Ni mengi yamekuwa yakizungumzwa juu ya changamoto zinazozikumba shule za kata zilianzishwa chini ya serikali yetu ya awamu ya nne. Pamoja na utetezi unaofanywa na wanasiasa wa chama tawala juu ya kuhalalisha uwepo wa shule za kata, mpaka kufikia baadhi ya wabunge kuhalalisha wanafunzi wa shule hizo kupata daraja sifuri wakidai kuwa ni bora hao waliopata sifuri kuliko watoto ambao hawakuweza kupata fursa ya kusoma.

Binafsi naungana na watanzania wengi wanaosikitishwa na mwenendo mbovu wa shule zetu za kata ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukichangiwa na siasa chafu zinazoingilia hata taaluma za watu. Siamini kuwa viongozi wetu na wataalamu wa sera; ambao ni washauri wa serikali; hawakuwa na muda wa kutosha kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa maagizo ya utekelezwaji wa mpango huu wa elimu.

Dhamira ya serikali inashindwa kufahamika juu ya mpango huu. Kama sehemu ya wananchi makini wanaoweza kuhoji mipango kama hii,  nimekuwa nikijiuliza je, serikali ilitaka kuwa na shule nyingi sana, zenye changamoto nyingi na kupelekea watoto wa maskini kufeli sana kwa kuwa watoto wa waheshimiwa husoma shule bora zaidi? Je, serikali ilitaka kuwa na wanafunzi wengi zaidi wanaopata fursa ya kupata elimu bora ya sekondari karibu na maeneo wanayotoka?  Kuna maswali mengi kila mtu aweza kujiuliza.

Ikiwa nia ya serikali yetu ilikuwa kuboresha elimu kwa kuhakikisha wahitimu wengi zaidi wanaomaliza elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari basi hapakuwa na haja ya kuwa na shule za kata katika kila sehemu ya nchi yetu. Unapozungumzia kata ukiwa Dar es salaam ni tofauti sana na neno kata katika baadhi ya wilaya za vijijini, hiki ndicho kitu ambacho serikali yawezekana haikukigundua katika mpango wake wa awali. Tofauti hii ndio inayopelekea upungufu wa walimu, maabara, maktaba, mazingira rafiki kwa walimu na wanafunzi, pamoja na changamoto nyinginezo.

Mfano halisi ni katika wilaya ya Tandahimba ambayo kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi Jumapili la Januari 30, 2011, wilaya hiyo ina shule za sekondari 26, walimu wa hisabati ni wawili tu wilaya nzima, aidha kwa mujibu wa gazeti hilo, ni shule nne tu kati ya ishirini na sita ndizo zina walimu wa masomo ya sayansi na pia katika matokeo ya kidato cha nne wanafunzi 1,164 kati ya wanafunzi 1,499 walifeli na kwamba hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la kwanza au/na la pili katika wilaya nzima.

Kutokana na taarifa hizi, siamini kama kulikuwa na haja sana ya kuwa na shule za kata katika wilaya kama hizi na badala yake tungekuwa na taasisi kubwa za jumuiya za elimu za kitaifa ambazo zingeweza kuchukuwa wanafunzi kama kama elfu mbili na zaidi, kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, katika taasisi hizi kungeelekezwa rasilimali zote za elimu za wilaya na hata kupata mgawo wa ruzuku kutoka serikalini, wanafunzi na walimu kutoka pande mbalimbali za taifa wangekutanishwa, kungewekwa miundombinu yote muhimu na ya  kitaasisi, makazi bora ya walimu, madarasa ya kutoa kozi za kujiendeleza kwa walimu, zahanati, maduka kwa ajli ya  kununua mahitaji yao mbalimbali ,miundombinu ya mawasiliano ya teknohama, na vingine vingi. Kwa hakika hakuna walimu ama wanafunzi wangepata usumbufu katika mazingira kama hayo na kiwango cha elimu nchini kingekuwa kwa kasi.

Kinachoonekana hapa ndicho kinachojitokeza hata katika ngazi ya vyuo vikuu ambapo wanasiasa wetu wanajipatia sifa kuona kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na vyuo vingi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wakati ambapo tulipaswa kuwa na chuo kimoja cha kitaifa na vingine vikibaki kama vyuo vishiriki kwa sababu unaweza ukakuta wanafunzi wanodahiliwa kwenye vyuo vyetu vyote vikuu  nchini ni ndogo sana ikilinganishwa na wanafunzi wanaodahiliwa katika vyuo vya nchi za wenzetu kama ilivyo kwa chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda.

Kwakuwa tumejifunza kutokana na makosa tuliyoyafanya katika utekelezwaji wa mpango wa shule za kata, napenda kutoa  pendekezo  kuwa ni lazima  tujue kama lengo letu ni kuongeza idadi ya shule ama kuongeza fursa kwa vijana waendao shule. Ni muhimu sana kwa taifa letu kuwa na wasomi kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji/mtaa, kata, tarafa na kadhalika lakini si muhimu wala lazima kuwa na shule katika ngazi zote hizo.

Ni muhimu turudishe mitihani muhimu kama ule wa kidato cha pili na darasa la nne uendelee kwani ilikuwa ikitumika kama kipimo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na pia kabla hatujatapeleka shule  shule za ‘A level’ kwenda katika kata. Pia ni lazima tujiulize; Je, kutakuwa na walimu wa kutosha? Maktaba,vitabu, maaabara?  Na pia kwanini tusifanye maboresho na upanuzi katika shule ambazo zipo kabla ya kuanza ujenzi kama ilivyofanyika kwenye shule za kata?

Hayo na mengi yatatusaidia kuelewa kwamba tunachokilenga ni fursa ya elimu bora kwa wanafunzi wote wa kitanzania na sio shule zilizo nyingi zaidi zisizokuwa na kiwango kinachotakiwa.


Imeandikwa na Costantine Deus Shirati

Simu: +255 717 492 023

Email: lukale8@yahoo.com

Blog: http:/costashirati.wordpress.com

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

One thought on “Tunahitaji wasomi kila kata, si shule kila kata”
  1. Nina mawazo yanayofanana na yako, mimi naona pia serikali haijaonesha nia halisi ya kufanya maboresho. Kwa mfano serikali iliahidi kuleta pesa mashuleni ifikapo tarehe 31 January.

    Kwa mujibu wa makubaliano kati ya Serikali na Benki ya Dunia ambayo inafadhili awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari serikali iliahidi kufikisha kwenye kila shule ya sekondari nchini Tanzania asilimia 40 ya fedha za ruzuku ya kuboresha mazingira ya kusomea ifikipo mwisho wa January 2011. Fedha hizo—asilimia 40%- ni sawa na Tshs 10,000 ambazo kila shule ingezitumia kufanya manunuzi muhimu kwa ajili ya mwaka wa masomo ambao ulikuwa ndio unaanza.

    Ufuatiliaji uliofanywa na marafiki wa elimu na wananachi sehemu mbalimbali nchini, na kuratibiwa na HakiElimu, Policy Forum na Twaweza umegundua kuwa asilimia 93 ya shule hazijapata pesa hadi hivi sasa, na zile zilizopata zimepata kati ya Tsh 146/- na 916/- tu kwa mwanafunzi. Kumbuka ahadi ilikuwa ni kupeleka TShs 10,000/- kwa kila mwanafunzi!

    Haijulikani kama hii pesa iliyofika ni kweli ile ya mwaka 2011 ama ni mabaki ya liyotakiwa kuwa yamefika mwaka 2010. Kilicho wazi ni kuwa shule za sekondari zimeanza muhula wa masomo zikiwa na pesa kidogo sana toka serikalini kwa ajili ya kufanya manunuzi ya kuboreshea mazingira ya kufundishia na hivyo kuongeza kiwango cha elimu inayotolewa.

    Tujiulize je, hizo pesa zingine zitafika lini, je kuna ahadi gani ya kuhakikisha ruzuku kamili ya Tshs 25 inafika mashuleni kwa wakati?

Leave a Reply

Your email address will not be published.