Ubakaji unavyotumika kama silaha ya mapambano Somalia

Jamii Africa

Imebaki changamoto moja katika bara la Afrika nayo ni vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vinatokea katika nchi mbalimbali na kukwamisha ukombozi wa bara hili  kuwa huru kiuchumi na kisiasa.

Sio dhamira yangu kujadili hali halisi ya Afrika bali nazungumzia athari mojawapo ya vita ambayo inajidhihirisha katika nchi ya Somalia ambayo inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa hasa katika mji wa Mogadishu ambao unapiganiwa na serikali na makundi mengine likiwemo kundi la Al-Shabab.

Ubakaji ni moja ya vitendo vya kikatili ambavyo vimeshamiri sana katika nchi hiyo na kuwaathiri wanawake  ambao ndio wahanga wa ukatili huo, ambapo wengi wamelazimika kuikimbia nchi hiyo na kwenda uamishoni kujinusuru na usumbufu unaofanywa na kundi la kigaidi la Al-Shabab.

Ukatili wa kingono umekuwa sugu katika nchi ya Somalia. Miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuangushwa kwa dola mara kwa mara kumesababisha idadi kubwa ya watu kutawanyika katika maeneo mbalimbali. 

Kutokana na hali hiyo taasisi na mashirika ya serikali yanayotakiwa kuwalinda wanawake na hatari hiyo nayo yameshindwa kufanya kazi na kukabiliwa na changamoto mbalimbali za utendaji. Wanawake waliopo katika kambi za wakimbizi na jamii za watu wanaoishi pembezoni mwa nchi pia wako katika hatari hiyo.

Tangu mwaka 2013, Umoja wa Mataifa umeripoti zaidi ya kesi 800 za ukatili wa kingono na kijinsia katika mji wa Mogadishu pekee. Idadi halisi ya waathirika ni kubwa kuliko takwimu zinazotolewa.

Waathirika wengi hawaripoti vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa kwasababu ya kukosa ujasiri, kutofikiwa na  huduma za afya na sheria, pia unyanyapaa na kuogopa aibu kwa jamii inayowazunguka kwa vitendo vya ubakaji.


“Katika kambi yetu kila tulipomuona mtu tulizoea kusema ‘habari yako’ lakini sasa kila tukionana tunaulizana ‘umebakwa leo?’” – Maryam.


Kwa mujibu wa Shirika la watoto (UN Chidren’s Fund), robo tatu ya waathirika wa ukatili wa kingono katika nchi ya Somalia ni watoto. Matokeo yake, wanawake na wasichana wadogo kwa mujibu wa mtaalamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu anasema wanakabiliwa na uathirika wa aina mbili ‘double victimazation’ – ambao ni kubakwa na kushindwa kwa mamlaka za serikali kutoa huduma bora za afya, misaada  ya kisheria na huduma za jamii.

Serikali ya Shirikisho ya Somalia ambayo ilianzishwa Agosti 2012 inategemea misaada ya Kimataifa na kijeshi kutoka kwa Umoja wa Afrika katika programu yake ya kutunza amani ya AMISOMI. Kutokana na kuwa nguvu ndogo ya kijeshi inatawala eneo dogo la mji mkuu wa Moghadishu hivyo kushindwa kuthibiti vitendo vya ubakaji kwasababu ya kukosa mamlaka kamili katika nchi hiyo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu (Human Right Watch) likishirikiana na wadau wa maendeleo lilifanya utafiti ulioitwa  katika nchi hiyo na kuandaa  mapendekezo mbalimbali ya kushughulikia suala hilo.

Utafiti huo ni muendelezo wa ushirikiano wa nchi hiyo na jumuia za Kimataifa kutokomeza ubakaji, ambapo mwaka 2013 serikali ya Somalia ilisaini itifaki ya pamoja na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa ili kutafuta njia mbadala za kumaliza tatizo hilo na kulifanya suala hilo kuwa moja ya kipaumbele muhimu katika mipango ya serikali.

Lakini serikali hiyo bado haijathibitisha kuchukua hatua za makusudi kuwazuia baadhi ya watu walioko katika vyombo vya usalama kutofanya vitendo hivyo na kuwaajibisha kisheria.

Shirika hilo lilimuhoji mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Maryam (37) ambaye alisema usiku mmoja kabla ya kuhojiwa na Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu, alimsikia mwanamke akishambuliwa na wanaume ambapo alikuwa na watoto sita katika mji mkuu Mogadishu. Tukio hilo lilimrudisha nyuma katika siku aliyofanyiwa ukatili wa kingono.

Maryam alisema ubakaji umekuwa ni tabia sugu katika kambi iliyoko wilaya ya Wadajir na hali ya wanawake ni mbaya kwa sababu na yeye alibakwa hapo hapo mwaka 2012.

Maryam anasema wakati anabakwa kwa mara ya kwanza alikuwa na ujauzito wa miezi mitano na alikuwa amelala katika kambi iliyopo wilaya ya Wadajir.

 “Wanaume wanne wote walinibaka wakati mmoja wao alikaa nje akilinda. Niligombana na mwanaume wa mwisho lakini alinipiga kwa kitako cha bunduki yake. Nilipiga kelele lakini hakuna mtu aliyekuja kunisaidia”.

Siku iliyofuata, Meneja wa kambi alikwenda kumuangalia kwasababu taarifa za kubakwa kwake zilienea katika kambi yote. Alichukuliwa mpaka kituo cha polisi ambako alidai kuwa mmoja wa wabakaji alivalia sare za polisi.

“Nilianza kutoka damu mfululizo ukeni”.

 “Waliniambia niende nyumbani na waliniamuru nioshe sakafu ambayo ilikuwa imetapakaa damu kabla sijaondoka na ndipo nilisafisha sakafu”.

Maryam hakurudi tena kituo cha polisi kufuatilia kesi yake, akihofia wabakaji wanaweza kuja tena na kumfanyia kitu kibaya zaidi. Baada ya muda mfupi mimba ya Maryam ilitoka na miezi mitatu baadaye alibakwa tena katika nyumba yake na kundi lingine la waharifu.

 Katika ripoti ya Shirika la Kimatifa la Haki za binadamu yenye kichwa  ““‘Here, Rape is Normal’: A Five-Point Plan to Curtail Sexual Violence in Somalia,”’  inaeleza kwa undani shuhuda za wanawake waliobakwa tangu serikali ya Shirikisho ya Somalia ianzishwe mwaka 2012.

Ripoti hiyo ilitazama tatizo hilo katika mji mkuu wa Mogadishu na wilaya ya Benadir, maeneo ambayo serikali inadhibiti na ambako mashirika ya kimataifa yanachunguza rasilimali muhimu za kuimarisha usalama na kuunda upya taasisi za  serikali ikiwemo vyombo vya sheria na huduma za afya.

Wakati rais Hassan Sheikh Mohamud akiingia madarakani aliahidi kutoa kipaombele katika usalama na haki, katika hali halisi ni sehemu ndogo ya juhudi hizo zimefanyika kutatua changamoto ya ubakaji na udhalilishaji wa kingono hasa kwa makundi na jamii zilizo katika hatari ya kukumbwa na vitendo hivyo.

Ripoti hiyo imeainisha mapendekezo matano ambayo yataisaidia serikali, wafadhili na mashirika mengine kuwa na mikakati endelevu ya kitaifa kupunguza udhalilishaji wa kingono, kuwapatia waathirika msaada wa haraka na kutengeneza mpango wa muda mrefu katika  kumaliza tatizo.

Njia ya kwanza ni kuimarisha usalama katika kambi za wakimbizi, kwa sababu wanawake wengi wanabakwa nyakati za usiku. Doria za usiku ambazo zitahusisha askari na wananchi zitasaidia kubaini waharifu na kuwalinda wasichana na wanawake wasivamiwe na kufanyiwa vitendo hivyo vya kidharimu.

Pia uboreshaji wa vituo vya dharura vinavyotoa huduma za afya, ambapo vifaa tiba na madawa yote yapatikane kwa wakati ili kuwasaidia wanawake ambao wanakumbwa na kadhia hiyo. Pia uanzishwaji wa madawati ya kijinsia ambayo yatasaidia kutoa elimu na ushauri na nasaha kwa wasichana. Hili linaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara na huduma za jamii ili kuwasaidia wahanga hao kufika kwa wakati katika vituo hivyo.

Kuhakikisha kunakuwa na taasisi imara zenye kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi. Msaada huo utasaidia wananchi kuelimika na kutambua athari za ubakaji, ambapo vyombo vya usalama vimetakiwa kudumisha umoja na ushirikiano na wananchi wanaoishi katika makambi ya wakimbizi.

Serikali imetakiwa kutunga sera na sheria mathubuti ambazo zitatekelezwa kikamilifu kupambana na vitendo vyovyote vya ubakaji. Zaidi ya hapo ni kufufua usawa wa kijinsia ambao kwa muda mrefu umekuwa changamoto, na wanawake nchini Somalia hawathaminiwi na kupewa haki zao za msingi ikilinganishwa na wanaume.

Somalia yenye neema iliyo na amani na utulivu inawezekana, ikiwa kila mwananchi na jumuiya za kimataifa kushirikiana kutokomeza vitendo vyote vya kibaguzi na kikatili ambavyo vinazuia nchi hiyo kupata maendeleo yaliyokusudiwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *