SERIKALI ya Tanzania, Burundi na Rwanda zimetiliana saini mkataba wa maridhiano ya pamoja katika kusimamia mradi mpya na mkubwa wa kuzalisha umeme, kwenye maporomoko ya maji katika Mto Rusumo uliopo Mkoa wa Kagera hapa nchini.
Mradi huo uliopo chini ya Uratibu wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (EAC), umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), na unatarajia kuzalisha megawati 90 za nishati ya umeme, na kwamba kila nchi itapata megawati 30 katika mradi huo mkubwa.
Mkataba huo wa pamoja ambao umetiliwa saini jijini Mwanza, umelenga kuchochea zaidi ukuaji wa maendeleo na kupunguza tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo wanannchi wan chi husika watanufaika na umeme huo.
- Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, William Ngeleja
Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, William Mganga Ngeleja alimwambia mwandishi wa habari hizi leo kwamba, nchi hizo zimefikia makubaliano hayo kwa lengo na la pamoja katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa umeme.
Alisema, mradi huo ni muhimu sana kimaendeleo ya kisekta katika nchi hizo tatu, na kwamba hiyo ni hatua mojawapo muhimu katika kuelekea kupunguza kabisa tatizo la umeme ambalo limekuwa changamoto kubwa.
“Tumetiliana saini mkataba wapamoja kuanza kusimamia mradi wa umeme katika Mto Rusumo. Huu mradi utakuwa na megawati 90 na kila nchi itapata umeme wa megawati 30.
“Tunaamini sana kwamba umeme huu wa Rusumo utachochea sana ukuaji wa maendeleo ya kisekta katika nchi zetu za Tanzania, Rwanda na Burundi”, alisema Waziri Ngeleja, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mkoani Mwanza (CCM).
Mkataba huo wa pamoja, umesainiwa na Mawaziri wa nchi hizo wanaoshughulikia masuala ya Nishati ambao ni Waziri Ngeleja wa Tanzania, Waziri wa Nchi, Maji na Nishati wa Rwanda, Emmanuel Isumbingabu pamoja na Waziri wa Burundi anayeshughulikia masuala ya Nishati, Maji na Madini, Manirakiza Come.
Waziri Ngeleja aliyataja maeneo hapa nchini yatakayonufaika na mradi huo wa umeme utokanao na maporomoko ya Mto Rusumo, kuwa ni pamoja na wilaya ya Sengerema na Geita (Mwanza), Kibondo na Kasulu (Kigoma), pamoja na maeneo ya Mkoa wa Kagera.
Hata hivyo, Waziri huyo wa Nishati na Madini alibainisha kwamba, tayari wamempa muda wa siku 45 mhandisi mshauri kuhakikisha ameandaa taarifa inayoonesha jinsi wananchi watakavyofidiwa ambao wanatarajiwa kupisha mradi huo.
Naye Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Burundi, Come pamoja na Waziri wa Rwanda anayeshughulikia Maji na Nishati, Isumbingabu kwa pamoja walieleza kwamba mradi huo utazinufaisha sana nchi zao, na kwamba ni vema nchi hizo zikajenga umoja wa kushirikiana katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo.
“Tumefurahi sana kufikia hatua hii nzuri ya kimaendeleo. Lakini tusikomee kwenye mradi huu wa umeme Rusumo, tushirikiane pia na mahala pengine pazuri pa kazi”, alisema Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Burundi.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza