Taifa Stars na Rwanda, Mwanza patakuwa hapatoshi wikiendi hii

Daniel Mbega

IKIWA imetoka kulamba Dola za Marekani 10,000 kwa kushinda nafasi ya tatu katika Mashindano ya Kombe la Castle la Baraza la Soka kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa), Taifa Stars sasa inaelekeza nguvu zake kukabiliana na timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi, katika mashindano ya kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).

Stars itahitaji ushindi katika mechi hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wikiendi hii ili kujiwekea mazingira mazuri ya kushiriki kwa mara ya pili fainali hizo baada ya kufanya hivyo mwaka 2009.

Kikosi cha Stars kilichokuwa Afrika Kusini kilicho chini ya kocha mzalendo, Salum Shabani Mayanga, hakijabadilika sana kwani bado kinao makipa Aishi Salum Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Yanga) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia walikuwa Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Yanga) wakati upande wa kushoto walikuwa Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans).

Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia ni nahodha Himid Mao Mkami (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.

Aidha, viungo wa kushambulia ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Yanga), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba) huku washambuliaji wakiwa Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kukutana na Rwanda katika mashindano ya Afrika ukiachilia mbali mashindano ya Kombe la Chalenji, ingawa ni mara yao ya nane kukutana.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Rwanda imekutana na Tanzania mara sita katika Kombe la Chalenji na Tanzania imeshinda mara moja tu na kufungwa mechi nne, huku wakitoka sare mara moja.

Julai 28, 1999 ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Rwanda na Tanzania (ikicheza kama Kilimanjaro Stars kwa kuhusisha wachezaji wa Tanzania Bara pekee) kumenyana katika mashindano hayo tangu Rwanda ilipojiunga na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali, Tanzania ilicheza na timu ya kwanza ya Rwanda (Amavubi) katika Kundi A ambapo zilitoka suluhu, hivyo wenyeji wakaongoza kundi hilo na Taifa Stars ikashika nafasi ya pili, ambapo haikufanya vizuri baada ya kuishia kwenye robo fainali.

Desemba 17, 2001 Tanzania ilipangwa Kundi la 2 na kufuzu robo fainali ambako ilikumbana na Rwanda B lakini ikakubali kipigo cha mabao 2-1. Rwanda ilifunga bao katika dakika ya kwanza tu kupitia kwa Witakenge Jeannot kabla ya Yussuf Macho ‘Musso’ kusawazisha katika dakika ya 5, lakini Kombi akaipatia Rwanda bao la ushindi dakika ya 56.

Desemba 11, 2002 jijini Mwanza, Kilimanjaro Stars ilikumbana na Rwanda katika nusu fainali ya mashindano hayo na safari hii ikafanikiwa kuichapa Amavubi mabao 3-0 kupitia kwa Abdul Mtiro dakika ya 44, Salvatory Edward dakika ya 69 na Athumani Machupa dakika ya 83.

Vikosi vya siku hiyo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba vilikuwa; Tanzania: Juma Kaseja, Mecky Mexime, Alphonce Modest, Costa Victor, Boniface Pawasa, Selemani Matola, Ulimboka Mwakigwe, Salvatory Edward, Athumani Machupa, Emmanuel Gabriel (Zuberi Katwila 74), Abdul Mtiro (Joseph Mwanakusha 69).

Rwanda: Ishimana Claude, Makara Pappy, Habimana Kheri, Lita Mana (Mukerezi Marie 68), Eric Nshimiyamana (Muhayimana Theoneste 46), Jean-Paul Habyarimana, Kamanzi Elias, Sibomana Abdul, Witakenge Jeannot, Jimmy Gatete (Nkuzingowia Rama 75), Milly Hassan.

Mwaka 2004 Tanzania na Rwanda zilipangwa Kundi A wakati mashindano hayo yalipofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, kundi ambalo lilikuwa na wenyeji pamoja na Burundi na Zanzibar.

Lakini safari hii Tanzania ilitia aibu baada ya kufungwa mechi zote nne huku ikikubali kipigo cha aibu cha mabao 5-1 kutoka kwa Rwanda Desemba 19.

Licha ya kuundwa na wachezaji mahiri kama Boniface Pawasa, Juma Kaseja, Mecky Mexime, Shaaban Kisiga, Athuman Machupa, Christopher Alex, Said Sued, Ahmed Haidery, Nurdin Bakari, Jumanne Ramadhani, Athuman Idd, Ally Miluno, Juma Jabu, Julius Mrope, Nizar Khalfan, Omari Matuta, Patrick Mangunguru, Hassan Bwaza, Ulimboka Mwakingwe, Victor Costa ikiwa chini ya kocha John Simkoko, timu hiyo haikuweza kufurukuta hata kidogo kwenye mashindano ya mwaka huo.

Katika mashindano ya mwaka 2005, Tanzania ilipangwa kundi A pamoja na Rwanda mjini Kigali ambapo pia kulikuwa na timu za Zanzibar, Burundi na Eritrea.

Kilimanjaro Stars ilijikuta ikipata kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Rwanda Desemba 6, ambapo mabao ya Amavubi yalifungwa na Jean Lomani aliyepachika mawili na Jimmy Gatete, wakati lile la Stars lilifungwa na Sammy Kessy.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukumbana kwenye mashindano hayo ilikuwa wakati wa robo fainali Desemba 5, 2006 jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo Rwanda ilishinda 2-1 huku Stars ikifaidika na bao la kujifunga la beki Elias Uzamukunda katika dakika ya 26. Mabao ya Rwanda yalifungwa na Robert Ujenza dakika ya 41 na Jeannot Witakenge kwa penalty dakika ya 55.

Kilimanjaro Stars wakati huo iliundwa na wachezaji wafuatao: Makipa – Juma Kaseja (Simba), Sudi Slim (aka Sued Suleiman?) (Mtibwa); walinzi – Saidi Morad (Ashanti), Idrissa Rajabu (Moro United), Yasini Juma (Pangolini), Dickson Daudi (Mtibwa), Juma Rajabu (Kagera), Erasto Nyoni (Burundi).

Viungo walikuwa – Adam Matunga (AFC), Hussein Sued (Ashanti), Meck Michael (Under-17), Amir Maftah (Mtibwa), Bantu Admin (Polisi Dodoma), Mrisho Ngassa (Kagera Sugar), Kigi Mkasi (Rolling Stone); washambiliaji – Danny Mrwanda (Simba), Jerrison Tegete (Makongo), Gasper Simon (Ruvu Shooting) na kocha alikuwa John Simkoko aliyekuwa akiinoa Polisi Morogoro.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *