TRA yaja na kanuni kudhibiti utoroshaji wa fedha nje ya nchi

Jamii Africa
BIASHARA: TRA yaja na kanuni za kudhibiti utoroshwaji wa fedha pamoja na kuiepusha nchi na kashfa za matukio ya utakatishaji fedha. Wananchi wanaosafirisha fedha taslimu zaidi ya milioni 22.5 (Dola 10,000 za Kimarekani) kwenda nje ya nchi watapaswa kujaza fomu yenye maelezo kuhusu fedha hizo Hatua hiyo ya TRA ambao wamepewa nguvu kisheria kusimamia zoezi hilo inakuja mwezi mmoja baada ya serikali kuandaa na kuzipitisha kanuni hizo za kudhibiti usafirishaji wa fedha kinyume na sheria. Akizungumza hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa warsha ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Onesmo H. Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizi, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wananchi wanaosafirisha fedha taslimu zaidi ya milioni 22.5 (Dola 10,000 za Kimarekani) nje ya nchi kujaza fomu yenye maelezo kuhusu fedha hizo ili kuiepusha nchi na matukio ya utakatishaji fedha.

Sheria ya Kudhibiti Fedha Haramu ya mwaka 2006, sura 423 na kanuni zake inasema mtu yeyote anayetaka kusafirisha fedha anatakiwa kutoa taarifa ya kiasi cha fedha taslimu na hati za malipo zinazosafirishwa kuingia au kutoka nje ya nchi.

Taarifa kwa wananchi iliyotolewa na  Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru, George I. Mnyitafu imeeleza kuwa TRA wanatekeleza sheria ya kudhibiti fedha halamu na kuhakikisha nchi inakuwa salama dhidi ya vitendo vyote vya kuhujumu uchumi.

“TRA inautaarifu umma kuwa, kuanzia tarehe 01 Oktoba 2017, msafirishaji yeyote wa fedha taslimu au hati za malipo zinazofikia kiwango kilichotajwa na kanuni hizi atalazimika kutoa taarifa kwa kujaza fomu zitakazopatikana kwa maafisa forodha mipakani” inaeleza taarifa hiyo.

Sheria hiyo imeipa Mamlaka ya Mapato Tanzania mamlaka ya kusimamia utoaji wa taarifa kuhusu fedha zinazosafirishwa kuingia au kutoka nchini.

Usafirishaji wa fedha taslimu au hati za malipo (Bearer Negotiable Instruments) zinazofikia au kuzidi dola za kimarekani 10,000 (elfu kumi) au fedha nyingine yoyote yenye thamani sawa na hiyo, iwapo fedha au hati hizo  zitasafirishwa kwa njia ya makontena ya kubebea mizigo, vifurushi na  mtu yeyote anayesafiri akiwa nazo au katika mizigo anayoambatana nayo au katika chombo cha usafiri.

TRA imewataka watu wanaosafirisha fedha kutoa taarifa sahihi za fedha zinazosafirishwa ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria endapo mtu atabainika ametoa taarifa za uongo. Pia sheria hiyo inakusudia kuweka utaratibu mzuri wa kusafirisha fedha na kuliepusha taifa na utakatishaji fedha na

“Kutotoa taarifa au kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu usafirishaji huo fedha au hati za malipo ni kosa kisheria. Utaratibu huu haukusudii kuzuia usafirishaji wa fedha taslimu na hati za malipo kuingia au kutoka nchini”, inaeleza taarifa hiyo.

Serikali yaandaa Kanuni za Usafirishaji wa Fedha

Hatua hiyo ya TRA ambao wamepewa nguvu kisheria kusimamia zoezi hilo inakuja mwezi mmoja baada ya serikali kuandaa na kuzipitisha kanuni hizo za kudhibiti usafirishaji wa fedha kinyume na sheria.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa warsha  ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Onesmo H. Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizi, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.

“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi”,

  “Wahalifu pamoja na mambo mengine, wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo mipakani” Alisisitiza Makombe.

 Utakatishaji Fedha Halamu

 Utakasishaji wa Fedha Haramu ni shughuli au vitendo vyenye lengo la kuficha ukweli au asili ya fedha au mali iliyotokana na uhalifu. Fedha halamu (Money Laundering) ni fedha ambayo haijapatikana kihalali  na kuingizwa kwenye mzunguko halali au kawaida wa fedha.

Mfano pesa iliyopatikana kwa kuuza mihadarati, madawa ya kulevya au uharamia ni fedhaa haramu (dirty money). Pesa hii iliyopatikana kiharamia ukiingiza kwenye mzunguko wa pesa kwa kununua biashara halali, kujenga nyumba au kuweka kwenye benki  hapo unakuwa umehusishwa na kosa la kutakatisha pesa.

Fedha hizo pia husafirishwa kwa njia zisizo halali ambapo huathiri uchumi wa nchi na kusababisha mfumko wa bei za bidhaa mbalimbali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *