Uchaguzi wa marudio Kenya: Vurugu zatawala, wengi wajifungia nyumbani

Jamii Africa

Vurugu na idadi ndogo ya wapiga kura katika vituo imeshuhudiwa katika uchaguzi wa marudi nchini Kenya, Tume Huru ya Uchaguzi  na Mipaka (IEBC)  imeahirisha uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo hadi Oktaba 28 mwaka huu.

Uchaguzi huo wa marudio wa rais unafanyika baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8 mwaka huu kumpa ushindi rais Uhuru Kenyatta  kufutwa na Mahakama Kuu kutokana na udanganyifu uliojitokeza katika Tume Huru  ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Taarifa kutoka Kenya zinaeleza kuwa vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 12 asubuhi lakini katika vituo vingi watu hawakujitokeza kupiga kura wakihofia fujo za waandanamaji wa Muungano wa NASSA unaongozwa na Raila Odinga ambao waliandamana katika maeneo mbalimbali kupinga marudio ya uchaguzi huo.

Kutokana na vurugu zilizojitokeza katika maeneo ya Kisumu, Homabay, Slaya na Migori, uchaguzi katika maeneo hayo umehairishwa.  Mwenyekiti wa Tume ya IEBC, Wafula Chibukati ametangaza kuwa  maeneo hayo yatafanya uchaguzi siku ya 28 Oktaba mwaka huu.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo amewataka wananchi wa Kenya kuwa watulivu wakati Tume hiyo ikiendelea na zoezi la kupokea matokeo kutoka katika vituo mbalimbali. Pia Polisi wametakiwa kuimarisha dolia ili kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani.

Mapema mwezi huu, Odinga alitangaza kujitoa katika marudio ya uchaguzi kwa madai kuwa uchaguzi huo usingekuwa huru na wa kweli. Aliwatuhumu wafanyakazi wa IEBC kwa kuvuruga uchaguzi mwezi Agosti huku akiwataka kujiuzuru na kuwapisha watu wengine waongoze uchaguzi wa marudio.  

Licha ya malalamiko hayo IEBC iliendelea na maandalizi ya uchaguzi wa marudio na siku ya leo imesimamia zoezi hilo la kupiga kura kwa masaada wa vyombo vya dola. Lakini zoezi hilo limeshuhudia idadi ndogo ya watu kwenye vituo vya kupigia kura ambapo watu wengi walibaki nyumbani wakihofia vurugu.

Shughuli nyingi za kiuchumi ukiwemo usafiri, biashara zimesimama ili kupisha uchaguzi huo ambao umeripotiwa kukumbwa na vurugu katika maeneo yanayosemakana kuwa ni ngome za NASA.  Katika kuonyesha hisia zao magenge ya vijana yalijitokeza na kuingia barabarani kupinga marudio hayo.

Katika maeneo ya Kisumu, Migori na Homabay, askari walikabiliana na waandamanaji ambao waliingia barabarani,  kuweka vizui na kuchoma mataili ya magari. Kulingana na gazeti la Daily Nation limelipoti kufa kwa watu 3 na wengine 8 kujeruliwa na kukimbizwa hospitali zilizo katika miji hiyo.

Katika Kaunti ya Kitui ambayo inatajwa kuwa ngome ya Odinga asilimia 19 ya watu wamejitokeza ikilinganishwa na idadi ya watu waliojiandikisha katika uchaguzi huo. Siku moja kabla ya uchaguzi wa leo, Odinga aliwataka wafuasi wake kususia uchaguzi huo na kukaa nyumbani wakisubiri tamko la muungano huo wa NASA baada ya uchaguzi.

Lakini hali imeoneka kuwa tofauti katika ngome inayoaminika kuwa ni ya Chama cha Jubilee kinachongozwa na rais Uhuru Kenyatta ambapo watu wengi wamejitokeza kupiga kura lakini idadi hiyo sio kubwa ikilinganishwa na uchaguzi wa awali wa Agosti.

Katika kaunti ya Nyeri inaripotiwa kuwa watu wamejitokeza kwa wingi kupiga kura na hadi kufikia nyakati za jioni wengi walikuwa wamepiga kura tayari. Huko jimbo la Eldoret watu wengi wamejitokeza wakiongozwa Mgombea Mwenza wa Jubilee, William Ruto ambaye alipiga kura yake mapema leo asubuhi. Naye Rais Uhuru Kenyatta alipiga kura katika shule ya msingi Mutomo eneo jimbo la Gatundu.

Uchaguzi Mkuu wa Kenya ulifanyika Agosti 8, mwaka huu ambapo rais Kenyatta alichuana vikali na mpinzani wake Raila Odinga na kumshinda. Siku chache baadaye Odinga lipinga matokeo hayo mahakamani na uchaguzi wa urais ukafutwa na kupangiwa tarehe ya leo.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2007 Kenya ilifanya uchaguzi wa rais lakini matokeo yalipotoka na kumpa ushindi Mwai Kibaki, nchi hiyo ilitumbukia katika machafuko ambapo watu  zaidi ya 1100 walikufa na kuwaacha wengine 600,000 wamekimbia makaazi yao na rais Uhuru Kenyatta na William Ruto kupelekwa mahakama ya kimataifa ya uharifu (The Hague).

Machafuko hayo yalipelekea nchi hiyo kufanya mabadiliko katika katiba yake ili kuwa na uchaguzi huru na kweli. Katiba hiyo ya Kenya inatajwa kuwa ni miongoni mwa katiba bora barani Afrika baada ya ile ya Afrika Kusini.

Kwa mara ya kwanza Kenya imeweka historia ambapo muhimili wa mahakama una nguvu kisheria. Kutokana na uhuru huo wa mahakama,  Jaji Mkuu David Maraga alitengua matokeo ya urais ya Agosti 8 mwaka huu yaliyompa ushindi rais Uhuru Kenyatta ambaye anagombea kipindi cha pili na cha mwisho.

 

 

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *