiri maelezo ya hapo juu, tunachukua nafasi hii kuwajulisha kwamba, baada ya kupitia vielelezo vyote vilivyowasilishwa Simba SC na TFF, ilionekana kwamba hakuna mabadiliko yoyote yanayotakiwa kufanywa katika uamuzi wa kamati maalum ya TFF…” ilisema barua hiyo ambayo ilisainiwa na Marco Villiger, Mkurugenzi wa Nidhamu na Utawala na Jorg Vollmuller, Mkuu wa Masuala ya Sheria.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *