Taifa Stars imefanya vizuri Cosafa, lakini si wakati wa kubweteka

Daniel Mbega
Himid Mkami of Tanzania challenged by Napo Matsoso of Lesotho during 2017 Cosafa Castle Cup match between Tanzania and Lesotho at Moruleng Stadium in Rustenburg on 07 July 2017 ©Samuel Shivambu/BackpagePix

TIMU ya Taifa, Taifa Stars, jana usiku Ijumaa, Julai 7, 2017 ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Kombe la Castle yanayoandaliwa na Baraza la Soka kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa) baada ya kuifunga Lesotho kwa mikwaju ya penalti 4-2.

Stars, ambayo inatarajiwa kurejea usiku wa kuamkia kesho Jumapili Julai 9, inatakiwa kuangalia matokeo mazuri katika mezi zijazo na siyo kubweteka na ushindi huo.

Nahodha wa Taifa Stars, Himid Mkami, akimiliki mpira huku akizongwa na mchezaji wa Lesotho, Napo Matsoso wakati wa mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa Kombe la Cosafa Castle kwenye Uwanja wa Moruleng mjini Rustenburg jana Ijumaa, Julai 7, 2015. Stars ilishinda kwa penalti 4-2.

Timu hiyo ambayo itarejea kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda itaondoka tena kwenda Mwanza Jumatatu saa 12.00 jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Fast Jet ili kuweka kambi kujiandaa na mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) dhidi ya Rwanda unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Julai 15, 2017.

Ni kweli kwamba, katika michezo tisa ya kimataifa iliyocheza mwaka huu, Stars imefanya vizuri kwa kushinda mitano, kutoka sare mitatu na kufungwa mmoja wa nusu fainali za Cosafa dhidi ya Zambia.

Mshindi wa tatu

Katika mchezo huo wa kutafuta mshindi wa tatu uliofanyika kwenye Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini, timu hizo zilitoka suluhu katika muda wa dakika 90, hivyo kuingia hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti.

Himid Mao, Abdi Banda, Simon Msuva na Raphael Alpha waliifungia Taifa Stars penalti huku mkwaju uliopigwa na Shiza Kichuya ukigonga mwamba wa juu, lakini Lesotho walikosa mapigo mawili – moja likiwa limegonga mwamba wa pembeni na penalti ya nahodha wa Lesotho, Thapelo Mokhehle, ikipanguliwa na kipa Said Mohammed.

Penalti za Lesotho katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Romeo Kasengele wa Zambia, aliyesaidiwa na Thomas Kusosa wa Zimbabwe na Helder de Carvalho wa Angola, zilifungwa na Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle.

Kwa ushindi huo, Taifa Stars imetwaa medali za dhahabu pamoja na kitita cha Dola za Marekani 10,000 wakati Lesotho wamepata dola 8,300.

Bingwa wa michuano hiyo atakayepatikana kesho Jumapili, Julai 9, 2017 baina ya Zambia na Zimbabwe katika Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg atapata Dola za Marekani 42,000 na mshindi wa pili Dola za Marekani 21,000.

Taifa Stars, ambayo ilikuwa Kundi A pamoja na Angola, Mauritius na Malawi, ilikwenda kushiriki mashindano hayo ikichukua nafasi ya Comoro ambayo ilijitoa.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kushiriki mashindano hayo, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1997 na ikashiriki tena mwaka 2015.

Kikosi cha Stars kilichokuwa Afrika Kusini chini ya kocha mzalendo, Salum Shabani Mayanga, kiliundwa na makipa Aishi Salum Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Yanga) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia walikuwa Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Yanga) wakati upande wa kushoto walikuwa Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans).

Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia ni nahodha Himid Mao Mkami (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.

Aidha, viungo wa kushambulia ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Yanga), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba) huku washambuliaji wakiwa Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).

Harakati zake

Taifa Stars ilianza harakati zake Juni 25, 2017 kwa kuikabili Malawi kwenye Uwanja wa Moruleng ambapo iliichapa mabao 2-0 yaliyopachikwa na Salim Abdallah.

Katka mechi yake ya pili Juni 27, Tanzania ikailazimisha suluhu Angola, ambayo ni bingwa mara tatu wa mashindano hayo, katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace.

Juni 29, 2017 mshambuliaji Simon Msuva aliipeleka Stars robo fainali baada ya kuisawazishia bao katika mechi dhidi ya Mauritius iliyomalizika kwa matokeo ya bao 1-1 katika Uwanja wa Moruleng.

Mauritius ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Kelvin Perticots aliyefunga katika dakika ya 67 kabla ya Simon kuisawazishia Taifa Stars katika dakika ya 68.

Matokeo hayo yakaifanya Stars imalize ikiwa kinara wa kundi lake ikiwa na pointi 5 sawa na Angola, lakini yenyewe ilifunga mabao matatu wakati Angola ilifunga bao moja tu.

Katika robo fainali ikakumbana na wenyeji Afrika Kusini na kwenye mchezo wao uliofanyika katika Uwanja wa Royal Bafokeng Julai 2, 2017, ikawashangaza wengi baada ya kushinda kwa bao 1-0 na kutinga nusu fainali.

Shujaa wa Stars alikuwa Elias Maguri ambaye alipachika bao hilo pekee katika dakika ya 18 kwa shuti la mahesabu akiunganisha pasi ndefu ya kiungo Muzamil Yassin, Stars ikitoka kushambuliwa.

Kwenye nusu fainali ilikumbana na Zambia, ambapo licha ya kuongoza, ikajikuta ikifungwa mabao 4-2 na kuyeyusha ndoto zake za kutinga kwa mara ya kwanza hatua ya fainali za michuano hiyo.

Hiyo ilikuwa mechi yao ya 31 katika historia, ambapo katika mechi 30 zilizopita za mashindano mbalimbali, ambapo Tanzania imemshinda mara tano tu huku Zambia ikishinda mechi 16 na mechi tisa zikiwa za sare.

Karia aipongeza Stars

Katika hatua nyingine, Kaimu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ameipongeza Taifa Stars kwa mafanikio ya kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Castle la Cosafa.

“Haya ni matunda ambayo tunayaota kila wakati kwa timu kupata ushindi. Tunawapongeza wachezaji, benchi nzima la ufundi likiongozwa na Kocha Salum Mayanga, pamoja na watendaji wote kwa mafanikio ya timu yetu ya Taifa Stars,” alisema Karia.

Alisema timu hiyo imeonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kutafuta mafanikio na ana imani kwamba Tanzania itashiriki michuano mingi ya kimataifa kwa kuwa ina wachezaji wengi makinda huku TFF ikiendelea kuwakuza wengine kwa ajili ya kutimiza ndoto za furaha ya Watanzania kwa sasa na hapo baadaye.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *