Steve Jobs wa Apple afariki dunia

Jamii Africa

Mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya kompyuta ya Apple Bw. Steve Jobs (56) amefariki dunia. Kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa na kampuni ya Apple Inc., Jobs amefariki siku ya Jumatano. Taarifa ya msiba huo mkubwa kwa kampuni ya Apple imesema kuwa “Bw. Jobs amefariki dunia leo.” Taarifa hiyo imeendelea na kusema kuwa “kutokana na akili yake, mapenzi yake na nguvu aliyokuwa nayo vilikuwa vyanzo visivyo kifani vya vitu mbalimbali alivyovibuni ambavyo vimebadilisha maisha yetu sisi sote”.

Taarifa hiyo ikizungumzia mchango mkubwa wa Jobs katika ulimwengu wa teknolojia imesema kuwa “dunia imenufaika sana na maisha ya Jobs. Mapenzi yake makubwa yalikuwa kwa mke wake Laurene na familia yake”.

Steve Jobs

Mtandao wa intaneti wa kampuni ya Apple umebadilisha ukurasa wake wa mbele kwa kuweka picha kubwa ya Bw. Jobs huku mwaka wake wa kuzaliwa na kufa vikiandikwa pembeni. Bw. Jobs alizaliwa Februari 24, 1955.

Akiwa na rafiki yake wa utotoni Steve Wozniak walianzisha kampeni ya Apple mwaka 1976 kwenye gereji ya wazazi wake kwa kuuza kile kinachotajwa kama kompyuta ya kwanza kwa matumizi ya kawaida ya watu. Modeli hiyo ya kwanza ilijulikana kama Apple II. Ubunifu wake na ujuzi wake wa mambo ya kompyuta umefanya baadhi ya watu kumlinganisha na Mmarekani mwingine ambaye ubunifu wake umebadilisha kabisa dunia Thomas Edison, mgunduzi wa umeme kama tunavyoujua sasa.

Akiwa kijana mdogo aliacha masomo ya chuo kikuu na kuingi kwenye biashara na alipofikisha miaka 25 alikuwa tayari milionea na akiwa na miaka 26 alipamba ukurasa wa jarida maarufu la Times.

Mchango wake katika ulimwengu wa teknolojia utamjada milele kwa kumhusisha kwa ugunduzi na matuzi ya kompyuta, Ipod, Ipad na teknolojia mbalimbali za programu za kompyuta ambazo zimeweza kubadilisha sana maisha ya watu.

Pamoja na mafanikio yake kwenye kampuni aliyoshiriki kuianzisha ya Apple alilazimishwa kuondoka Apple mwaka 1986 baada ya mgongano wa madaraka na wenzake. Hata hivyo kuondoka kwake Apple kuliacha ombwe la ubunifu na uongozi na kufanya kampuni hiyo kuwa matatani kwa muda mrefu. Alienda na kuanzisha kampuni ya NExt Computer ambayo haikufanya vizuri sana kama alivyotarajia. Hata hivyo mwaka 1996 kampuni ya Apple iliinunua kampuni ya Jobs na hivyo kumrudisha Jobs Apple na vile vile kumrudisha kama Afisa Mtendaji Mkuu.

Alipoitambulisha iPod mwaka 2001 alifanya uwe mwisho wa Walkman na kaseti za kusikiliza mtu akiwa unatembea. Kimashine kile cheupe cha muziki kikawa ndio mwanzo wa kurudi kwa nguvu kwa mapuni ya Apple chini ya Jobs.

Jobs ameacha mke na watoto wanne pamoja na dadake.

Mjadala juu ya kifo cha Steve Jobs unaendelea katika JamiiForums kupitia kiunganishi hiki

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *