Tanga: Wapewa risiti bandia wakinunua dawa jirani na Hospitali ya Bombo

Jamii Africa

BAADHI ya maduka ya dawa za binadamu jijini Tanga wanakaidi agizo la serikali la kutumia mashine za kielektroniki (EFD) kutoa risiti kwa wateja wao.

Kukaidi agizo hilo na kutoa risiti ambazo hazijathibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kunaikosesha mapato serikali.

Mashine za EFD husaidia kudhibiti upotevu wa fedha za serikali – kodi, zinazotokana na kufanya biashara.

FikraPevu imebaini kuwa duka la dawa la Amboni Pharmacy lililopo ndani ya majengo ya Chuo cha Uuguzi cha Hospitali ya Bombo, halina risiti za EFD, hatua ambayo inasaidia kupotea kwa mapato halali ya kodi.

FikraPevu pia imebaini kuwa risiti zinazotolewa Amboni Pharmacy zina anwani ya Savannah Pharmacy yenye anwani ya Bamaga Area, Barabara ya Bagamoyo, Sanduku la Barua 33239, Jijini Dar es Salaam.

Hii ni risiti aliyopewa mteja baada ya kununua bidhaa.

Kadala, aliyejitambulisha kwa jina hilo moja, kuwa ni mfamasia wa duka la dawa la Amboni, lililopo pembeni mwa geti la Hospitali ya Rufaa ya Bombo, ameiambia FikraPevu kuwa vitabu halali vya mauzo vyenye anwani ya duka la dawa la Amboni viliisha, hivyo wamepeleka maombi kiwandani ili vitabu husika viweze kuchapwa.

“Tuliishiwa vitabu vyenye nembo ya Amboni Pharmacy Limited, lakini Mkurugenzi wa Amboni na Savvanah ni yuleyule, kwa hiyo tumeona tutumie vya Amboni na sisi mashine ya kielektroniki hatujawahi kupata tangu tupeleke maombi TRA, kwa hiyo bado tunatumia mfumo wa zamani,” alisema Kadala.

Aidha, hakufafanua kama vitabu vya mkoani Tanga hutumika kukagua hesabu zake jijini Dar es Salaam, kwa sababu licha ya mmiliki kuwa mmoja hizo ni biashara mbili tofauti.

Geti la kuingilia Hospitali ya Rufaa ya Bombo jijini Tanga.

Tunachokijua FikraPevu

Ukwepaji kodi wa kutoa stakabadhi ya aina moja kwa biashara zaidi ya moja zenye leseni tofauti huku wafanyabiashara wengine wakitoa stakabadhi bandia, umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu kwa misingi ya kuikosesha serikali mapato, hatua iliyoilazimu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha mashine za EFD.

Ingawa mashine hizo zilileta utata baada ya wafanyabaishara kuzigomea kwa maelezo kuwa zinauzwa ghali, lakini hata pale serikali ilipoamua kutatua tatizo hilo kwa kuzigawa bure, bado ziliendelea kulalamikiwa kwamba hazifai.

Aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Philip Mpango, ambaye sasa ndiye Waziri wa Fedha na Mipango, alitangaza mwaka 2015 kwamba mashine hizo hazitauzwa na kuagiza wafanyabiashara nchini kupewa bure, huku akisisitiza kwamba kila anayenunua bidhaa ni lazima adai risiti na anayeuza lazima atoe risiti.

FikraPevu inatambua kwamba, kama mfanyabiashara atanunua bidhaa za jumla na kupewa risiti na akauza bidhaa hizo kwa kutoa risiti, ili serikali ipate kodi.

Inaelezwa kwamba, hatua ya serikali kufanikiwa kukusanya kiasi cha Shs. 1.31 trilioni ikiwa ni asilimia 101 ya malengo kwa mwezi Machi 2016 ilitokana pia na matumizi ya mashine hizo za EFD.

Mkazo wa serikali katika kudhibiti ukwepaji kodi uliweza kubaini kampuni nne ambazo zilidaiwa kukwepa kodi ya Shs. 29.2 bilioni kwa kutumia mashine hizo za EFD ambapo taarifa ya pamoja baina ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na TRA ilizitaja kampuni hizo kuwa ni SKOL Building Material Ltd, Farm Plant (T) Limited, A.M. Steel & Iron Mills Limited na A.M. Trailer Manufacturers Limited.

Kampuni hizo zilidaiwa kwamba zilikuwa zikinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na kuzitumia risiti hizo kudai marejesho ya VAT bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na muhusika, kitendo ambacho kiliinyima Serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria.

Mwezi Juni 2016 TRA na Takukuru walimkamata mfanyabiashara Mohammed Mustafa Yusuf Ali kwamba alikuwa anaiba kati ya Sh. 7-8 milioni kila dakika kwa kutoa risiti feki za EFD, wizi ambao ulielezwa kwamba ulifanyika kati ya mwaka 2010 na 2014, hivyo kuikosesha serikali matrilioni ya shilingi.

Udanganyifu katika mapato ya umma na utoaji wa risiti feki umekuwa ukitokea hati katika ngazi za chini katika jamii ambapo Julai 3, 2016 mkutano wa wananchi wa Mtaa wa Onjucatian, Kata ya Sokoni One jijini Arusha ulivunjika baada ya viongozi kushindwa kusoma taarifa ya mapato na matumizi huku wakionyesha risiti bandia za vitu vilivyodaiwa kununuliwa kwa michango ya wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *