Tunduru yaja na mkakati mpya wa kutokomeza mimba za utotoni

Jamii Africa

Imeelezwa kuwa wasichana katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wako katika hatari ya kukatisha masomo na kutofikia ndoto zao kielimu kutokana na tatizo la mimba za utotoni kuongezeka shuleni.

Kulingana na takwimu za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, zilizotolewa wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Tunduru zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi minne ya mwanzo (Januari hadi Aprili) ya mwaka 2018, wasichana 10 walipata mimba na kuacha masomo.

Hiyo ina maana kuwa kila mwezi takribani wasichana wawili wanapata mimba. Kama hali hiyo itaendelea kwa mwaka mzima, wanafunzi wa kike zaidi ya 24 wataondolewa shuleni kwa kupata ujauzito.

Ikumbukwe kuwa rais John Magufuli alitoa tamko mwaka 2017 kwamba serikali inayoiongoza haitaruhusu wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Chanzo kikubwa cha wasichana kupata mimba kati umri mdogo katika wilaya hiyo ni kuwepo kwa mazingira yasiyo rafiki ya kusomea; upungufu wa shule, vyumba madarasa, vyoo na huduma muhimu za kijamii kama maji na umeme.

Pia umbali wa shule na makazi wanayoishi wanafunzi ni changamoto nyingine kwa watoto wa kike ambao hurubuniwa na waendesha bodaboda wakati wakitoka shuleni.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera amesema wilaya yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya shule na upungufu wa madarasa, jambo linalowakatisha tama walimu na wanafunzi kukaa shuleni.

Amebainisha kuwa wilaya yake ilikuwa na madarasa 65 ya nyasi, ambayo siyo rafiki kwa wanafunzi hasa wasichana ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kibaolojia.

Kutokana na tatizo la elimu wilayani humo, wanafunzi wa kike wanakosa ulinzi na mwishowe wanaingia kwenye tabia hatarishi ikiwemo kuanza ngono mapema.

Baada ya kujifungua mtoto hulea mtoto mwenzake

 

Nini kifanyike?

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amewaagiza watendaji wa Halmashauri ya Tunduru kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kuwapa mimba wanafunzi ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

“Niwaase wale wote wanaoshirikiana na watia mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Tunduru, mkoa hauko tayari kuwafumbia macho,nawaombeni msiwakwamishe waacheni wasome,” alisema Mndeme.

Alisema katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Tunduru inaongoza kwa  idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatiza masomo (dropout), na katika  kipindi cha Januari mpaka hadi kufikia mwezi Aprili, wanafunzi kumi (10) wamepata mimba.

Mndeme amewataka viongozi wa Tunduru kushirikiana katika kutokomeza mimba na wanafunzi wajawazito wasiendelee na shule kwa sababu serikali inatoa elimu kwa wanafunzi na siyo kwa wazazi.

Pia amewataka walimu kuwa wazazi na walezi kwa wanafunzi wao na sio vinginevyo ili kuboresha mfumo wa elimu na kutoa elimu inayozingatia usawa wa kijinsia.

“Ninaomba shule zote zilizopokea miradi kuhakikisha kuwa ndani ya miezi mitatu(siku 90) ujenzi uwe umekalimika, kama ni darasa, nyumba ya mwalimu, hosteli au matundu ya vyoo viwe vimekamilika ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kusomea kwa wanafunzI,” alisema Mndeme.

                              Elimu bila malipo, mtoto aende shule kila mdau awajibike

 

Katika kuboresha elimu mkoa wa Ruvuma umeshapokea zaidi ya bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza miundombinu ya shule za msingi na sekondari.

 

Mikakati ya Wilaya kutokomeza mimba

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera amesema halmashauri yake inaendelea kuboresha mazingira ya kusomea ili kuwawezesha wanafunzi wa kike na wa kiume kupata elimu bora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru , Chiza Cyprian Marando amesema kuwa halmashauri ilianzisha mkakati wa kuondoa changamoto ya miundombinu ya shule kwa kila kijiji kuwa na benki tofali laki moja (100,000) katika mwaka wa fedha 2016/2017, ili kuhakikisha sera ya  elimu bila malipo inafanikiwa kwa kuwashirikisha wadau  wa elimu.

Katika kutekeleza kauli mbiu ya mkoa ya “Elimu bila malipo, mtoto aende shule kila mdau awajibike” halmashauri ya tunduru ilianza kwa kuwashirikisha wadau wa elimu katika msimu wa zao la korosho mwaka 2017/2018 kwa kuanzisha mfuko wa elimu, ambapo kwa hiari ya wakulima wa zao hilo walikatwa  shilingi 30 kwa kila kilo moja ya korosho.

Fedha hizi zilipelekwa moja kwa moja katika mfuko wa elimu na  kuboresha miundombinu ya shule ambapo  milioni 608.24 zilikusanywa.

“Tumefanikiwa kununua malighafi za ujenzi kutoka viwandani kwa bei ya jumla ili kupunguza gharama, vifaa vyenye thamani ya milioni 225,251,040 ambayo ni saruji mifuko 8720,bati 3132, na nondo 880 na kuokoa shilingi milioni 36,516,000 ambazo zinaweza kujenga hosteli moja na kukamilika” alisema  Marando.

Wilaya ya Tunduru ina shule za msingi 150, ambapo 149 ni za serikali na moja ya mtu binafsi na shule za sekondari 23 ikiwa 21 ni za serikali na 2 ni za watu binafsi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *